Unguja. Ili kuongeza nguvu katika utekelezaji wa dhamira ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, kwa mwaka wa fedha 2024/25 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetenga Sh41.6 bilioni kutoa mikopo kupitia programu ya Inuka.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 20, 2024 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipofungua tamasha la pili la Fahari ya Zanzibar.
Amesema Serikali imeongeza kiasi cha fedha baada ya kuona mafanikio makubwa walipoanza utaratibu huo kwa kutoa Sh15 bilioni lakini zimezalishwa na kufikia Sh30 bilioni.
Programu hiyo inaendeshwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA).
Kutokana na hali hiyo, Dk Mwinyi amesema wanatarajia kuzindua mifumo ya kupata huduma zitakazotolewa na ZEEA ambayo imefanikishwa kwa ushirikiano na Kampuni ya Airpay na Serikali mtandao.
“Haya ni mafaniko makubwa kuendeleza wananchi kiuchumi, hatua hii ya kutayarisha na kuanza kutumia mifumo katika uombaji na uidhinishaji wa mikopo, mafunzo na masoko ya mtandao ambayo yanavuka mipaka ya nchi yetu ni ya kupongezwa na kuungwa mkono,” amesema.
Dk Mwinyi amesema ni imani yake kuwa mwelekeo huo mpya utasaidia kuongeza utaalamu katika kuchakata maombi yanayopokewa, kupunguza urasimu na muda wa maombi ya huduma zinazotolewa na ZEEA, hasa mikopo.
Katika msingi huo wa kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi, ZEEA inaingia katika utekelezaji wa mradi wa pamoja wenye thamani ya Sh13 bilioni kwa ufadhili wa Benki ya Dunia utakaotekelezwa kwa ushirikiano na Wizara ya Ustawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.
Pia, kuna mradi wa Fast wenye thamani ya Sh8 bilioni utakaotekelezwa na ZEEA kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
“Miradi yote hii inalenga kuongeza fedha za mikopo na programu nyingine za uwezeshaji wananchi,” amesema.
Katika utekelezaji wa dhamira ya kuimarisha mazingira ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, Dk Mwinyi amesema Serikali imekuwa ikitekeleza miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara za mijini na vijijini ili kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa na kuweza kuyafikia masoko kwa urahisi na haraka.
Kutekelezwa kwa miradi hiyo amesema kumechangia kwa kiasi kikubwa kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kukuza sekta ya utalii na kuzalisha ajira, hasa kwa vijana na kutoa soko la uhakika kwa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali.
Amesema tathmini iliyofanyika imeonyesha zimezalishwa ajira 187,651 kati ya hizo wanawake ni 94,622 na wanaume 93,029 katika fani mbalimbali.
“Takwimu za jumla zinaonyesha ajira katika sekta rasmi ni asilimia 62.9 na ajira katika sekta isiyo rasmi ni asilimia 37.1. Hali hii inamaanisha kuwa sekta isiyo rasmi inaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuzalisha ajira nchini,” amesema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Sharif amesema tamasha hilo la wiki moja kuanzia Septemba 20 hadi 27, 2024 litakuwa na matukio mbalimbali, huku sekta mbili za utalii na biashara zikinufaika zaidi.
Mkurugenzi wa ZEEA, Juma Burhan amesema mbali na kukuza matumizi ya kidijitali, tamasha linalenga kusaidia wajasiriamali wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kupata masoko ya bidhaa na huduma zao.
Faida nyingine amesema itapatikana kwa kuzindua nembo ya bidhaa zinazotoka Zanzibar ili kuzitambua na kukuza bidhaa za wajasiriamali kwenye masoko ya kitaifa na kimataifa.