HEKAYA ZA MLEVI: Kiswahili cha waswahili changamoto

Dar es Salaam, Hivi haikushangazi kuona asilimia kubwa ya wanafunzi wanafaulu masomo ya kigeni kuliko somo la Kiswahili, lugha waliyozaliwa kwao na wanayoitumia wakati wote? Kiswahili ni kigumu sana. 

Unaweza kuwa daktari bingwa baada ya kupata alama ndefu kwenye masomo ya sayansi, lakini ukiulizwa matokeo yako kwenye mtihani wa Kiswahili unaweza kupigana.

Kiswahili si sawa na lugha za asili zilizonyoka. Mtu akisema “ntakuua” kwa kilugha chake kaa naye mbali kwani atainyofoa roho yako. Lakini kwa Kiswahili cha sasa unaelewa nini pale unaposikia “Katika ile shoo mnyama kaua mpaka basi…” 

Hapo hamaanishi kwamba onesho liliingiliwa na dubu, bali mnyama ni nguli na kuua ni kupagawisha (ah! Unaona sasa, kupagawisha ndio nini?).

Kiswahili ni mchanganyiko wa lugha za kibantu zilizochanganywa ili kuwaletea tija watumiaji. 

Ujio wa wakoloni uliongeza maneno mengi ambayo hatukuwahi kuwa nayo. Waajemi kilichangia maneno kadhaa likiwemo “cherehani”, Wareno nao wakatuongezea maneno kama “bendera”, “gereza” na “meza”, Wajerumani “shule” na “hela”, Wahindi “gunia”.

Lakini Waarabu na Waingereza ndiyo waliokijaza Kiswahili kwa maneno mengi zaidi. 
Kutokana na mseto huu wa maneno, Kiswahili kimekuwa kama bendera. Kinakwenda kikichanganya lugha hadi mzungumzaji anajikuta akirudia maneno yaleyale kwenye sentensi moja. 

Wakati mwingine maana ya neno inaweza kubadilika kufuatana na hali iliyopo na aina ya mpokea maneno. Tena maana huweza kubadilika zaidi yakitafsiriwa au kuelezwa na mtu wa tatu kutoka kwa msemaji. 

Enzi zile Profesa Ndumilakuwili aliwahi kuwaingiza watu mjini kwa tafsiri isiyo rasmi. Kitongoji chao kilitembelewa na mtalii wa Kimarekani. Lilikuwa jambo adimu sana hasa kwa wakati ule, hivyo parapanda ikalia kuwakusanya wakazi ili wasalimiane na mgeni. 

Lakini kutokana na uduni wa elimu kwa wakazi wa hapo enzi hizo, ilibidi atafutwe Profesa kama mkalimani. 

Mtalii huyo alijitambulisha na kujieleza kama ifuatavyo (kwenye mabano ni tafsiri kutoka kwa Ndumilakuwili): My name is Livingstone (Jina langu ni Jiwe Linaloishi). 

I was born in New York (Nilizaliwa kwenye Kiini Kipya cha Yai). I visited Johannesburg (Nimetembelea Begi la Yohana). Thank you and see you again (Hapo anasema amefurahi sana na anaomba mumchangie nauli ya kurudi kwao.”

Mzungu akashangaa kuona kapu linasogezwa kando yake na shilingi zinaanza kumiminika humo. Mzungu akashangaa lakini Ndumilakuwili akamtuliza kwa ishara za mikono kumtaka atulie kwanza na ataelezwa maana yake hapo baadaye.

Mwisho wa mchezo Ndumilakuwili akauma kuwili; akalipwa kwenye ukalimani na kutoroka na mchango ule usio rasmi. Huyo ndiye Ndumilakuwili, nyoka anayeuma pande mbili kichwani na mkiani.

Lugha aliyotumia profesa huyu wa uswahilini ni lugha mchanyato. Baadhi ya maneno yalibebeshwa maana isiyo yake na mengine hayakuwa ya kweli. Yote yakamiminwa kwenye chombo kimoja, yakapondwapondwa na kutoa maana ingine kabisa. Waswahili humwita “fundi” mtu wa aina hii.

Mimi si mtaalamu wa fasihi, na ninaamini watumiaji wengi wa lugha si wataalamu wa lugha hizo. Kama nilivyotangulia kueleza hapo mwanzo, pamoja na kuzaliwa katika Kiswahili lakini si ajabu ukapata mwalimu mgeni wa kukufundisha Kiswahili.

Tunachofanya mwanzoni ni kukwepa makosa yanayokwepeka kirahisi. Unapofanya mtihani anza kuyajibu maswali yaliyo rahisi kwanza.

Wataalamu wa sayansi ya lugha (isimu ya lugha) wanakubaliana kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu (bahati) ambazo hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao. Chombo kikipita njiani na kutoa sauti ya “pikipikipiki” bila shaka kitaitwa Pikipiki ili wasihangaike kukitaja.

Kingine cha aina hiyo lakini chenye sauti nzito ya “tukutukutuku” kitachukua jina la Tukutuku. Lakini Kiswahili kina changamoto kutoka lugha mama za Kibantu ambapo baadhi ya herufi huingizwa na mtumiaji kutokana na mazoea ya ulimi wake (mother tang).

Wengi wetu kutoka bara tumezoea “mutu” badala ya “mtu” na “mutoto” badala ya “mtoto”. Wazambia “mbwa” hutamka “umbwa” wakati Wakongo hutamka “mumbwa”. Kule kusini “M” hugeuzwa kuwa “N” na kuleta maneno kama “ntu”, “nti”, “ntoto”, “ntaa” na kadhalika.

Tena kuna wanaotokea Kaskazini mwa Tanzania hutamka “Hosiptali” badala ya “Hospitali”. Wengine husema “kusheherekea” badala ya “kusherehekea”. Mtindo wa uongeaji wa watu wa Pwani huharibu kabisa maana ya sentensi wanaposema “toka nje” badala ya “toka ndani” (ili uende nje). 

Au “kaondoka Mbagala” badala ya “kaenda Mbagala”.  Pia kuna usemi wa “nimemkuta hayupo” badala ya “sijamkuta”. Wengine hawajui tofauti ya umoja na wingi. utasikia “Hii nyimbo” badala ya “Huu wimbo”. 

Tofautisha kati ya “wimbo wa asili” na “nyimbo za asili”. Au unaposikia “Kwa niaba yangu mwenyewe” fahamu kuwa “niaba” ni neno la uwakilishi kwa asiyekuwepo.

Huwezi kusimama na kujiwakilisha mwenyewe. Hii haitofautiani na sentensi ya “Atapita barabara ya Nyerere Road”. Barabara na road ni kitu kilekile.  Mwenzenu mmoja alijitetea mahakamani kwa kusema.

“Mimi nakataa katakata kwamba sijaiba.” Matokeo yake alifungwa kwa sababu kukataa kufanya na kukataa kutofanya ni vitu tofauti kabisa. Yeye alikataa kutoiba badala ya kukataa kuiba. Kwa hiyo alikubali kwamba aliiba.
 

Related Posts