Unguja. Profesa Karim Manji (65) wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), amechaguliwa kuwa mmoja wa washindi wa tuzo ya Mhitimu Bora wa Chuo Kikuu cha Harvard.
Anaelezea safari yake ya miaka 20 ya utafiti kupitia machapisho 250 na mchango wake katika sekta ya afya kwa miaka zaidi ya 35, siyo tu nchini Tanzania, bali pia katika mataifa mengine.
Hivi karibuni Profesa Karim alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo, aliyotunukiwa kwa kutambua mchango wake mkubwa katika sekta ya afya.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Unguja Zanzibar, Profesa Karim anasema tuzo hiyo ni matokeo ya kujituma na kujitoa kwake katika kazi. Alianza kufanya kazi katika Muhas mwaka 1988.
Anasimulia jinsi alivyopokea kwa mshangao taarifa ya kushinda tuzo hiyo, kiasi cha kufurahia hadi kumliza. Anasema licha ya kujitolea kwa weledi katika kuokoa maisha ya watoto, hakutarajia kutambuliwa kwa kiwango hiki.
Ansema furaha yake iliongezeka zaidi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumpongeza kupitia mtandao wake wa X.
Profesa Karim, ambaye ameandika zaidi ya machapisho 250, anasema anakumbuka tafiti zake mbalimbali ambazo zimekuwa na mchango mkubwa kwa Serikali na nchi nyingine, huku akitaja chapisho lake la kwanza lililompatia uprofesa.
“Namuomba Mungu tuzo hizi zisije kuniletea kiburi au kunifanya nibadilishe tabia yangu ya kuwahudumia watoto kwa upendo na bila ubaguzi,” amesema.
Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa huduma bila kujali changamoto au utukufu unaokuja na mafanikio.
“Tuzo hii ina maana kubwa, siyo tu katika maisha yangu binafsi, bali pia kwa taifa la Tanzania na mataifa mengine,” amesema Profesa Karim na kuongeza: “Huu ni uthibitisho kwamba kazi nzuri inayofanywa kwa moyo wa dhati haipotei.”
Akiendelea kueleza furaha yake, anasema hakutarajia kutambuliwa na Rais Samia, jambo lililomshangaza, lakini pia kumpa furaha kubwa.
Anasema anafurahi kuona juhudi zake za kuboresha afya za watoto zinatambuliwa na mwajiri mkuu wa taifa, jambo aliloliona kuwa na heshima kubwa kwake.
Profesa Karim, aliyesomea magonjwa ya watoto wachanga Ulaya, anasema mwaka 2002 alihitimu masomo ya uzamili katika afya ya jamii kutoka Harvard, ndipo alipoanza kazi zake za utafiti kwa kiwango kikubwa zaidi.
Anasema milango ya utafiti ilianza kufunguka, na mara kwa mara alikuwa na tafiti tatu kwa wakati mmoja, zote zikilenga afya ya watoto wachanga na masuala ya lishe.
Tafiti nyingi alizozifanya zililenga kuboresha afya za watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wale wa chini ya mwezi mmoja.
“Huu ndio ulikuwa msingi wa utafiti wangu kwa miaka mingi sasa,” anasema.
Mara nyingi jamii inapoona utafiti umefanywa, huona kama jambo la kawaida, lakini profesa huyo anabainisha kuwa utafiti unahitaji uadilifu na uaminifu wa hali ya juu.
Anasema kufanya utafiti kunahitaji ujasiri na uadilifu mkubwa na siri ya mafanikio yake ni kuonyesha viwango vya juu vya uadilifu, hali iliyowafanya watu wengi kutaka kumshirikisha wanapofanya utafiti.
Anasisitiza kuwa Muhimbili imekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio yake, huku akisema watu wanaotafuta kufanya utafiti wanachagua taasisi yenye heshima na hadhi kama Muhimbili.
Katika miaka 20 ya kufanya utafiti na 35 ya kuhudumu Muhas, Profesa Manji amewafundisha madaktari na wauguzi waliojifunza zaidi kuhusu utafiti.
“Siyo hao tu, bali pia wapo watafiti kutoka mataifa mengine ambao wameungana nami, jambo ambalo limenifanya niwe mwalimu wa kimataifa,” anasema.
Akipokea tuzo ya pili kwa mchango wake katika kuboresha afya za watoto wachanga, kwa msaada wa Serikali ya Ujerumani, Profesa Karim anasema walitengeneza mitalaa maalumu kwa ajili ya kufundisha madaktari.
Anasema mitalaa hiyo imetoa madaktari waliobobea katika magonjwa ya watoto wachanga na yeye alikuwa mmoja wa waanzilishi wa mitalaa hiyo.
Tafiti zake zasaidia kutengeneza sera za afya
Profesa huyo anasema matokeo ya tafiti zake yamechangia kutengeneza sera za afya, hasa katika tiba kwa watoto wachanga na wale wa chini ya miaka mitano.
Historia inaonyesha machapisho yake yamekuwa msingi wa sera za kimataifa na mataifa mengine yametumia matokeo ya tafiti za profesa huyo kama mfano wa kuigwa.
Miongoni mwa tafiti muhimu alizofanya ni ile ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Utafiti huo ulijikita katika matumizi ya dawa ya Nevirapine kwa mtoto, ukilenga kuzuia maambukizi wakati akiendelea kunyonya maziwa ya mama.
Matokeo yake yalipunguza maambukizi kutoka asilimia 15 hadi asilimia 0.5, hatua kubwa katika afya ya umma na mojawapo ya mafanikio yake yaliyompatia uprofesa.
Sasa, sera hiyo inatambulika kimataifa na dawa hiyo inamwezesha mama kuendelea kunyonyesha kwa usalama bila kuhatarisha afya ya mtoto.
Kumbukukumbu ya kazi yake siku ya kwanza
Mtaalamu huyo anasema anakumbuka siku ya kwanza akiwa wodi B pamoja na mwalimu wake, Profesa Charles Mgone (marehemu) ambaye alimueleza kuna watoto wengi wanaougua sana na jukumu lake kubwa ni kuhakikisha hakuna mtoto anayefariki dunia.
Aliniambia; “Sikiliza, hapa kuna watoto wanaumwa sana, ulichojia hapa sio kujaza attendancy na kupata mshahara, bali kuhakikisha asife mtoto hapa katika wodi B.” Profesa Karim anasema kuwa baada ya kuelezwa hayo, aliweka ahadi ya kufanya kila awezalo kuokoa maisha ya watoto.
“Niliahidi kwa kadiri ya uwezo wangu, nitahakikisha watoto hawafi. Kama ni matatizo mengine sawa, hiyo tutamuachia Mungu, lakini nitatumia uwezo wangu wote kuhakikisha hakuna mtoto anayekufa mikononi mwangu,” anasema Profesa Karim.
Alivyotumia mdomo kuwapulizia watoto hewa
Anasema ili kutimiza ahadi yake, alifanya kila juhudi kuhakikisha anaokoa maisha ya watoto, alitumia mdomo wake kuwapulizia hewa kipindi hicho hakuna vifaa vya kisasa.
“Miaka 30 iliyopita, nilitumia mdomo wangu kuwapulizia hewa watoto ili waweze kuhema. Kuna mengi niliyoyafanya na leo inanipa amani,” anasema mtaalamu huyo, aliyeokoa maelfu ya uhai wa watoto wachanga, wakiwemo wale waliozaliwa kabla ya wakati, maarufu kama ‘njiti’ Hospitali ya Muhimbili.
Alichojifunza katika kazi yake
Profesa Karim anasema mbali na kujifunza fani yake, amejifunza pia umuhimu wa utu na ubinadamu.
“Unaweza kuwa mtaalamu mzuri katika fani yako, lakini ukitumia lugha ya kejeli au kutokuwa na huruma, unakuwa siyo binadamu. Ni muhimu kutumia lugha nzuri na kumfariji mgonjwa ili apate ujasiri wa kutumia dawa vizuri, badala ya kutumia maneno ya kejeli,” anasema. Pia anasema amejifunza kuwa karibu na familia za wagonjwa, jambo alilosema lina umuhimu wake.
“Ukimwona mtoto anaumwa na mama hana fedha, huku mtoto akiwa mahututi, ukimfariji mama na kumgusa, unampa matumaini makubwa.”
Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, Profesa Karim anasema wataalamu waliobobea katika masuala ya watoto wachanga walikuwa watatu tu aliowataja kuwa ni Dk Masawe, Joyce Mgone, na yeye mwenyewe.
Anasema kwa sasa kuna zaidi ya madaktari 12 waliobobea katika afya ya watoto wachanga nchini kote. Wengi wao wamesoma chini ya wataalamu hao watatu.
Profesa Karim amebainisha kuwa vifo vya watoto wachanga vilikuwa kikwazo kikubwa katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu. Hata hivyo, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika kuboresha afya ya watoto wachanga, hasa wale wenye uzito pungufu au njiti. Anasema mwaka 2008, aliandika jarida kuhusu afya ya watoto wachanga Tanzania, alionyesha wakati huo kulikuwa na vituo vinne tu vya matibabu kwa watoto, lakini sasa kuna zaidi ya vituo 60.
Changamoto zinazoikumba sekta ya afya
Licha ya mafanikio, Profesa Karim anasema bado kuna changamoto katika huduma za watoto. Anahisi watoto hawapewi kipaumbele cha kutosha kwa sababu hawana mchango wa moja kwa moja katika kuingiza mapato. Bajeti ya kununua vifaa vya watoto ni changamoto kwa kuwa vifaa hivi ni ghali, lakini anasisitiza kuwa kuokoa maisha ya watoto ni muhimu zaidi ya gharama hizo.
Mbali na utafiti wa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Profesa Karim anajivunia utafiti wake kuhusu watoto wanaoharisha na matumizi ya dawa ya zinki. Aliweza kubaini kuwa dozi ndogo ya zinki inaweza kupunguza kuharisha bila kusababisha kutapika, na matokeo ya utafiti wake yalitambuliwa na WHO mwaka 2019, ambapo alipewa tuzo barani Ulaya.
Aidha, utafiti wake ulionyesha kuwa watoto wanaoharisha hawahitaji antibiotiki, isipokuwa wale wanaoharisha damu au choo chenye mlenda. Pia amefanya tafiti kuhusu lishe ya watoto wenye uzito pungufu na jinsi ya kuwasaidia wanawake kunyonyesha kwa usahihi, kupitia programu ya mafunzo ya “rectation management” katika hospitali ya Amana.
Profesa Karim ana furaha kuwa tafiti zake zimeleta mabadiliko makubwa katika sera na utoaji wa huduma za afya kwa watoto nchini Tanzania.
Teknolojia, mbinu na mabadiliko ya tiba kwa watoto
Mtaalamu huyo anasema katika tiba ya watoto wachanga, hawahitaji teknolojia za hali ya juu sana, lakini teknolojia zilizopo kama vile mashine za kusaidia kupumua zimeleta mabadiliko makubwa.
Anasema licha ya huduma za afya kuimarika nchini, bado hazijafikia kiwango kinachoridhisha, na kuna haja ya kufanya kazi kubwa zaidi.
Profesa huyo, ambaye alistaafu kazi Juni, mwaka huu, anasema hajisikii kutaka kustaafu kwa sababu bado ana hamu ya kuwasaidia watoto. Hata hivyo, amepewa mkataba maalumu wa “Emeritus” ambao utamruhusu kuendelea na kazi hiyo hadi atakapojihisi kuchoka mwenyewe.
Ushirikiano na mataifa mengine
Anasema tafiti mbalimbali zinazofanyika zimewaunganisha na mataifa kama Ujerumani, Marekani na nchi za Kiarabu katika juhudi za kuboresha afya ya watoto.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuweka mkakati wa kuongeza ufadhili kwa madaktari wa kawaida ili waweze kusoma utaalamu maalumu, hasa katika ubingwa wa watoto, kwani mara nyingi Serikali haina fedha za kutosha kuwafadhili.
Kuhusu wafanyakazi wapya katika sekta ya afya, amebainisha kuwa wanapimwa vigezo vyao, lakini changamoto kubwa ni vijana kupendelea mishahara mikubwa na kazi nyepesi.
Hivyo, amesisitiza kuwa mbinu za kuhudumia watoto wenye uzito mdogo zinahitaji kuboreshwa zaidi ili kuongeza ufanisi.
Anasema sera za afya nchini ni nzuri, hata baadhi ya nchi jirani zimekuwa zikinakili sera hizo, lakini changamoto kubwa ni utekelezaji wake.
“Tunazo sera nzuri, lakini bila utekelezaji haina maana. Zinahitaji fedha, ufadhili, na mabadiliko ya fikra,” anasema Profesa Karim.
Aidha, amebainisha kuwa kuboreshwa kwa huduma hospitalini kumehamasisha wanawake wengi kwenda kupata huduma, tofauti na zamani walipoona hakuna umuhimu wa kufanya hivyo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa huduma hizi zinapaswa kuboreshwa zaidi ili kufikia viwango vinavyohitajika.