KIKOSI cha Azam kesho Jumapili kinashuka Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam kuivaa Wagosi wa Kaya, Coastal Union mchezo wa Ligi Kuu Bara, huku kocha wa timu hiyo, Rachid Taoussi akisema bado anasikilizia na kujipa muda zaidi akiwa na kikosi hicho, licha ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya KMC, kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, jijini Dar es Salaam siku chache zilizopita.
Taoussi aliyetua Azam hivi karibuni kutoka Morocco alisema anaona timu inazidi kuimarika kadri siku zinavyosonga mbele, lakini anaendelea kujipa muda kwanza kujiweka pazuri zaidi.
“Tuna wachezaji wazuri kiufundi na tuna morali nzuri ya ushindani na kikosi kinaimarika baada ya wachezaji waliokuwa majeruhi na waliokuwa timu za taifa kurejea kikosini,” alisema Taoussi na kuongeza;
“Katika mechi ya kwanza (dhidi ya Pamba Jiji) sikuwa na wachezaji wote, lakini sasa baada ya wiki mbili, timu imeonyesha kile tulichofanya kwenye mazoezi. Wachezaji wameonyesha kukumbuka na kukifanyia kazi vizuri walichojifunza.”
Aliwapongeza kwa kutekeleza maelekezo yake kwa ufanisi, akisisitiza umuhimu wa kuwaweka wachezaji katika nafasi sahihi kwa mujibu wa mfumo.
Pia aliangazia umuhimu wa nidhamu ya kiufundi; “Tunapopoteza mpira, tunarudisha ndani ya sekunde 5-7, na tunapokuwa na mpira, wachezaji wamekuwa wakikaa katika maeneo sahihi na kutengeneza nafasi za kufunga.”
Kuhusu ushindi huo wa 4-0, alisema; “Ni kitu kizuri kwa timu zinazokuja kucheza dhidi yetu, lakini lazima tuwe makini. Hatuwezi kusherehekea ushindi huu na kusahau kazi inayotukabili.” Pia aliwakumbusha wachezaji wanahitaji kufanya kazi kwa bidii kwa mechi zijazo.
“Kila mechi ni tofauti na tunaiheshimu kila timu, lakini lazima tuzingatie jinsi tunavyocheza,” alisema Taoussi.
Alisema anahitaji muda zaidi kuboresha timu na ana matumaini baada ya miezi kadhaa, itakuwa imeimarika zaidi.
Akizungumzia wachezaji chipukizi, alisema; “Lazima pia tutoe nafasi kwa wachezaji vijana kutoka akademi. Ni muhimu kwa maendeleo ya klabu yetu. Tutafanya mabadiliko kadhaa ili kuepuka majeraha kwa wachezaji wanaocheza michezo mfululizo. Ni muhimu kuhakikisha wachezaji wanapata muda wa kupumzika ili wawe tayari kwa mechi zinazokuja.”
Leo kuanzia saa 1:00 usiku, Azam itavaana na Coastal iliyoanza msimu kwa kukusanya pointi moja tu na kupoteza mechi mbili, lakini mapema saa 10:00 jioni maafande wa JKT watakuwa wenyeji wa KMC kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, jijini Dar es Salaam.