Dereva, kondakta na abiria 16 wakamatwa Mara kwa kumpiga Askari

Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia watu 18, wakiwemo dereva, kondakta na abiria 16, kwa tuhuma za kumpiga askari wa usalama barabarani aliyekuwa akikagua gari walilokuwa wamepanda. Tukio hilo lilitokea Septemba 18, 2024, saa 12 jioni katika mkoa wa Mara.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Ofisa Mnadhimu wa Jeshi la Polisi Trafiki Kuu, Butusyo Mwambelo, amesema kuwa askari huyo alikumbwa na kipigo wakati akijaribu kushusha abiria waliokuwa wamesimama kwenye gari. Hata hivyo, kondakta wa gari hilo alifunga mlango na wote waliokuwa ndani ya gari, akiwemo dereva, kondakta, na abiria, walianza kumshambulia askari huyo.

“Askari wetu alikuwa akitekeleza wajibu wake wa kuwataka abiria waliokuwa wamesimama kwenye gari washuke. Lakini ghafla walimzonga kwa maneno ya kebehi, na kondakta kufunga mlango wa gari. Ndipo dereva, kondakta na abiria wao wakaanza kumpiga askari akiwa ndani ya gari. Je, kweli tumefika hatua hiyo kama Watanzania?” alisema Mwambelo.

Mwambelo alitoa maelezo hayo wakati wa operesheni ya ukaguzi wa magari iliyofanyika Septemba 19, 2024, katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Geita, ambapo alisisitiza kuwa tukio hilo ni la kusikitisha na halitavumiliwa. Jeshi la Polisi limechukua hatua za haraka kuhakikisha wote waliohusika katika tukio hilo wanawajibishwa kisheria.

Related Posts