Hapatoshi maandamano ya Chadema, wadau wacharuana

Dar es Salaam. Kufuatia hali ya sintofahamu ya demokrasia nchini, baadhi ya wadau wa siasa na demokrasia wametaka kuwepo kwa mazungumzo ya kutafuta mwafaka miongoni mwa vyama vya siasa.

Mazungumzo hayo yameshauriwa yafanyike ili kurejesha hali ya maridhiano katika kipindi ambacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamepanga kufanya maandamano Jumatatu ya Septemba 23, 2024.

Chadema wamepanga kufanya maandamano hayo kuishinikiza Serikali kueleza walipo wanachama wake wanaodaiwa kutekwa. Pia, kupinga tukio la aliyekuwa kada wake, Ali Kibao kutekwa na watu wenye silaha akiwa kwenye usafiri umma na kisha kuuawa.

Ushauri hao wa kufanyika kwa meza ya mazungumzo baina ya Serikali na wadau wa siasa hususan wa upinzani,  umetolewa leo Alhamisi, Septemba 19, 2024 katika mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) uliowakutanisha wadau kujadili tathmini ya hali ya demokrasia nchini.

Miongoni mwa wadau walioshauri hilo ni Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, wenyeviti wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), John Cheyo (UDP), Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi-Bara, Joseph Selasini na  Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu.

Mkutano huo ulioandaliwa na TCD ambayo kwa sasa inaongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema umekutanisha wadau mbalimbali kujadili, kutoa ushauri na mapendekezo na utahitimishwa kesho Ijumaa.

Alichokisema Jaji Warioba

Akizungumza kwenye mkutano huo, Jaji Warioba aliyekuwa mgeni rasmi amesema kuna matatizo mengi yanatokea, lakini pande zinazosigana hazikutani kuzungumza ili kutafuta suluhisho la changamoto zao.

Jaji mstaafu Joseph Warioba

Alitoa mfano wakati ule Chadema wakiandaa maandamano kupinga sheria tatu kupitishwa na Bunge, alisema alimtafuta Katibu Mkuu wa chana hicho, John Mnyika ili afahamu tatizo lilipo.

Baada ya siku chache, alisema alikutana na viongozi wa Chadema waliomtembelea nyumbani kwake na kuzungumza nao.

Alisema baada ya kuwasikiliza, aliutafuta upande wa pili ambapo alizungumza na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana ambaye alimweleza Rais Samia ametoa hakikisho kwamba mambo yatakuwa mazuri kwenye chaguzi zijazo.

“Tunayo matatizo lakini hatukutani kuzungumza. Kila mtu anatumia madaraka yake badala ya kukaa na kushauriana,” alisema Jaji Warioba, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Jaji Warioba alisema kuna wakati fulani Msajili wa Vyama vya Siasa alisikia tamko la kiongozi mmoja wa kisiasa, akaona dalili za uvunjifu wa amani, akazuia mkutano huo uliokuwa ufanyikie jijini Mbeya. Ulikuwa mkutano wa vijana wa chama hicho (Bavicha) na Jeshi la Polisi nalo likatangaza kuzuia mkutano huo.

Hata hivyo, alihoji kwa nini Msajili wa Vyama vya Siasa hakuwaita Chadema na kuzungumza nao kwa kuwa moja ya majukumu yake ni kuwa mlezi wa vyama.

Waziri mkuu huyo mstaafu amesema hali hiyo inaongeza ukubwa wa tatizo badala ya kutafuta suluhisho.

“Hivi hakuna njia ya mashauriano? Kwa mapambano hamuwezi kuleta suluhisho. Bado muda mfupi tunakwenda kwenye uchaguzi. Viongozi wote wanaohusika tuwe tumekubaliana la sivyo tukienda na mapambano haya tuliyonayo inaweza kujenga misingi ya vurugu nchini,” amesema.

Katika msisitizo wake, Jaji Warioba amesema:”Tukienda kwenye uchaguzi bila makubaliano, zitatokea vurugu, mambo haya ya uchaguzi yanasababisha vurugu. Yaliyotokea mwaka 2001 bado yanapita kichwani, nisingependa yatokee tena:”

Katika maelezo yake, Jaji Warioba amekumbuka kipindi ambacho alihoji mwingiliano wa mihimili ya Bunge, Mahakama na Serikali jambo ambalo amesema halipo sawa kiutendaji, walijibiwa kuwa wanawashwa.

Msingi wa hoja ya Jaji Warioba ilikuwa ni kuonyesha namna mihimili hiyo inavyopaswa kufanya kazi pasi na kuingiliana.

“Nadhani mwaka 2016/17 baadhi yetu tulitoa ushauri kwa wanaoanza kufanya hivyo, ilifikia kiongozi wa Mahakama na Bunge wakawa wanahudhuria vikao vya Rais.

“Viongozi wa mihimili hiyo siyo kama hawakutani bali wanapaswa kukutana kwa njia maalumu mfano kwenye uapisho, lakini katika kazi zao za kawaida hawachanganyiki. Mkiwaleta pamoja watu wataanza kuwa na wasiwasi.

“Na tuliposema tukaambiwa hawa wazee nao wanawashwa washwa. Lakini, si vizuri wakuu hao kukutana kwenye vikao kwani ikitokea wakawa na mawazo tofauti inakuwa na matatizo yake pia,” amesema Warioba.

Hoja hiyo ya mazungumzo ilizungumzwa katika jopo la majadiliano, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kwa hali ya demokrasia ilivyo sasa nchini, yakiitishwa maandamano yanaweza kuleta machafuko na kusababisha watu kukimbia nchi kama ilivyotokea mwaka 2001.

Kauli ya Profesa Lipumba imekuja wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeshatangaza maandamano yatakayofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 23, 2024 kwa lengo la kupinga matukio ya utekaji na mauaji nchini. Hata hivyo, Polisi imeyapiga marufuku.

Profesa Lipumba amekumbusha maandamano yaliyofanywa na CUF mwaka 2001 na kuzalisha wakimbizi kutoka Kisiwa cha Pemba waliokimbilia Mombasa nchini Kenya.

“Mimi nina uzoefu wa masuala haya yalitokea mwaka 2001, tuliitisha maandamano hayo, matokeo yake watu walipoteza maisha, tukazalisha wakimbizi. Mpaka sasa bado inaniletea matatizo,” amesema.

Ameishauri Chadema na vyombo vya dola kujadiliana masuala hayo kabla hayajaleta maafa. 

“Kwa uzoefu nilionao na kwa kutazama vyombo vya dola vilivyo, Mheshimiwa Mbowe, nakuona hapa nakuelewa msimamo ulionao, lakini ni muhimu tutazame yale maoni ambayo Mzee Warioba ameyatoa, tufanye mazungumzo na majadiliano.

“Waziri wa Katiba na Sheria (Profesa Palamagamba Kabudi), tufanye majadiliano na mazungumzo mambo haya yasiharibike zaidi. Ni muhimu wenzetu wa dola wawe wepesi wa kusikiliza na kuchukua haya yanayopendekezwa na wengine ili tuyafanyie kazi,” amesema.

Amevitaka vyombo vya dola kufanya mazungumzo na wanasiasa kuliko kukimbilia kupambana.

“Tukienda katika hali hii tukaenda kwenye maandamano na vyombo vyetu vya dola vilivyo tunaweza kujikuta tunaingia kwenye hali ngumu zaidi ya kupoteza wananchi wengi katika nchi yetu. Mimi mambo haya niliyaona Zanzibar,” amesema.

Akitoa tathmini kuhusu hali ya demokrasia nchini, Profesa Lipumba amesema imeporomoka.

“Kwa kweli demokrasia imeporomoka. Hata ile kazi kubwa, yale mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba tuliacha hatukufanya mwendelezo,” amesema.

Amesema hata ulipofanyika mkutano wa vyama vya siasa Desemba 2021, suala la kufufua upatikanaji wa Katiba yenye misingi ya demokrasia halikuzungumzwa.

“Kwa kipindi cha 2015 hadi 2020 kulikuwa na matukio yaliyoturejesha nyuma sana kidemokrasia,” amesema Profesa Lipumba, akidai kuwepo kwa makada wa chama hicho waliopotea mpaka leo hawajapatikana.

“Kwa hali ilivyo sasa na unyeti wa mambo yalivyo sasa, ni muhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa kukutana na kuyajadili kuchukua yote yaliyotolewa na mapendekezo yote yaliyotolewa tuweze kuona tunapata njia gani.

“Najua wenzetu wa Chadema mlifanya mazungumzo, unajua ukishagongwa na nyoka kidogo, hata ukiuona ukamba kidogo unakuwa unashtuka, lakini kwa sisi ambao hatujapata fursa hiyo tushiriki ili tuokoe jahazi letu,” amesema.

‘CCM haifurahii matukio haya’

Hoja ya kufanya mazungumzo iliungwa mkono na Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu aliyesema hakuna mwanachama wa CCM anayefurahia matukio ya watu kutekwa na kuuawa, akisema matukio hayo yapo duniani kote.

“Katika kipindi hiki panapojitokeza changamoto tunakaa pamoja tunajadiliana tunatafuta suluhisho. Sina maana kwamba kuna mwana CCM anaweza kufurahia jambo la mtu fulani kuumizwa katika mazingira ya kutekwa na kumuua mtu,” amesema.

Amesema mazingira ya sasa yanafanana na wakati wa baada ya vita vya kwanza na vita vya pili vya dunia.

“Tumeshuhudia juzi pale Israel wametekwa watu na kuuawa zaidi ya watu 1,000 nina takwimu, Uingereza peke yake wamepigwa risasi watu 109, Marekani wameuawa watu 48,000 kwa bunduki.

“Sijasema kwamba ni halali watu kutekwa na kuuawa, ila panapotokea changamoto hizo, tukae pamoja tujadiliane sio kunyoosheana vidole.

“Taifa linapofika hali hii tuiteni tukae chini tuambiane, Serikali mnakosea hapa, vyama mnakosea hapa, tunataka tujenge mustakabali wa Taifa letu, tusiligawe Taifa vipande vipande,” amesema.

Kauli hiyo pia imeungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini ambaye alikwenda mbali akiitaka Chadema isitishe maandamano inayotarajia kuyafanya Setemba 23, ili kuruhusu mchakato wa mazungumzo.

Selasini amesema Chadema wametoa kipindi ambacho wanataka kufahamu wanachama wake wanaodaiwa kutekwa kurejeshwa na kinachopaswa kufanywa ni Serikali ama Polisi kuwajibu Chadema juu ya madai yao.

“Hivi Chadema wakijibiwa juu ya madai yao hao maandamano yatakuwepo, kwa hiyo mimi naomba Chadema watafakari hili. Sisemi yasifanyike, ila yaahirishwe ili kuruhusu Serikali ifanye utaratibu wa kikao,” amesema Selasini aliyewahi kuwa mwanachama wa Chadema.

Katika msingi huo, amesema ni kweli kati ya vyama vilivyoumia na vinavyoumia ni Chadema ukilinganisha na vyama vingine na kusisitiza msingi ni kufanyika kwa mazungumzo.

Naye Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, maarufu ‘Bwana Mapesa’ amesema pamoja na mambo yote yanayoendelea, ili kutoka hapa ni lazima kuwe na meza ya mazungumzo ya pamoja na si vyama kukutana kwa makundi, kwani hilo halina afya.

“Mimi nasisitiza tuzungumze na Rais, kama TCD inaweza kutuongoza katika hicho kikao kishirikishe vyama vyote sio kujifungua vyama viwili au vitatu. Mara vyama 13 mara vyama viwili. Ili kutoka hapa ni kuzungumza, tuzungumze kwani ndio njia,” amesema Cheyo.

Wakati wadau wakitahadharisha kufanyika kwa maandamano na kushauri kuwepo kwa mazungumzo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati akifungua mkutano huo amesema hawatarudi nyuma katika kutetea haki.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Amesema mwezi huu, chama hicho kimekuwa kwenye maombolezo kufuatia matukio ya utekaji na mauaji ya viongozi wake na vyombo vya dola kutokuwa na majibu kuhusu wahusika wa matukio hayo ili wafikishwe kwenye mkondo wa sheria.

Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa TCD, amesema viongozi wa chama chake wamekuwa wakipotea katika mazingira ya kutatanisha huku akitolea mfano Katibu wa Chadema, Jimbo la Sumbawanga, Dioniz Kipanya ambaye amepotea wiki sita zilizopita.

Mbali na Kipanya, Mbowe amesema Katibu wa Vijana wa chama hicho, Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise, haijulikani walipo.

Mwenyekiti huyo wa TCD amesema, wakiwa hawajapata majibu ya viongozi hao walipo, kiongozi aliyekuwa mjumbe wa sekretarieti ya chama hicho, Ali Kibao akatekwa na watu wenye silaha, Septemba 6, 2024 kisha mwili wake ukaonekana umetupwa, Ununio.

“Hatutarudi nyuma katika kutetea haki katika taifa hili. Kama tunataka kwenda mbele, lazima tuwe jasiri kusimama na kusema ukweli,” amesema Mbowe.

Ameongeza kuna haja ya kupata vyombo huru vya kuchunguza matukio hayo kwani kila mmoja ana thamani yake kipekee, hivyo kupotezwa kwa watu ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mwanasiasa huyo amesema Katiba inatambua haki ya msingi ya kuishi bila kujali rangi yake, imani yake au mahali anakotokea, lakini katiba haifuatwi katika kusimamia maisha ya watu.

Mwenyekiti huyo amesema chama hicho kinatamani wakati wote nchi iongozwe na Katiba iliyo bora ili kutengeneza ustawi ulio bora kwa wananchi wote na si utashi wa kiongozi mmoja.

“Tunaamini Katiba iliyo bora itazaa sheria bora na vyote kwa pamoja vitatengeneza ustawi ulio bora kwa raia wote. Nayazungumza haya nikiamini kwa muda mrefu katika nchi yetu kumekuwa na utamaduni wa walioko katika madaraka kuamini utashi wa kiongozi mkuu ndiyo unapaswa kuwa Dira ya Taifa.

“Dira ya Taifa letu wakati wote ili iwe ya haki kwa makundi na watu wote haipaswi kuwa utashi wa kiongozi mkuu. Inapaswa kuwa imechimbiwa kwenye katiba ya nchi,” amesema Mbowe.

Akihitimisha siku ya kwanza, Mbowe amesema: “Tumesikia ushauri kuhusu watu wazungumze, tumezungumza sana nchi hii. Samahani kwa kusema hili, ni kwamba CCM imechukulia nchi hii kirahisi sana kwa muda mrefu. Kwamba mtazungumza, mtazungumza, tutaelewana tutaendelea, lakini vitendo hakuna. Tumezungumza sana.”

Katika kikao hicho, kulikuwa na mabalozi wanaoziwakilisha nchi  za Marekani, Uholanzi na Ireland.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle

Balozi wa Marekani, Michael Battle amesema siku zote Marekani imewekeza kwa watu na demokrasia, hivyo wanathamini mchakato wa demokrasia unaowahusu watu moja kwa moja.

Alisema siku za hivi karibuni kuelekea kwenye uchaguzi, Tanzania na Marekani zimekabiliwa na vurugu ambazo zinatishia mchakato wa demokrasia katika mataifa hayo.

“Ni wazi kwamba mauaji na kupotea kwa watu havitakiwi kuwa na nafasi katika demokrasia yetu, si Marekani wala hapa Tanzania,” alisema Balozi Battle.

Alisisitiza Marekani na Tanzania zina ushirikiano wa muda mrefu na katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Marekani imetoa Dola za Marekani 7.5 bilioni kwa ajili ya kuimarisha uchumi, afya na elimu kwa Watanzania.

“Tunafurahi washirika wa Tanzania…Hatutarudi nyuma, inapokuja kwenye masuala ya haki za binadamu ambayo ndio msingi wa demokrasia,” alisema Battle.

Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi, Wiebe De Boer alisema demokrasia ni mchakato unaomtaka kila mmoja kushiriki, iwe ni wananchi, asasi za kiraia au vyama vya siasa.

Balozi wa Ireland, Nicola Brennan alisisitiza ushirikishwaji wa wanawake na wasichana katika mchakato wa kidemokrasia hasa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa sababu nao wana uwezo wa kuwa viongozi.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.

Related Posts