Msako mwanafunzi aliyepotea kuhamia mtaani, wenzake waeleza alivyotoweka

Arusha. Msako wa kumtafuta mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara, wilayani Babati, Joel Johannes (14), aliyepotea tangu Septemba 14, 2024 walipokwenda Mlima Kwaraa kwa ziara ya masomo, sasa kuhamia mtaani.

Joel alipotea tangu Jumamosi iliyopita akiwa kwenye ziara ya masomo katika mlima huo uliopo Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, Emmanuel Dahaye, amedai katika mazingira ya sasa wanahisi mwanafunzi huyo ametoroka na yuko mtaani, hivyo kwa sasa nguvu kubwa inapelekwa huko kumtafuta.

“Katika mazingira haya tunahisi kijana ametutoroka yuko mtaani kwa hiyo hatua inayofuata sasa hivi ni kupeleka nguvu kubwa mtaani kumtafuta hii ni changamoto katika kazi. Tunaomba Mungu  tufanikiwe tunaendelea kumtafuta hatujakata tamaa tuna imani atapatikana,”amesema mkuu huyo wa shule.

Amesema kuwa siku ya safari hiyo ya masomo, Septemba 14, 2024 ilihusisha wanafunzi wa kidato cha pili ambao walikuwa 103 ambapo kati yao wasichana walikuwa 62 na wavulana 41 na kuwa baada ya mwanafunzi huyo kupotea walianza kumsaka hadi leo bila mafanikio.

“Tumeshirikiana na ofisi ya Mkuu wa wilaya, Polisi, TFS (Taasisi ya Misitu), mgambo, wananchi na wazazi wa mtoto huyo tangu ile siku,”amesema.

Akizungumzia tabia ya mwanafunzi huyo, Mwalimu Dahaye amesema kuwa mwanafunzi huyo hakuwahi kuonyesha tabia yoyote mbaya.

“Kama ametoroka tunamuomba arudi shuleni tutampokea, kipindi cha ukuaji kina mambo mengi vijana wana mengi, arudi shule aondoe taharuki ya wazazi, walimu na jamii,”

“Aje aendelee na masomo yake na anatarajia kufanya mitihani ya Taifa Oktoba 28, 2024  na kama kuna mwajamii amemuona atoe taarifa ili apatikane arudi shuleni aendelee na masomo yake, ameongeza Emanuel

Baadhi ya wanafunzi wenzake waliopanda naye mlima wamedai kuwa siku hiyo mwenzao alikuwa tofauti na siku nyingine na kuwa alikuwa na hali ya kujitenga na wenzake tofauti na ilivyo siku zote.

Mmoja wa wanafunzi hao, Amani Mollel amedai kuwa wakiwa wanapanda kwa makundi yeye akiwa kundi la pili na wenzake, walipokaribia kileleni walimkuta Joel amekaa chini ya mti peke yake akijikuna kwa madai kuwa amepita kwenye majani yamemuwasha.

“Tukamwambia twende akakataa akasema nyie nendeni mtanikuta hapa nimekaa kwenye kivuli, tukamlazimisha hadi akatukubalia akatufuata tukawa tunatembea naye na baadaye tukakutana na kundi lingine, tukafuata njia moja tukakuta njia imefungwa.

“Tukasema tuangalie kama njia ipo na wakati huo Joel tulikuwa naye ila tulipofika mbele walimu wakatuita tukaanza kugeuka nikamwambia Joel turudi kule akasema sawa ila alikuwa anaonyesha hana nia ya kurudi ana mpango wa kuendelea mbele, tukafika mbele tukapotea tena tukakuta njia imefungwa,”ameendelea kusimulia Amani.

Amani ameendelea kusimulia: “Wakati tunageuza hapo ndipo alipochoropoka hadi tulipokutana na wenzetu tukagundua hakuwapo. Hana tabia mbaya, mimi nahisi kuna kitu, tunahisi Joel ameshuka chini ya mlima yuko mtaani amejificha,”amedai

Akizungumza leo Ijumaa Septemba 20, 2024, Katibu Tawala Wilaya ya Babati, Halfan Matupula amesema licha ya kuongeza nguvu ikiwemo mgambo 60, walioungana na vyombo vingine vya usalama, wananchi na wazazi  hadi sasa hawajafanikiwa kumpata.

“Wametafuta siku hizi zote wakiungana na wazazi na wazazi na timu imejiridhisha mtoto hajapatikana na ni kweli hayupo na kwa mujibu wa mhifadhi kwa maeneo ambayo yanafikika yamepitiwa,”amesema

Halfan amesema kwa sasa jitihada zinapelekwa upande mwingine kwa jamii kwa sababu inawezekana mwanafunzi huyo amepotea kweli baada ya kuachwa na wenzake mlimani akashuka mwenyewe.

“Lakini pia kuachwa na wenzake hilo linaweza kuwa ni kosa sana na anafahamu wazazi wanamtafuta huenda yuko kwa wenzake, amekaa anakuwa na hofu , tunachokifanya sasa hivi ni kupita kwenye maeneo ya karibu,’’ amesema.

Mmoja wa waongozaji aliyepanda mlima na wanafunzi hao, aliyejitambulisha kwa jina la Adam, amedai siku ya tukio wakati wanarudi walikutana na kundi la wanafunzi waliopotea na wakawaita wakawa mbele wakaanza kushuka mlima.

Amedai walipofika mbele wanafunzi hao walidai kuwa Joel hawamuoni na kuwa walilazimika kurudi nyuma na kuanza kumsaka mwanafunzi huyo huku wakimuita jina lake bila mafanikio na baadaye walirejea kuwarudisha wanafunzi wengine.

“Sijui imekuwaje ni kitu gani kimempata lakini wanasema alikuwa akiambiwa twende hivi anapita njia yake,”amedai mwongozaji huyo.

Related Posts