Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza inayodhibitiwa na Kundi la Hamas imetoa taarifa hizo siku ya Jumamosi. Shambulizi hilo kwenye shule ya Zeitoun iliyopo kwenye mji wa Gaza pia limewajeruhi watu wengine 30.
Mapema siku ya Jumamosi, Jeshi la Israel lilisema limeishambulia kamandi ya kundi la Hamas, wanayodai ilikuwa imefichwa kwenye jengo ambalo zamani lilikuwa linatumika kama shule.
“Kundi la kigaidi la Hamas linakiuka sheria ya kimataifa kwa kuendesha oparesheni zake ndani ya miundombinu ya kiraia” imesema taarifa ya jeshi la Israel.
Jeshi la Israel kila wakati limekuwa likililaumu kundi la Hamas kwa kufanya shughuli zake kwenye maeneo ya kiraia ndani ya Ukanda wa Gaza, ikiwemo shule na vituo vya Umoja wa Mataifa.
Hezbollah yavurumisha makombora kaskazini mwa Israel
Katika hatua nyingine kundi la wanamgambo la Hezbollah la nchini Lebanon limesema kwamba limefyetua makombora mawili kuelekea kaskazini mwa Israel.
Taarifa hizo zimetolewa katika wakati jeshi la Israel limetangaza kufanya awamu mpya ya mashambulizi ya kuzilenga ngome za Hezbollah.
Kupitia taarifa ya Hezbollah, kundi hilo linaloungwa mkono na Iran limesema limefyatua “makombora aina ya Katyusha” kuzilenga kambi za kijeshi za Israel “ikiwa ni jibu kwa mashambulizi ya Israel” kwenye vijiji na maakazi ya watu kusini mwa Lebanon.
Shirika la habari la AFP limeripoti mashambulizi makali ya Israel kwenye maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon.
Makabiliano hayo yanatokea siku moja baada ya Israel kufanya shambulizi lililomuua kamanda mwandamizi wa Hezbollah Ibrahim Aqil mjini Beirut. Shambulizi hilo la siku ya Ijumaa limesababisha pia vifo vya watu wengine 30.
Kwenye taarifa ya kuthibitisha kifo cha Aqil, ambaye alikuwa akitafutwa na Marekani kwa kuhusika katika ulipuaji wa ubalozi wa Marekani mjini Beirut mwaka 1983, Hezbollah ilimsifu kama “mmoja wa viongozi wake muhimu”.
Itakumbukwa kuwa mwezi Julai mwaka huu shambulio la Israel mjini Beirut lilimuua Fuad Shukr, Mkuu wa Operesheni za kundi na mauaji ya sasa ya kamanda mwandamizi Ibrahim Aqil yameongeza hofu ya kuzuka vita kamili kati ya Hezbollah na Israel.
Miito ya kuzuia vita kusambaa yatolewa katikati ya wasiwasi unaongezeka
Katika hatua nyingine Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa Rosemary DiCarlo amezihimiza nchi zote zilizo na ushawishi juu ya Israel na kundi la Hezbollah kutumia ushawishi huo kuzirai pande hizo hasimu kusitisha mvutano ili kuepusha kutanuka kwa mzozo katika eneo la Mashariki ya Kati.
Bi Rosemary ametahadharisha kuwa iwapo vita kamili vitatokea kati ya Israel na Hezbollah huenda vikasababisha uharibifu mkubwa zaidi kuliko ule ulioshuhudiwa hadi sasa.
Ametoa rai hiyo kwa wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kulipuka kwa vifaa vya mawasiliano vya Hezbollah ambapo watu 37 waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.
Waziri wa mambo ya nje wa Lebanon Abdallah Bou Habib ameilaumu Israel kwa kuhusika na hujuma hiyo na kuongeza kuwa hakuna mtu yoyote duniani aliye salama.
Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon amesema nchi hiyo haina nia ya kuutanua mzozo katika eneo la Mashariki ya Kati lakini haitaruhusu kundi la Hezbollah kuendelea na uchokozi wake.