Kennedy aukubali mziki Singida Black Stars

NAHODHA wa Singida Black Stars, Kenedy Juma amesema licha ya ugumu na ushindani uliopo katika Ligi Kuu Bara lakini wamepambana na kuongoza ligi ikiwemo ushindi katika mechi tatu za ugenini, huku akisisitiza kwamba uwepo wa wachezaji wengi wa kikosi kikosini haumpi presha ya namba.

Singida Black Stars inaongoza Ligi Kuu Bara baada ya kuvuna pointi 12 katika michezo minne ikizifunga Ken Gold, Kagera Sugar, KMC na Pamba Jiji huku ikikabiliwa na mechi mbili ngumu zinazofuata dhidi ya Yanga na JKT Tanzania.

Kennedy aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Simba, alisema wachezaji wana umoja na dhamira ya kuipa ushindi timu yao ndiyo maana mchezaji hata asipoanza wanahamasishana kupambana kupata ushindi.

“Tumeanza ligi salama na tunaongoza ni jambo la kujivunia ligi ni ngumu ndiyo sababu mchezaji ukiwa ndani ama nje ya uwanja ucheze ama usicheze lazima tuhamasishane jamani tupambaneni tushinde,” alisema Kennedy.

Akizungumzia ushindani wa namba ndani ya kikosi hicho, nyota huyo ambaye ameanza katika mchezo mmoja dhidi ya Pamba Jiji, alisema haimpi presha kwa sababu ni kazi ya benchi la ufundi kuamua nani aanze kutokana na mchezo unaowakabili.

“Kocha ndiye anapanga kikosi chake kwahiyo ushindani wa namba huwezi kusema mchezaji uweze kushindania namba lakini mwalimu ndiye anajua leo ampe nani nafasi na kutoa nafasi kwa kila mchezaji, jambo la msingi ni kumuomba Mungu na kupambana kupata alama tatu,” alisema Kennedy.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, alisema siri ya matokeo mazuri wanayoendelea kuyapata kwenye ligi ni kazi na kujituma mazoezini, umoja na ushirikiano kati ya wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi ndani ya klabu hiyo na kufurashia wanachokifanya.

“Kwa sasa tuko kileleni na tunapambana kuhakikisha tunaendelea kubaki hapo juu na hatuna presha, ninachotaka wachezaji wangu wafurahie na kucheza soka la kuvutia na ndicho tunachokifanya sasahivi na pia kuna maeneo ya kuendelea kuboresha,” alisema Aussems.

Related Posts