Wanyofoa sanamu la Nyerere Tabora

Tabora. Katika hali isiyokuwa ya kawaida watu wasiofahamika wamevamia na kuvunja sanamu la Mwalimu Nyerere lililopo mtaa wa Matola, Kata ya Chemchem Manispaa ya Tabora,  ambapo wameondoka na shingo ya sanamu hilo pamoja na mfano wa fimbo aliyokuwa akitembea nayo kiongozi huyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora Richard Abwao, amethibitisha kutokea kwa tukio la kuvunjwa kwa sanamu hiyo na wahalifu kuondoka na baadhi ya vipande vya sanamu hiyo na tayari uchunguzi umeanza ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo.

Picha zikionyesha Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora wakikagua eneo lilipokuwa sanamu la Mwalimu Nyerere kabla ya kuharibiwa na watu ambao hawajafahamika mara moja. Picha na Johnson James

“Tumefika hapa na kukagua eneo la tukio na ni kweli kwamba sanamu hili limeondolewa kutoka kwenye sehemu ambayo lilikuwa limehifadhiwa kwenye mnara wake na baada ya kuondolewa sanamu limevunjika maeneo matatu kichwa kimevunjika, pamoja na kiuno.

“Tunaendelea kuchunguza  kujua limeanguka katika mazingira gani. Kikubwa tunachunguza kujua ni mazingira gani yamesababisha sanamu lifike chini” amesema na kuongeza: “Kwenye eneo la tukio kwenye uchunguzi wa awali tumekuta kipande cha shuka, suruali nyeusi na kipande cha fimbo ambacho kilitengenezwa kwa zege hakipo na uchunguzi tunaofanya utatupa majibu maana changamoto ya eneo husika ni eneo ambalo halina ulinzi, pia hakuna umeme na kwa usiku inakua giza na tukio hili limegundulika asubuhi,” amesema Abwao.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Septemba 21,2024 Rajab Mohamed amesema kuvunjwa kwa sanamu hilo kunaleta fedheha katika mkoa huo,  maana lilipo sanamu hilo ni eneo ambalo ulifanyika mkutano wa kupiga kura tatu za maamuzi ya kutafuta uhuru wa Tanzania mwaka 1958.

“Tabora ni mkoa wa kimkakati na wenye historia lukuki kwa nchi yetu hivyo kuvunjwa kwa sanamu la Mwalimu Julius Nyerere ni fedheha kubwa kwani hatukutegemea kuona likitokea hili. Sanamu hii ilikuwa nembo kwetu watu ambao hawakumuona Nyerere walimuona kupitia sanamu hili kiukweli watu hawa wametukosea.

“Niviombe vyombo vya ulinzi na usalama vinalo jukumu la kuwatafuta wahusika wote na kuwatia nguvuni ili sheria ichukue mkondo wake kwa kuwakamata waliohusika maana sanamu hili ilikua nembo ya mkoa wetu sasa limevunjwa tutawafundisha nini wajukuu zetu? ” amesema

Kwa upande wake,  Elisha Daud mkazi wa Manispaa ya Tabora amesema uwepo wa sanamu hilo ni heshima kubwa kwa Wanyamwezi hivyo kubomolewa kwake imaonyesha namna ambavyo mkoa huo umekosa uzalendo.

Kwa upande wake,  Athuman Kapera ambaye alikuwa kibarua wakati ujenzi wa mnara huo wa sanamu la Mwalimu Nyerere, amesema amesikitika na namna sanamu hilo lilivyovunjwa.

“Nakumbuka mwaka 1984 nilishiriki kujenga huu mnara ambao baadaye iliwekwa sanamu ya Nyerere na nilikuwa kibarua wa kawaida mbele ya mhandisi mmoja ambaye ni Mkenya ambaye simkumbuki vizuri.

Kwa upande wake,  diwani wa kata ya Chemchem Alhaji Kasongo amesema yeye alipata taarifa za kuvunjwa kwa sanamu hilo alfajiri.

“Nilitoka kwenye ibada alfajiri nikawa kwenye kijiwe cha kahawa ndio nikapata taarifa kwamba sanamu la Mwalimu Nyerere limevunjwa na kudondoka chini ndio nikaja haraka…’’ amesema Kasongo.

Related Posts