Majaliwa aagiza kuimarishwa ufuatiliaji na tathmini kuleta maendeleo

-Atoa Maagizo Matano Kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini

-Dk. Biteko Awataka Wataalam kuilinda Taaluma

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amezitaka taasisi za ufutiliaji na tathmini kufanya kazi kwa weledi na kuimarisha eneo hilo ili kuendana na mahitaji yanayolenga kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hayo yameelezwa leo Septemba 20, 2024 Zanzibar na Dk. Biteko wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Katika Kongamano la Tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza.

Amesema wataalam wa ufuatiliaji na tathmini wanawajibika kuilinda taaluma hiyo na kuwashawishi kwa hoja wakuu wa taasisi husika kupenda kazi zinazotokana na taaluma hiyo badala ya kujisikia wanyonge kitaaluma.

Aidha, Dk. Biteko amewataka washiriki muda wote kusisitiza misingi ya taaluma hiyo na baadaye kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa na watu wake. “Inawezekana katika maeneo yenu ya kazi wakawepo wakuu wa taasisi au viongozi wa serikali ambao hawapendi mfanye kazi yenu vizuri, kukubaliana na hilo ni kujiua wenyewe. Mnapotoka hapa mkafanye mkuu wa taasisi au kiongozi aone umuhimu wenu katika shirika,” amesema Dk. Biteko.

Aidha, amewataka wataalamu hao kusema ukweli na kusimamia taaluma yao. “Nataka niwaombe mkajiamini Rais Samia ameahiza na kuelekeza uwepo wa vitengo vya tathmini ndani ya Serikali, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wafanyekazi na kitengo cha ufuatiliaji kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu mfuatilie fedha zinazopelekwa kwenye miradi na matokeo yake kwenye kubadilisha hali za maisha ya watu.” Amesisitiza Dk. Biteko.

Kupitia kikao hicho, ametoa maagizo matano yakilenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na kujifunza.

“Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu ikamilishe mapema Mfumo Ufuatiliaji na Tathmini na kuwezesha taarifa za utendaji wa Serikali kupatikana kwa urahisi.Tume zetu za Mipango zikamilishe uchambuzi wa miradi yote inayotekelezwa ndani ya Serikali na kila mwaka kutoa taarifa ya utekelezaji. Namna hii itawezesha Serikali kuona tija ya miradi inayoidhinishwa na kutekelezwa hapa nchini,” amesema Dk. Biteko.

Aidha ameielekeza Ofisi hiyo kukamilisha Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ili iwezeshe utekelezaji sahihi wa eneo la ufuatiliaji na tathmini nchini. Sambamba na TanEA na ZaMEA kuweka mikakati ya kujiimarisha kiuchumi ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa uanzishwaji wake.

Aidha, Dk. Biteko aziagiza TanEA na ZaMEA kuwa Sera pamoja na mikakati yake ziwe zinafanyiwa Tathimini kila baada ya miaka mitatu baada ya kuandaliwa. Hii itasaidia kujua kila hatua inayofikiwa kwa utelezaji wake pamoja na utatuzi wa changamoto za utelezaji na maboresho wakati wa uhuishaji wa Sera.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema kuwa Kongamano hilo la tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza lenye kauli mbiu isemayo  ‘Kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia teknolojia katika  ufuatiliaji na tathmini na matumizi ya matokeo ya tathmini katika kufanya maamuzi’ limepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau na washiriki.

Ametaja lengo la Kongamano hilo kuwa ni kuweka msisitizo kwenye lengo kuu la Serikali la kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi na kuwa katika kutimiza azma hiyo, washiriki wamehamasishwa kutumia vizuri taaluma na mafunzo mbalimbali wanayoyapata kuhakikisha wanakuwa jicho la Serikali katika mipango yake, utendaji wake na utekelezaji wa miradi ili iweze kupata maendeleo.

Aidha, Lukuvi amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi wamekuwa vinara wa ufuatiliaji na tathmini katika utendaji wa Serikali kwa ujumla wake, utekelezaji wa miradi yote nchini na utoaji wa huduma bora kwa wakati kwa wananchi wote.

Amesema kuwa marais hao wanafanya hayo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambapo kwa sekta zote umewekwa mkazo wa ufuatiliaji na tathmini katika utendaji, utekelezaji wa miradi na utoaji huduma.

“Katika kuimarisha Sekta ya Fedha, ibara ya 20 (f) ya Ilani ya CCM inaitaka Serikali kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya mashirika na taasisi zilizobinafsishwa ili kuhakikisha mikataba inatekelezwa ipasavyo na Sekta ya Ujenzi, ibara ya 51(a)(ii) ya Ilani  inaitaka Serikali kuboresha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za barabara kwa kuhakikisha thamani ya ubora wa kazi inaendana na fedha zilizotumika.” Amesema Mhe. Lukuvi.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk. Jim Yonazi amesema kuwa kupitia Kongamano hilo wamepata fursa mbalimbali ikiwemo kuwa  na mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa wataalamu. Sambamba na washiriki kujifunza mbinu mpya za kuboresha mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini, hasa kwa kutumia teknolojia na takwimu sahihi ili kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.

“Kongamano hili limesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika mchakato mzima wa Ufuatiliaji na Tathmini ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha Serikali na wahisani wanatoa huduma zenye tija. Pia, ushirikishwaji wa waananchi utasaidia kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inawafaidisha moja kwa moja.” amesema Dk. Yonazi.

Vilevile ameongeza kuwa, kongamano hilo limelenga kukuza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo, kwa kuleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wa serikali, wabunge, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi, aidha, limetoa jukwaa la kujadili jinsi ufuatiliaji na tathimini unavyoweza kutumika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na uwajibika.

Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Dk. Ameir Haji Sheha amesema kuwa ushiriki wa Kongamano hili limeibuwa haja na mahitaji mbalimbali  na kuwa Kongamano hilo limejumuisha washiriki 738 na ameishukuru Ofisi ya Waziri, Sera, Bunge na Uratibu kwa ushirikiano wakati wote wa maandalizi wa Kongamano hilo.

Related Posts