Amesisitiza kuwa serikali kwa sasa inawekeza katika kahawa kwa kugawa miche na mbolea ya ruzuku hivyo,anatarajia kupigwa vita na wafanyabiashara kutokana na kukemea kangomba lakini hatarudi nyuma kwa maslahi ya zao hilo.
Waziri Bashe amesema hayo katika muendelezo wa ziara yake Mkoani Ruvuma mara baada ya kutembelea mashamba, viwanda vya kuchakata kahawa na skimu za umwagiliaji wilayani Mbinga na Nyasa.
“Najua haya maamuzi yatakuwa na maumivu na yatakuwa na kelele, mimi kelele nimezoea, kamateni wanaonunu kahawa kwa kangomba,”amesema.
Amesema, anatarajia vita kubwa dhidi ya wafanyabiashara wanaonunua kahawa kwa njia ya Kangomba na hatarudi nyuma.
“Tutegemee kelele nyingi kutoka kwa wafanyabiashara lakini sipo tayari kuona kangomba katika kahawa.Kelele zitakuwa nyingi watapitishia kwa wakulima tujiandae lakini nasema ili kufikia soko la kimataifa hatuwezi kuvumilia ununuzi usiofaa,”amesema.
Amesisitiza kuwa, hatua ya serikali kuwekeza katika zao hilo, imelenga kuijengea ubora kahawa ya Tanzania kimataifa na kunufaisha wakulima.
“Tunatoa mbolea na miche kwa ruzuku na kuwezesha kilimo hiki kuhimili ushindani dhidi ya kahawa za nchi nyingine,”amesema.
Akiwa katika miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Waziri Bashe amesema“Nimejionea kiwango cha umasikini wa watu wetu hapo mambo tumeanza kuyafanyia kazi.Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia Suluhu Hasan kwa kutupatia fedha mwaka huu, nimemwambia Mbunge Injinia Stella Manyanya, tutafanyia kazi changamoto za watu wetu.
“Tumeshatangaza na tumeshapata mkandarasi kwa skimu zenye hekta 8395 tutajenga barabara za ndani ya shamba, madaraja na vigawa maji ndani ya shamba na usanifu umeshakamilika na mkandarasi amepatikana”,amesema Waziri Bashe
Pia Waziri Bashe ameitaka,kufanya usanifu na kuziingiza barabara za Lipingo katika mpango wa utekeleza wa mradi huo wa Umwagiliaji
“Nimegiza Tume ifanye usanifu, waingize kwenye mradi barabara zote mbili hapa Tume inatekelez miradi ya zaidi ya Bilioni 25 kwa Wilaya ya Nyasa pekee haishindwi kujenga hizo barabara zote,”amesema.
Aidha amesisitiza haja ya Skimu zilizopo katika Halmashauri ya Nyasa na idadi ya skimu zitakazo anza kufanyiwa utekelezaji kwa haraka.
“Halmashauri ya nyasa kuna skimu nane na kwa kuanzia tutaanza kuzijenga skimu mbili kuanzia mwaka huu wa fedha na ndani ya miaka 2 zote hizo zitakuwa zimejengwa.Muwape ushirikiano wataalamu wanaotekeleza miradi”
“Pia Tume mfanye ujenzi wa ghala katika eneo la mradi na mashine ya kukoboa mpunga ili wananchi waweze kuuza mchele badala ya Mpunga,”amesema.
Ameongeza kuwa Wizara ina mpango wa kuanza kuzalisha wa mbegu karibu na eneo la mradi wa Lundo katika kata ya Lipingo na kuanzisha vituo vya zana za kilimo na kujenga kituo cha mbolea.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nyasa Injinia Manyanya, amesema Wilaya hiyo inahitaji kukua kiuchumi na tegemeo kubwa ni kilimo cha mpunga hivyo wanatarajia miradi ya umwagiliaji iwe chachu ya uzalishaji.