Monduli. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kushughulikia mgogoro wa ardhi katika Mlima Lendikinya.
Mgogoro huo unawahusisha wananchi 3,000 ambao wanadaiwa kuvamia eneo hilo.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga akizungumza mbele ya Waziri Mchengerwa leo Alhamisi Septemba 19, 2024, amedai msitu huo umevamiwa na wananchi 3,000 ila wameshindwa kuutatua kwa madai kuwa kuna kigogo (hakumtaja jina) alipewa hati miliki katikati ya msitu huo na Serikali ya wakati huo.
Hivyo, Waziri Mchengerwa akamtaka Makonda kufanyia kazi mgogoro huo na kama atakakwama amjulishe ili nguvu zaidi iongezwe.
“Mimi siogopi mtu, hata kama ni big fish, mbele ya sheria na haki hakuna huyu ni mtu mkubwa au alikuwa mtu mkubwa, lazima sheria ifuate mkondo wake,” amesema waziri huyo.
Hayo ameyasema leo akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi na kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.
Mchengerwa amesema hatakubali kuona mwananchi mnyonge akidhulumiwa haki yake na kama wataamua kuwaondoa wananchi katika eneo hilo, hata huyo kigogo naye aondoke.
“Kama yeye wanamuacha basi na hawa wananchi pia waacheni na mfanye utaratibu wa kuligawa eneo hilo kwa wananchi,” amesema Mchengerwa na kuongeza;
“Kuhusu uvamizi wa msitu, sina uhusiano na papa wala nyangumi. Mkuu wa mkoa, umelisikia hili; anza kulifanyia kazi kwa sababu nimekupa baraka zote. Siwezi kukubali hali kama hii inayowafanya baadhi ya Watanzania hawana nafasi sawa. Hakuna kusema huyu ni nyangumi au papa katika kipindi changu, huyo hayupo,” amesema.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewaelekeza wawasaidie wanyonge, hao manyangumi na mapapa ndiyo wanapaswa kushughulika nao.
“Kama mnaona hamuwezi kumuondoa huyo mtu, ni bora muondoe wananchi maskini. Ni bora wananchi wote wabaki kwenye eneo hilo kuliko kuacha tajiri pekee, na kama mnaona hamtaweza, ni bora mgawanye eneo hilo kwa wananchi wote,” ameongeza.
Waziri Mchengerwa amesema, “Hamuogopi mtu yeyote. Kama mtu hafuati utaratibu, anapaswa kuondolewa. Haki ndiyo msingi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Taifa lilipitisha misingi hii, hivyo lazima iendelezwe.”
“Yule ambaye anaona misingi hii haimfai na ni kiongozi, akae pembeni mapema. Nitashughulika naye mapema na sitasita kumchukulia hatua,” amesema.
Mkuu wa Wilaya alitoa taarifa kwamba, kufuatia maelekezo ya Makonda kwa wakuu wa mikoa kuhusu kutatua migogoro, wameweza kushughulikia migogoro sita lakini hawajafanikiwa kutatua mgogoro mmoja.
“Tatizo kubwa ni kwamba serikali ilimpa hati mtu katika eneo la msitu wa serikali, jambo ambalo limeleta ugumu kwa kuwa yule mtu ni “big fish” ambaye alikuwa RC na Mwenyekiti wa Mkoa. Hati hiyo inafanya iwe vigumu kuwahamisha wananchi,” amesema.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Mkoa Makonda amesema akiwa kwenye ziara wilaya za Mkoa wa Arusha, aliwapa wakuu wa wilaya miezi mitatu kutatua migogoro ya ardhi na kuwasilisha taarifa kwake.
Hata hivyo, amedai kuna baadhi ya watendaji wa Serikali wanatengeneza leseni za kughushi na atatoa majina kwa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa uchunguzi. Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) utasaidia kupunguza mianya ya rushwa.
“Katika Mkoa wa Arusha, watu wanatafuta maisha kwa njia zisizo za halali, kama kuunda leseni feki. Tunawaomba Takukuru tusaidie, kwani baadhi ya wafanyabiashara wanapewa leseni ambazo hazikubali kwenye mfumo,” amesema Makonda.