ACT-Wazalendo yaitaka Serikali itafakari upya fidia wakazi Jangwani

Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo, kimeitaka Serikali kutafakari upya malipo ya fidia kwa wakazi wa Jangwani wanaopisha mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa kwa nyakati jana Alhamisi Septemba 19, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita alipowatembelea wakazi hao kwa lengo la kujua changamoto zao zinazowakabili kutokana na hatua ya Serikali kutangaza maboresho ya eneo hilo.

Mapema mwaka huu, mratibu wa mradi huo kutoka Ofisi ya Rais (Tamisemi), Humphrey Kanyenye alisema wameshatangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakayetekeleza mradi huo utakaogharimu Sh650 bilioni ambazo ni mkopo usiokuwa na riba kutoka Benki ya Duniani (WB).

Kwa mujibu wa Kanyenye, Sh4 milioni zitatolewa kwa kila kaya kwa ajili ya fidia ya ardhi kwa wakazi wa eneo litakalopitiwa na mradi ambapo zilianza kulipwa Februari 7, 2024.

Hata hivyo, Mchinjita amesema fedha za fidia zilizotoka haziendani na thamani ya ardhi ya wananchi wanaopisha mradi huo, ndiyo maana baadhi ya wakazi wamegomea mchakato huo.

“Nimekutana na mama mmoja ameniambia nyumba yake inataka kubomolewa lakini apewe fidia Sh14 milioni ambayo hata kiwanja huwezi kupata, sasa hivi viwanja vimepanda bei.

“Sasa leo unawaondoa raia katika ya jiji unawapa Sh14 milioni sasa viwanja watapata wapi? Serikali ifikirie upya suala hili, kitendo cha kuwafukuza wakazi hawa kisha kufanya uwekezaji utakaongiza mabilioni pasipo kuwajali wananchi mnaowaondoa sio sawa,” amesema Mchinjita.

Mchinjita amesema sera ya chama hicho  uendelezaji wa miji ardhi inayochukuliwa kwa ajili ya uwekezaji lazima iwanufaishe wananchi walioko katika maeneo husika.

Miongoni mwa mambo yatakayotelezwa katika mradi huo ni na ujenzi wa daraja la juu ‘fly over’ kupita Jangwani hadi Fire sambamba na kingo za mto Msimbazi.

Related Posts