Watatu waachiwa huru usafirishaji kilo 21 za heroini

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imewaachia huru washtakiwa watatu walioshtakiwa kwa makosa ya kusafirisha kilo 21.67 za dawa za kulevya aina ya heroini.

Hukumu iliyowaachia huru washtakiwa hao wakazi wa jijini Dar es Salaam imetolewa jana Septemba 20, 2024 na Jaji Sedekia Kisanya aliyesema upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha ushiriki wao katika shitaka hilo.

Walioachiwa huru ni Ramadhan Gumbo, Fahadi Salehe na Ashraf Hamis waliotetewa na mawakili, Abdul Azizi na Nehemia Mkoko katika shauri hilo.

Jamhuri ilidai awali kuwa, Julai 13, 2019 eneo la Mbezi wilayani Kinondoni washitakiwa walikamatwa wakisafirisha kilo 21.67 za heroini kinyume cha sheria.

Tangu mwanzo wa kesi washitakiwa walikana kuhusika na makosa hayo. Upande wa mashitaka ukiongozwa na jopo la mawakili wanne wa Serikali, uliita mashahidi 11 kuthibitisha shitaka hilo.

Mashahidi hao walidai jioni ya Julai 12, 2019 wakiwa doria eneo la Kimara, Malamba Mawili, polisi walipokea taarifa kuhusu nyumba iliyopo Kwembe ikihifadhi dawa za kulevya.

Shahidi wa nne, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Hassan Nasawika na maofisa wenzake wakiwamo wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya, walifuatilia taarifa hizo zilizobainisha huenda mzigo huo ungehamishwa usiku huo.

Amedai walifuatilia na kwenda kwenye nyumba hiyo, wakiongozana na kiongozi wa mtaa, Christina Mgandi aliyekuwa shahidi wa tano ili ashuhudie upekuzi utakaofanywa.

Kwa mujibu wa ushahidi, walipofika walimkuta mlinzi, Hussein Nyundo aliyekuwa shahidi wa sita aliyewaeleza funguo za nyumba alikuwa nazo mmiliki wake anayeishi Ilala Bungoni, Dar es Salaam.

ASP Nasawika alimwagiza shahidi wa tisa na ofisa mwingine kuwatafuta wamiliki wa nyumba akisaidiana na shahidi wa sita ambao asubuhi ya siku iliyofuata walimkamata mshitakiwa wa kwanza (Gumbo) akiwa Ilala Bungoni.

Gumbo alidaiwa kukamatwa nyumbani kwa wazazi wake na baada ya upekuzi hakuna dawa za kulevya zilizopatikana.

Shahidi wa tisa alidai mshitakiwa aliwaelekeza maofisa hao kwa mshitakiwa wa pili (Salehe) aliyekuwa akiishi jirani na hapo. Shahidi wa tisa akawaamuru maofisa wa chini yake kwenda kumkamata.

Saa 5.00 asubuhi Julai 13, 2019 ilidaiwa shahidi wa tisa alirejea Kwembe akiwa na washtakiwa wa kwanza na wa pili, na shahidi wa sita ambaye wakati huo alikuwa mshukiwa na mlinzi katika nyumba iliyodaiwa ni ya washitakiwa.

Gumbo alikuwa na funguo na baada ya upekuzi ilidaiwa kupatikana paketi 22 zilizokuwa na unga laini uliosadikiwa ni kuwa dawa za kulevya.

Inadaiwa wakiwa eneo la tukio, Gumbo alikiri mbele ya shahidi wa nne kuwa alipokea dawa hizo kutoka kwa Abdalah maarufu Dulla mkazi wa Kinondoni.

Shahidi wanne alidai wakiwa doria alipokea taarifa kuhusu Dulla na mtu mwingine, Ashraf Hamis ambaye ni mshitakiwa wa tatu kwamba wanahusika na usafirishaji wa dawa hizo.

Alidai timu hiyo ilikwenda eneo waliloelekezwa na kumkamata mshitakiwa wa tatu, huku Dulla akitoroka.

Kwa mujibu wa ushahidi, shahidi wa nne alimtaka mtuhumiwa huyo awapeleke nyumbani kwake Sinza Palestina walikofika saa 9.00 usiku wakafanya upekuzi.

Imedaiwa walikamata kisanduku walichoshuku kutumika kuhifadhi dawa za kulevya ambacho kilipelekwa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya (ADU) kukihifadhi.

Baada ya Jaji kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka aliwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu.

Gumbo akijitetea alidai alikamatwa Julai 13, 2019 na Wakaguzi wa Polisi, Emanuel Msakuzi na Abdallah Juma nyumbani kwao Ilala Bungoni akituhumiwa kwa wizi wa kimtandao.

Alidai alipokamatwa vitu vyake ikiwamo simu aina ya iPhone X Max na kompyuta mpakato aina ya HP vilichukuliwa na alisafirishwa hadi Arusha ambako aliwekwa mahabusu na baadaye kurejeshwa Dar es Salaam bila utaratibu kufuatwa.

Alidai alikuta dawa za kulevya kwa mara ya kwanza aliposomewa shitaka la kusafirisha dawa hizo alipofikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shitaka hilo.

Alikana mashtaka akidai hata hati ya kukamata mali siyo sahihi na hana uhusiano na nyumba ya Kwembe au magari. Alidai ushahidi dhidi yake ni wa uongo, pia alikana kuwaelekeza polisi kwa mshitakiwa wa pili, Salehe.

Kwa upande wake, Salehe alieleza alikamatwa Julai 13, 2019 eneo la Magomeni Mikumi na maofisa wa polisi waliokuwa wakipeleleza wizi wa vipuri vya pikipiki akapelekwa Kituo cha Polisi Kariakoo.

Baadaye alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi na kuwekwa mahabusu kabla ya kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kushitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya, kosa lililomshangaza akikana kulitenda.

Hamisi, kwa upande wake alisema alikamatwa Mei 29, 2020 akiwa Kinondoni Mkwajuni akishukiwa kuuza gari bovu lakini Juni 12, 2020 akashitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya na kupelekwa gerezani.

Akichambua ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Kisanya alisema anakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi juu ya dosari zilizojitokeza katika ushahidi wa Jamhuri kuhusu eneo la tukio, ambazo alisema ni kubwa na hazitibiki.

Hoja iliyoibuliwa na mawakili wa washitakiwa ilihusu taarifa za kosa kutofautiana na ushahidi uliotolewa mahakamani kuhusu wapi hasa kosa lilitendeka. Taarifa ilisema ni Kwembe wilayani Kinondoni.

Mawakili walisema ushahidi wa mashahidi namba 4, 5, 6, 9 na 11 wa Jamhuri, unaonyesha eneo la tukio liko Wilaya ya Ubungo, wakieleza kuthibitisha eneo ni muhimu hivyo kosa hilo ni kubwa na halitibiki.

Jaji alikubaliana na hoja ya mawakili hao na kwamba licha ya taarifa ya siri waliyopewa haikuweza kuthibitika mahakamani kama washitakiwa walisambaza dawa hizo zinazodaiwa kukamatwa na Polisi.

Jaji alisema washitakiwa  walikuwa hawaishi nyumba iliyokutwa dawa hizo na funguo haitoshi kuthibitisha ushiriki wao katika kosa hilo.

Ushahidi amesema unaonyesha nyumba hiyo ilikuwa imefungwa kamera za usalama (CCTV) na kwamba picha ni sehemu ya vitu vilivyochukuliwa na polisi na zingesaidia kuonyesha uingiaji na utokaji wao wakiwa na vitu vyenye kutia shaka badala yake picha za CCTV hazikutolewa mahakamani kama kielelezo na wala shahidi wa nne na wa tisa hawakutoa taarifa yoyote kuhusu maudhui waliyoyakuta katika kamera hizo au hata kueleza kama hazikuwa zimeunganishwa au la.

Jaji amesema kukosekana kwa ushahidi huo kunatia shaka kesi ya upande wa mashitaka hasa ikizingatiwa kuwa washitakiwa walikana kutenda kosa hilo.

Kutokana na uchambuzi wake, Jamhuri ilishindwa kuthibitisha mashitaka hayo.

Amesema baada ya kuchambua kwa umakini ushahidi kwa ujumla, inathibitisha mashaka yaliyoibuliwa na upande wa utetezi kwamba ushahidi wa upande wa mashitaka ulikuwa dhaifu na chini ya viwango.

Related Posts