Pamoja na kuruhusu mashabiki kuingia bure katika Uwanja wa Sokoine, mashabiki wa Mbeya City wameondoka uwanjani vichwa chini baada ya timu yao kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Bigman katika mchezo wa Ligi ya Championship.
Mchezo huo ambao ulikuwa wa ufunguzi, Mbeya City walikuwa wenyeji ambapo matarajio ya wadau na mashabiki wa timu hiyo jijini Mbeya ilikuwa ni ushindi tofauti na kilichotokea.
Mbeya City waliowahi kutesa Ligi Kuu na kushuka misimu miwili sasa, ndio walitangulia kupata bao kupitia kwa Maliki Joseph kisha Bigman kusawazisha kupitia kwa Salum Kanon na kwenda mapumziko nguvu sawa.
Kipindi cha pili City walionyesha kumiliki mpira na kutengeneza nafasi kadhaa, lakini walishindwa kumalizia mipira ya mwisho.
Dakika ya 60 Eliud Ambokile aliiandikia bao la pili City ambapo kabla ya mpira kumalizika Omary Kusaga aliyetokea benchi aliisawazishia Bigman na kufanya dakika 90 kuisha kwa sare.
Timu hizo zimekutana ikiwa kila upande una kumbukumbu yake, ambapo City ilidumu Ligi Kuu misimu 10 mfululizo, huku Bigman (zamani Mwadui FC) ikishuka misimu mitano nyuma.
Mmoja wa mashabiki wa Mbeya City, Haruna Goba amesema matokeo hayo siyo mazuri kwao akieleza kuwa wachezaji walijisahau kutimiza majukumu.
“Benchi la ufundi lifanye tathimini ya kina, haiwezekani straika yupo eneo la goli anashindwa kufunga bao. Siyo matokeo mazuri ukizingatia tupo nyumbani na hii ni mechi ya kwanza,” amesema Goba