Mkotya awa Mwenyekiti Mgombezi Amcos

 

WAKULIMA wa Chama cha ushirika cha msingi cha wakulima wadogo wa mkonge (Amcos), Mgombezi, wamemchagua mwanahabari Khamis Mkotya kuwa Mwenyekiti. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tanga … (endelea).

Uchaguzi huo umefanyika leo katika eneo la Mgombezi lililopo wilayani Korogwe mkoani Tanga, ambapo wajumbe walichagua bodi mpya itakayokaa madarakani kwa miaka mitatu (2024-2027)

Mkotya ambaye ni mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amewashinda wapinzani wake wanne kwa kupata kura 37 kati ya 76 zilizopigwa huku mpinzani wake wa karibu Moses Chawala akipata kura 19 hivyo kuwa Makamu Mwenyekiti.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na afisa ushirika mkuu wa halimashauri ya mji wa Korogwe, Denis Nguruse ambaye aliwataka wanachama kushirikiana ili kujikwamua na matatizo yanayokikumba kilimo cha mkonge.

Khamis Mkotya

Akizungumza wakati akitoa shukuran Mkotya, amesema amedhamiria kukomesha wizi, ubadhirifu, uzembe, mifugo kuingizwa shambani na matatizo ya mashine ya kuchakata mkonge (corona) na gharama kubwa anazotozwa mkulima.

“Ndugu zangu, mkonge ni uchumi wetu nawaombeni tushirikiane kutatua changamoto zinazotukabili ili tupige hatua zaidi na kujikomboa kwenye lindi la umasikini” alisema

Mkotya ameongeza kuwa makato makubwa wanayokatwa wakulima yamechangia kuwakatisha tamaa ya kuendelea na kilimo hicho lakini uongozi wake utapunguza yale yasiyo ya lazima ili mkulima anufaike zaidi.

“Hili la corona nitahakikisha tunalipatia ufumbuzi ikiwezekana tupate mpya ili tuondoe malalamiko ya wakulima kutovuniwa kwa wakati, katika hili tumedhamiria kumnufaisha zaidi mkulima” alisema

Alisema serikali ya awamu ya sita kupitia wizara ya kilimo imejipambanua kuinua sekta ya kilimo ndo maana imetangaza mazao matano ya kimkakati na mkonge ukiwemo

Kuhusu mifugo kuingia mashambani, Mkotya amesema bodi mpya itashirikiana na mamlaka za serikali kuzuia ng’ombe hao wanaoingia katika mashamba ya wakulima na kuharibu mkonge

Naye Makamu Mwenyekiti, Moses Chawala alisema uzoefu alionao katika kilimo cha mkonge na kwa ushirikiano na wenzake anaamini watapiga hatua zaidi.

“Nina imani na Mkotya, tushirikiane tujikwamue kiuchumi. Mkonge ni mali tusikate tamaa kuhudumia mashamba yetu” alisema.

Katika uchaguzi uliofanyika leo, nafasi tano za ujumbe wa bodi ndizo zilizokuwa zikigombewa na waliojitokeza walikuwa saba.

Waliogombea na kura zao kwenye mabano ni Khamis Mkotya (37), Moses Chawala (19), Rehema Majeba (9), Alex Mtama (7), Agustino Mwikalo (5), Dikson Shosi (3) na James Nyari (3).

Baada ya wajumbe kuwachagua wajumbe watano, pia walipiga kura kumchagua mwenyekiti na makamu wake ambapo Mkotya na Chawala waliibuka washindi.

About The Author

Related Posts