VIDEO: ‘Boni Yai’ apelekwa mahabusu, hatima ya dhamana Septemba 23

Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka mawili, akidaiwa kuchapisha taarifa za uwongo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter).

Jacob aliyefikishwa mahakamani hapo leo Septemba 19, 2024 amekana mashitaka dhidi yake baada ya kusomewa.

Anadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

New Content Item (1)

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akizungumza jambo na Boniface Jacob maarufu ‘Boni Yai’ mahakamani Kisutu

Boni Yai amesomewa mashtaka hayo na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Nurati Manja.

Katika shtaka la kwanza anadaiwa Septemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uwongo kuwa “Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa moja katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey.”

Katika shtaka la pili anadaiwa Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uwongo kuwa, “mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu Kwa kutenda uhalifu …, Bali Ma-RCO waliokuwa kuteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi.”

Jamhuri katika kesi hiyo, pia imewasilisha maombi mawili, kwanza Mahakama imuamuru aruhusu vifaa vyake vya kielektroniki na akaunti yake ya X kuwezesha mpelelezi kuingia na kufanya uchunguzi.

Pia, inaomba Mahakama izuie dhamana yake kwa muda.

Upande wa Jamhuri unaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema.

Jacob anawakilishwa na jopo la mawakili likiongozwa na Peter Kibatala.

Mrema alisema maombi ya Jamhuri yanatokana na ukinzani uliosababishwa na mjibu maombi (Jacob), akidai utaratibu chini ya sheria unataka mtuhumiwa anapokamatwa na vifaa ya kielektroniki vifanyiwe upelelezi.

Alidai alipokamatwa alikutwa na vielelezo ambavyo ni simu zilizochukuliwa kwake na wakati wa upelelezi alipotakiwa kutoa ushirikiano kutokana na vielelezo hivyo (simu na akaunti yake ya X) alikataa kutoa ushirikiano kwa kutoa nywila (neno la siri), ikiwemo ya akaunti hiyo.

Alidai kwa mujibu wa kifungu cha 32(3) (a) cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, mtuhumiwa akikataa kutoa ushirikiano Jamhuri inatakiwa kuwasilisha maombi mahakamani ili Mahakama imlazimishe atoe nywila, ili upelelezi ufanyike ndani ya vielelezo hivyo.

Hayo yamo kwenye kiapo cha Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kinondoni, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Davis Msangi kutoka Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kinondoni.

Katika kiapo amedai mshitakiwa alipokamatwa na kufunguliwa jalada la uchunguzi kuhusu makosa ya kimtandao aliyoyafanya, alikataa kutoa nywila, hivyo kufanya mpelelezi kushindwa kufanya jukumu hilo.

“Ili ofisa mtekelezaji wa sheria aweze kukamilisha upelelezi unaoendelea, sehemu ya upelelezi unatokana na simu hizo pamoja na akaunti hiyo ya X.

Ni hoja yetu kwamba Mahakama yako tukufu iweze kutoa amri ambazo nimezieleza hapo mwanzo,” alieleza katika kiapo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nasoro Katuga amesema wanaomba dhamana izuiwe kwa ajili ya usalama wake (Jacob).

“Kiapo hiki hakijapingwa na matokeo yake kutokupingwa kiapo ni ushahidi ambao ni wa kweli. Kwa mapenzi mema niliwauliza mawakili wa utetezi kama wanataka kukipinga (kwa kuwasilisha kiapo kinzani) lakini wakasema sina mapenzi hayo,” amedai.

“Kutokukipinga maana yake inakubaliana nao na sasa huwezi kuja kulipinga kwenye mawasilisho ya hoja, isipokuwa kama ni kupinga basi ni kuhusiana na hoja ya kisheria,” amedai.

Kwa mujibu wa kiapo, mshtakiwa alisema kuwa usalama wake uko hatarini kwamba, baada ya ‘kujilipua’ kwa kutoa taarifa hizo anajua kuwa atatekwa na kuuawa.

“…Hoja hii tulitarajia kuwa ingepingwa na mjibu maombi ambaye ndio alimwambia RCO lakini kutokuipinga Mahakama yako haina namna zaidi ya kuamini na hawawezi kukipinga kwenye uwasilishaji wa hoja,” amedai.

Wakili Katuga ameirejesha Mahakama katika kesi mbalimbali zilizoamuriwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kuhusu msimamo huo akisema:

“Tunatambua kuwa dhamana ni haki Kikatiba lakini pia ulinzi au usalama wa mtu binafsi ni haki ya Kikatiba na ndiyo maana kifungu cha 148 (5) kinaeleza Mahakama kuwa kama usalama wa mtuhumiwa uko hatarini basi dhamana yake inaweza kuzuiwa.”

RCO katika kiapo amesema bado wanafuatilia ni nani wanaomuweka kwenye hatari, wanaopanga kumuua na kwamba ili awe salama ni vyema aweze kuhifadhiwa mpaka pale itakapoonekana kuwa sasa yuko salama.

“Kwa hiyo tunaona ni busara ya Mahakama kutumia kifungu hicho kuzuia dhamana ya mshtakiwa mpaka pale tutakapoona malalamiko ya kuwa katika hatari amekuwa salama,” amesema.

Wakili Kibatala amedai wanafahamu kuwa hatia ya maombi ndiyo msingi wa kiapo.

“Kwa hiyo ni hoja yetu kwamba hakuna kiapo hapa maana hakuna maombi hapa mahakamani ya kumlazimisha mshtakiwa simu zake zichunguzwe,” amedai.

Amedai mahakamani hakuna maombi maana kazi ya hati ya maombi na kiapo ni tofauti.

Kibatala amedai kifungu cha 32 kinamtaja ofisa mtekelezaji wa sheria ndiye anapaswa kupeleka maombi na si Jamhuri.

Amedai hakuna maombi yaliyowasilishwa na ofisa mtekelezaji wa sheria SSP Msangi bali kuna kiapo pekee.

Kibatala amedai kiapo chochote lazima kishuhudiwe na wakili na majina yake na muhuri wake lazima vionekane pamoja na saini yake lakini hilo halijafanyika, hivyo kiapo kina kasoro.

Amedai wameombea amri kwenye kesi ambayo haiko mbele ya Mahakama.

Kuhusu kutowasilisha kiapo kinzani, amedai wakili amejipotosha kwa kuwa huo si msimamo wa sheria.

“Kwa kuzingatia kasoro hizi ni kwamba, upande wa mashtaka hawajatimiza wajibu wake wa kisheria kwenye hili. Wamekutajia tu hizi simu, lakini hawajaweka uthibitisho kama vile hati ya ukamatwaji mali ili Mahakama iwe na uhakika kuwa inatoa amri kwenye mali za nani, kwa hiyo hawajatimisha mambo ya msingi,” amedai.

Kuhusu madai kuwa vifaa vina taarifa za uwongo amedai ni suala la ushahidi maana mpaka Mahakama ijiridhishe kweli kwamba kuna hizo taarifa na nani kazitoa.

Wakili Hekima Mwasipu amedai kwa kusema taarifa ni za uwongo tayari wameshamuhukumu mshtakiwa jambo ambalo halitakiwi kuwepo kwenye kiapo maana linahitaji ushahidi.

Amedai kwa kasoro hizo za kisheria kiapo hakiwezi kukubalika.

Related Posts