Dodoma. Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kusomewa mashitaka ya mauaji ya mama na mwanawe waliokuwa wakazi wa Mtaa wa Muungano ‘A’ kata ya Mkonze wilayani Dodoma.
Kesi hiyo namba 23436 ya mwaka 2024 iliyoko kwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule, imetajwa kwa mara ya kwanza jana Septemba 19, 2024.
Hata hivyo, ilisikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Denis Mpelembwa kutokana na hakimu aliyepangiwa kesi hiyo hakimu Mpangule kutokuwepo.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Patricia Mkina amewataja washtakiwa hao kuwa ni Fikiri Senyengwa (45) maarufu kwa majina ya Gidioni ama Baba Chichi mkazi wa Ipagala jijini Dodoma.
Wengine ni Daudi Nyakombe (34) na Rajabu Nemdachi (45) wote wakazi wa Mkonze jijini Dodoma.
Amedai kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 6 mwaka 2024, Mkonze jijini Dodoma ambapo washtakiwa hao waliwauwa Mwamvita Mwakibasi (34) na Salma Ramadhani (12).
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 4, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.