Timu ya Taifa ya Tanzania ya soka la ufukweni imepangwa katika kundi la vigogo kwenye fainali za Afrika za soka la ufukweni zitakazofanyika mwezi ujao huko Misri.
Katika droo iliyochezeshwa jana huko Cairo, Misri, Tanzania imepangwa katika kundi A lenye timu za Misri, Ghana na Morocco.
Misri ambayo ni mwenyeji wa fainali hizo mwaka huu, ina uzoefu wa kutosha na ni miongoni mwa timu tishio katika soka la ufukweni Afrika.
Fainali zilizopita ilifika hatua ya fainali ambapo ilifungwa na Senegal na kiujumla imeshiriki fainali za Afrika mara 11 ikishika nafasi ya pili mara moja, kumaliza katika nafasi ya tatu mara nne, imeshika nafasi ya nne mara mbili kama ilivyo kwa nafasi ya tano huku ikishika nafasi ya sita mara moja na mara moja ikiishia hatua ya makundi.
Morocco imeshiriki katika fainali tisa za nyuma za mashindano hayo na mafanikio yake makubwa yalikuwa ni kumaliza katika nafasi ya tatu mwaka 2013, 2021 na 2022 huku ikiishia katika nafasi ya nne mara mbili, mara tatu ikimaliza ikiwa ya tano na mara moja ilishika nafasi ya sita.
Ghana ndio timu pekee kwenye kundi hilo ambayo haipaswi kuitisha Tanzania vile haina historia ya kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Ghana imeshiriki mara tatu tu ambapo mara mbili ilishika nafasi ya saba na mara moja iliishia hatua ya makundi.
Ikumbukwe hizi ni fainali za tatu kwa Tanzania kushiriki katika soka la ufukweni Afrika.
Mara ya kwanza ilishiriki fainali za soka la ufukweni Afrika 2018 na kuishia katika nafasi ya saba na kisha nwaka 2021 iliposhika nafasi ya sita.
Kundi lingine katika fainali za mwaka huu linaundwa na mabingwa watetezi Senegal, Msumbiji, Malawi na Mauritania.
Timu mbili ambazo zitatinga hatua ya fainali ya mashindano hayo, zitafuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia ambazo Shelisheli mwakani zikishirikisha timu 24.