Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Jerry Silla amesema ubunifu wa kidigitali ndio njia pekee itakaowezesha vijana kujiajiri na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Ameyasema hayo leo Septemba 19, 2024 katika kongamano la mashindano ya ubunifu wa teknolojia (US-Tanzania Tech Challenge 2024) yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Marekani lililofanyika jijini Dar es Salaam.
“Tungependa vijana wajiajiri, wanaposoma Tehama, sayansi ya kompyuta, au uhandisi wa kompyuta. Lengo ni kutengeneza teknolojia inayoweza kutumika kutaua matatizo, kwa mfano kuna watu waligundua hii M-Pesa inayotumika na jamii nzima kutuma na kupokea pesa,” amesema.
Amesema mbali na teknolojia kuwezesha vijana kujiajiri, itarahisisha utoaji wa huduma za jamii na biashara.
“Sisi ni wizara wezeshi, kwa mfano leo utoaji wa huduma za afya, inaeleweka kwamba ni mgonjwa akutane na daktari, lakini kupitia Tehama, daktari anaweza kuwa Dar es Salaa akatoa huduma Kagera au Mtwara. Leo mkulima wa kahawa Kagera au mkulima wa korosho Mtwara anaweza kutumia Tehama kupata mnunuzi ndani na nje ya nchi,” amesema.
Naibu Balozi wa Marekani nchini, Andrew Lentz amesema idadi kubwa ya waombaji inaonyesha kuwa Tanzania kuna mwamko wa ubunifu wa kidigitali.
“Ni mashindano ya kihistoria kwa sababu tumekuwa tukiendesha mashindano haya maeneo mbalimbali duniani lakini kwa Tanzania imetoa idadi kubwa ya maombi ya ubunifu wa kidigitali. Wengi wao ni vijana chini ya miaka 45 wanawake kwa wanaume. Tanzania ina mwamko mkubwa wa ubunifu wa kiteknolojia,” amesema.
Miongoni mwa washindani waliotuma maombi ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Hamasa Media Group, Baraka Kiranga aliyesema kampuni hiyo kampuni yao inaendana na kukua kwa sekta ya habari.
“Miaka10 iliyopita tumeshuhudia ongezeko la vyombo vya habari kwa mfano kuna vituo vya televisheni 60, magazeti zaidi ya 300 na redio zaidi ya 200. Sasa vyombo vya habari vinapokuwa vingi kunakuwa na haja ya kuzichakata taarifa hizo ili kuiwezesha Serikali na wadau mbalimbali kupata taarifa wanazoweza kuzifanyia kazi wakiwa na ushahidi.
“Tuna uwezo wa kuchakata taarifa za vuyombo vya habari 100 wa wakati mmoja na kutoa taarifa za kiinteljensia kwa wadau wanaotumia habari kufanya maamuzi yao. Tumeanzia hapa Tanzania na baadaye tutahamia nchini Kenya na Zimbabwe,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa maudhui kutoka The Launchpad Tanzania, Warda Mansour amesema wameshiriki mashindano hayo ili kukuza ushiriki wa vijana na wanawake katika matumizi ya mitandao ya jamii.
“Tunafurahi kushiriki kwenye mashindano haya, kwa sababu tumepata fursa ya kuonyesha uwezo wetu kwenye masuala ya ushiriki wa wananchi. Kuna programu ya Sauti Zao tuliyoianzisha inayomruhusu kijana kutoa maoni kwa matatizo wanayokumbana nayo katika jamii,” amesema.