Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC kwa sasa wanaishi kwa kupiga hesabu za vidole kabla ya kutetea ubingwa ambao utakuwa wa 30 tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo. Ni wiki tatu za jasho kabla ya Mei 22.
Yanga wapo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 62 baada ya kucheza mechi 24, zimebaki mechi sita kumaliza msimu huku hesabu zao zikiwa ni kukusanya pointi 11 pekee kuanzia sasa ili kutangaza ubingwa bila ya kuangalia matokeo ya washindani wao wa karibu, Azam na Simba.
Ipo hivi; Yanga ina pointi 62 katika mechi sita zilizosalia zenye pointi 18, wakikusanya 11 watafikiwa 73 ambazo hata Azam ikishinda mechi zake zote sita itaishia pointi 72, huku Simba kama ikishinda mechi zote nane itamaliza na pointi 71.
Nafuu zaidi ya Yanga inakuja kutokana na namna ratiba ilivyo kwa wapinzani wake Azam na Simba kwani kuna mchezo unawakutanisha wenyewe na ikitokea matokeo ya sare, basi Yanga itausogelea zaidi ubingwa.
Hesabu za Yanga katika kukusanya pointi 11 zipo ndani ya mechi nne zijazo dhidi ya Mashujaa (ugenini), Kagera Sugar (nyumbani), Mtibwa Sugar (ugenini) na Dodoma Jiji (ugenini). Baada ya hapo, itacheza dhidi ya Tabora United na Tanzania Prisons zote nyumbani.
Rekodi ya Yanga katika uwanja wa nyumbani ni nzuri ikiwa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza wala kutoka sare msimu huu, hivyo mechi tatu za nyumbani zilizosalia kati ya sita kuna asilimia kubwa ikafanya vizuri kulinda rekodi. Achana na zile za ugenini ambazo pia timu hiyo rekodi yake si mbaya.
Ukiangalia mwenendo wa Yanga msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara unawapa nafasi kubwa ya kuendelea kukaa kileleni hadi kubeba ubingwa kwani mpaka sasa timu hiyo imeshuka dimbani mara 24, imeshinda 20, sare mbili na kupoteza mbili. Ndiyo timu iliyoshinda mechi nyingi zaidi. Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, raia wa Argentina, imekuwa haina nyumbani wala ugenini – popote inaweza kuibuka na ushindi.
Rekodi zinaonyesha kwamba Yanga katika mechi sita zilizobaki ilipocheza na timu hizo katika mzunguko wa kwanza ilishinda tano na sare moja, hivyo ilikusanya pointi 16 kati ya 18 ikimaanisha kwamba mwendo wao huo unaweza kuwabeba nyakati hizi za kuwania ubingwa.
Ikitokea Yanga ikashinda mechi zote nne zijazo basi itatangaza ubingwa wake kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma mbele ya wenyeji wao Dodoma Jiji.
Ikifanikiwa katika hilo, itakuwa ni mara ya pili mfululizo Yanga kutangaza ubingwa wa ligi mbele ya Dodoma Jiji, lakini itakuwa ni mara ya kwanza katika misimu mitatu ya karibuni kutangaza ubingwa ugenini.
Msimu wa 2021/22 ambao Yanga ilitwaa ubingwa baada ya Simba kutawala kwa misimu minne mfululizo nyuma, timu hiyo iliifunga Coastal Union mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar na kutangaza ubingwa zikisalia mechi tatu baada ya kufikisha pointi 67 ambazo hazikuweza kufikiwa na wapinzani wake. Mwisho wa msimu ikamaliza na pointi 74.
Msimu uliopita wa 2022/23, Yanga ilitangaza ubingwa Mei 13, 2023 baada ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kufikisha pointi 74 ambazo hazikuweza kufikiwa na wapinzani wake, wakati inatangaza ubingwa zilisalia mechi mbili. Ikamaliza msimu na pointi 78. Msimu huu ikishinda mechi nne zijazo itatangaza ubingwa zikiwa zimesalia mechi mbili.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amezungumzia mbio za ubingwa kwa timu yake akisema wanachokifanya kwa sasa ni kushinda mechi zao bila ya kuangalia wapinzani wanafanya nini.
“Tunapaswa kuzicheza vizuri mechi zetu zilizobaki bila ya kupoteza pointi, tunapaswa kuendelea kuhakikisha tunapata pointi tatu kila mchezo,” anasema Gamondi na kuongeza:
“Siangalii nyuma yaliyopita wala siangalii wapinzani wangu bali ninaiangalia timu yangu, katika kipindi kama hiki sijali wengine wanafanya nini, hiyo ndiyo siri yangu lakini ninawaheshimu wapinzani.”
“Nilichokiona katika Ligi ya Tanzania timu zimeimarika zaidi mzunguko huu wa pili kitu ambacho ni kizuri kwani hiyo inatufanya kupambana zaidi,” alisema kocha huyo ambaye anapambana kuona anashinda ubingwa wake wa kwanza tangu ajiunge na Yanga msimu huu akichukua mikoba ya Kocha Nasreddine Nabi raia wa Tunisia.
Kocha wa Azam FC, Yossouph Dabo anasema katika mechi zilizosalia wanapambana kwa hali na mali kuhakikisha wanafanya maajabu kama ilivyokuwa mechi zilizopita lengo likiwa ni kuwa sehemu nzuri.
“Mechi zilizobaki tunahitaji ushindi wa hali na mali, naendelea kuiandaa timu kufanya maajabu mengine kama tulivyofanya katika michezo iliyopita ikiwemo dhidi ya Yanga, kikubwa tunahitaji kumaliza ligi katika nafasi nzuri ikiwezekana ubingwa,” anasema Dabo.
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda ambaye amekabidhiwa timu hiyo hivi karibuni baada ya timu hiyo kuachana na Abdelhak Benchikha, anasema ana kazi kubwa ya kufanya kukabiliana na changamoto zote zilizopo, lakini atapambana kuona mechi zilizosalia anashinda zote.
“Nimekutana na wenzangu wa benchi la ufundi na kuzifahamu changamoto zilizopo ambazo tunatakiwa kupambana nazo, ninaamini tutafanya vizuri katika mechi zilizobaki, tuombe Mungu. Suala la ubingwa kwetu tusubiri mpaka mwisho kuona hesabu zinasemaje,” anasema Mgunda ambaye katika mechi yake ya kwanza tangu akabidhiwe timu hiyo ameshuhudia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo.