Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania yashinda Tuzo ya Ubora katika Usalama

Johannesburg, Afrika Kusini, tarehe 19 Septemba 2024, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kupitia Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) imepokea tuzo ya kuwa Kiwanja chenye Ubora wa Usalama Afrika kwa mwaka 2024. Tuzo hii imetolewa na Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege (Airport Council International – ACI), ambalo hufanya tathmini ya ubora wa huduma zinazotolewa kwenye viwanja vya ndege kote duniani.

Tuzo hii inaipa heshima Tanzania katika ukanda wa Afrika na duniani kwa ujumla katika sekta ya usafiri wa anga, na kuthibitisha ubora wa viwango vya usalama vinavyotekelezwa katika viwanja vya ndege nchini.

Tuzo hiyo imepokelewa kwa niaba ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Walter Kahyarara, ambaye amesema kuwa tuzo hii ni kielelezo cha dhamira ya Tanzania katika kutekeleza viwango vya kimataifa vya utoaji wa huduma kwenye viwanja vya ndege. Prof. Kahyarara ameongeza kuwa tuzo hii inafungua milango kwa Tanzania kama sehemu salama kwa usafirishaji wa abiria kwa njia ya anga, na itachochea maendeleo katika sekta za utalii, uwekezaji, na uchumi wa nchi.

Tuzo za usalama za ACI ni miongoni mwa tuzo kubwa na zenye heshima duniani katika sekta ya usafiri wa anga, zikithibitisha kuwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inazingatia viwango vya kimataifa katika usalama wa viwanja vya ndege.

Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuzingatia viwango vya kimataifa kwa kufanya uwekezaji katika teknolojia, kutoa mafunzo kwa watumishi wake, kuboresha miundombinu, na kununua vifaa vya kisasa vya usalama kwenye viwanja vya ndege. Ushindi huu unaonesha kwamba jitihada hizo zimezaa matunda na kuiweka Tanzania katika orodha ya nchi zenye viwanja vya ndege salama na bora duniani.

Related Posts