Wananchi 5, 000 kunufaika na umeme vijijini Tabora

Tabora. Jumla ya vitongoji 180 vya majimbo 12  mkoani Tabora, vinatarajiwa kuunganishwa na umeme katika mradi wa umeme kwenye vitongoji wa HEP,  utakaotekelezwa kwa muda wa miaka miwili na kampuni ya Sinotec kutoka China.

Akizungumza na Mwananchi jana Septemba 19, 2024, Meneja wa Miradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Oscar Migani amesema mradi huo wa awamu ya kwanza,  unatarajia kuwanufaisha wateja zaidi ya 5,000 huku vitongoji 180 vikiunganishwa na huduma ya  umeme.

“Mradi huu utakaogharimu Sh19 bilioni utanufaisha vitongoji 180 katika majimbo yote 12 na utahakikisha miundombinu ya umeme inasogea kwenye vitongoji.

“Mradi huu utafunaisha wateja 5,940 ambapo kwa kila jimbo limepewa vitongoji 15 wateja 495 watafungiwa umeme na wateja hawa watanufaika na umeme wa msongo mdogo,’’amesema.

Amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi Sinotec kutoka China aliyeanza kazi Septemba 3, 2024 na atafanya kwa miezi 24 akisimamiwa na REA na Tanesco.

Kaimu Meneja Tanesco Mkoa wa Tabora, Mhandisi Sostenes Maganga, amesema wamejipanga kuusimamia ipasavyo mradi huo ili ukamilike kwa ubora unaotakiwa, huku wananchi wakitakiwa kupisha maeneo ili wapate mradi huo.

“Mradi huu utawanufaisha wananchi moja kwa moja na hautakuwa na fidia hata kidogo, hivyo utakapopita kwenye maeneo ya watu watu watoe maeneo kwa ajili ya mradi huo ili wakazi wanufaike na nishati hiyo, maana vijiji vitakavyonufaika ni vile ambavyo havijapata kabisa nishati hiyo tangu kuanza kwa programu hii,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Jimbo la Ulyankulu, Mbunge Rehema Juma amesema uwepo wa mradi huo, utasaidia kuwainua wananchi wa jimbo hilo kiuchumi kwa kuwa wataweza kufanya biashara kwa kutumia nishati hiyo.

“Kuna baadhi ya vitongoji ambavyo vilikua havijapata umeme kabisa hivyo mradi huu utasaidia kuwainua kiuchumi wananchi ikiwemo kuuza vinywaji baridi na shughuli zingine za kuwaingizia kipato wakazi wa jimbo langu sababu ya uwepo wa nishati hii ya umeme,” amesema.

Mkandarasi Jared Zhang wa Sinotec amesema atahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi hao waweze kunufaika na umeme huo.

Related Posts