Dar es Salaam. Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe amewataka wataalamu wa mifugo nchini kuwa mstari wa mbele kuzuia usambazaji wa magonjwa ya mifugo kushambulia binadamu ili kuisaidia Serikali kutotumia fedha nyingi kutibu magonjwa yanayozuilika.
Amesema kuzuia magonjwa ya wanyama kwenda kwa binadamu ni rahisi kuliko matibabu ambayo huhitaji fedha na muda mwingi.
Profesa Shemdoe ameyasema hayo leo Septemba 19,2024 jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya miezi minne yaliyoratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) yakilenga kuwezesha wataalamu wa mifugo kubaini, kuzuia na kurekodi magonjwa ya wanyama yaambukizwayo kwa binadamu.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa wataalamu wa mifugo, kutibu magonjwa ya mifugo kwa binadamu tunatumia fedha nyingi kuliko kuyaangalia magonjwa haya mapema.
“Ni muhimu kuwa mstari wa mbele kuzuia magonjwa haya kwenda kwa binadamu kufanya hivyo tutakuwa tumesaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali ambazo zingetumika kwenye matibabu,” amesema.
Hoja hiyo inafafanuliwa na Mratibu wa Mafunzo ya Epidemiolojia na Usimamizi wa Maabara wa Wizara ya Afya Dk Rogath Kishimba akisema, chanjo ya mifugo gharama yake ni ndogo lakini ugonjwa ukihamia kwa binadamu kutoka kwa mnyama gharama ya matibabu ni kubwa.
Akitolea mfano wa kichaa cha mbwa, Dk Kishimba amesema chanjo hiyo huchanjwa mbwa kwa Sh2,000 lakini mtu anapong’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo hulazimika kupata chanjo nne ambazo hutolewa kwa Sh30,000 hadi Sh60,000 kwa dozi moja.
Profesa Mdoe amewataka wataalamu hao kutumia mafunzo waliyopata kuchanja mifugo ili Tanzania iendelee kukuza soko la nyama kimataifa, kwani tayari kuna nchi inaangalia uwezekano wa kuagiza tani 54,000 za nyama kutoka nchini.
Kwa upande wake Dk Kishimba amesema mtu anapopatwa na kichaa cha mbwa na kuanza kuonyesha dalili, uwezekano wa kupona kwake ni mdogo.
“Ukiwa na wagonjwa 100 ni wastani wa wagonjwa wawili pekee ndio wanaweza kupona au wote wasipone kabisa, ndio maana tunasisitiza muhimu kuadhibiti, yakiwa kwa wanyama ni nafuu kutibu na kuzuia,” amesema.
Naye, Mkurugenzi wa huduma za mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Benezeth Lutege amesema katika kuongeza upatikanaji bora wa chanjo, Serikali imeondoa kodi ya chanjo za mifugo zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
“Chanjo na dawa za mifugo nchini zinaingizwa bila kodi, kwahiyo gharama za chanjo tunategemea zitakuwa ndogo. Pia, tuna chanjo ya mbwa tunatarajia kuzalisha na ipo katika hatua mbalimbali za uzalishaji na huenda hadi 2030 tutakuwa tumeanza kuzalisha, pia tumeandaa mkakati wa kutokomeza kichaa cha mbwa 2024 hadi 2028 na tumeshawasilisha Shirika la Nyama Duniani,” amesema.
Mkakati huo utakapopitishwa utaipa Tanzania nafasi ya kuanza kupokea chanjo ya kichaa cha mbwa kutoka kwenye shirika hilo.
Kwa hali ilivyo, mtaalamu wa mifugo kutoka Masasi Innocent Mrope amesema katika watu 300 walio na umri wa miaka 18 na kuendelea waliowafanyia utafiti katika vijiji 15 wilayani hapo, asilimia 54.6 hawana uelewa kuhusu kichaa cha mbwa na asilimia 32.3 walikuwa na mtazamo hasi kuhusu tatizo hilo.
Amesema ni muhimu wilaya hiyo ikajikita kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kichaa cha mbwa kwani asilimia 14 pekee ndio wenye mtazamo chanya kuhusu ugonjwa huo, wengi wao wanapopata tatizo linalohusisna na ugonjwa huo hawaamini kupona kupitia matibabu au kuchanja mbwa wao.
Akizungumzia wahitimu wa mafunzo hayo, Mratibu wa Programu FAO Mosses Ole Neselle amesema wataalamu wa mifugo waliowezeshwa mafunzo hayo ni 30 kutoka Tanzania bara 20 na Zanzibar 10.
Amesema mafunzo hayo ni muhimu kwasababu magonjwa ya wanyama yanahatarisha usalama wa chakula duniani na kuzorotesha uchumi wa nchi.
Wataalamu waliojengewa uwezo wanaweza kukusanya taarifa, kufanya utafiti wa magonjwa ya mlipuko na kubaini viashiria vya magonjwa.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Magonjwa ya Wanyama Duniani asilimia zaidi ya 70 ya magonjwa yanayotokea duniani ni kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Magonjwa yanayoambukizwa binadamu yatokayo kwa wanyama ni mafua ya ndege, kichaa cha mbwa, marburg ugonjwa wa Ebola na MPox.
Kuna zaidi ya magonjwa 200 yanayohusishwa na wanyama kuhamia kwa binadamu, hii ikiwa na maana kwamba magonjwa 6 kati ya 10 ya kuambukiza ambayo huathiri watu husambazwa na wanyama, ikiwa ni pamoja na wanyama wafugwao nyumbani hiyo ni kwa mujibu wa Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC).
Tovuti ya National Library of Medicine ya nchini Marekani inaonyesha magonjwa yahamayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu, yameripotiwa matukio bilioni 2.5 vifo milioni 2.7 vikishuhudiwa.