AKILI ZA KIJIWENI: Aggrey Morris anafuata njia za Aliou Cisse

KABLA ya mafanikio ya kufundisha timu ya taifa ya Senegal, Aliou Cisse alianzia kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya nchi hiyo chini ya umri wa miaka 23.

Ingewezekana Cisse angekimbilia moja kwa moja kufundisha kikosi cha wakubwa cha Senegal lakini kuanza kwa watoto ilikuwa njia sahihi ya kufikia ndoto zake za kuwa kocha mkubwa ndani na nje ya Afrika.

Kwanza timu za watoto hazina presha kubwa hivyo inampa uhuru kocha kuonyesha uwezo wake wa kufundisha timu pamoja na mchezaji mmojammoja tofauti na timu za wakubwa ambazo muda wote huwa zinahitaji matokeo mazuri.

Lakini timu za vijana ndio jukwaa sahihi kwa kocha ambaye bado hajajenga wasifu mzuri katika taaluma hiyo kuanzia ili apate uzoefu ambao utamsaidia siku za baadaye pindi atakapopata fursa ya kufundisha vikosi vya wakubwa.

Nimemkumbuka Cisse baada ya kuona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limempatia fursa ya kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15.

Aggrey Morris ni jina kubwa katika soka la Tanzania na amecheza kwa mafanikio makubwa katika kikosi cha Azam FC na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, pia ana leseni ya ukocha ngazi B ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Wasifu huo unatosha kumfanya Aggrey Morris kupata timu ya kufundisha ya wakubwa kwa vile analifahamu soka kwa undani akiwa ni mchezaji mwandamizi pia kwa kulisoma darasani kama mahitaji ya mchezo huo yanavyotaka.

Hata hivyo, jamaa ameamua kuanza na kufundisha watoto ili kumjenge na kumpatia uzoefu zaidi katika safari ya ndoto zake za kuwa miongoni mwa makocha wazuri kuwahi kutokea hapa nchini.

Tuendelee kumuombea heri na mafanikio Aggrey Morris huenda baada ya kumshangilia na kumheshimu akiwa mchezaji mkubwa, tutamuimba akiwa kocha mkubwa.

Related Posts