Mwanza. Viongozi wa dini kamati ya amani Mkoa wa Mwanza, wamelaani vitendo vya mauaji, utekaji, upoteaji na ukatili vinavyoendelea kuripotiwa nchini.
Kamati hiyo iliyokutana leo Jumamosi Septemba 21, 2024 jijini humo wakiadhimisha siku ya amani duniani pia wamevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutokata tamaa na badala yake viendelee kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli Mwanza, Dk Jacob Mutashi amewataka vijana kutojiingiza kwenye mihemko inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani, huku pia akiwataka viongozi wa dini kutokuwa na upande wowote wa kiitikadi.
“Kamati inalaani vitendo vyote vya mauaji, kupotea kwa watu, kutekwa na ukatili wa aina zote na pia kamati imeomba Serikali kutumia nguvu zake zote katika kukomesha matendo hayo ambayo tumelaani,” amesema.
Ameongeza: “Kamati imeviomba vyombo vya ulinzi na usalama kutokata tamaa na kuendelea kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria bila kujali hali zozote,”
Hata hivyo kamati hiyo imewaomba viongozi wa dini kutengeneza ratiba ya kuliombea Taifa huku pia wakiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura linalotarajia kuanza Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu huku wakiepukana na vitendo vya rushwa kipindi cha uchaguzi.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo, Hassan Kabeke amewataka vijana kuacha kufanya uamuzi kwa kukurupuka na badala yake watafakari kwanza na kuchukua tahadhari juu ya mambo wanayoamua. “Vijana ni hazina kubwa, hamna taasisi au kada ambayo inaweza kuimarika bila kundi hili, basi ni muhimu tuwe watu wenye uamuzi sahihi. Tusikurupuke, tuwe watu wa akili za kuambiwa changanya na zako. Chukua tahadhari kwanza kuangalia maisha yako, ya familia yako na maisha ya jamii yako kuwa makini katika kuyaendea mambo,” amesema.
Ameongeza: “Wito wetu kwa Watanzania wote, Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini na waandishi wa habari ni kuhakikisha tunailinda amani ya Tanzania kwa matendo.’’
Naye mjumbe Kamati ya Amani Wilaya ya Nyamagana, Saada Abbas ametoa wito kwa wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kutengeneza kizazi bora kijacho
“Wito wangu kwa wazazi tuige malezi ambayo tulipewa na wazazi wetu sisi wazazi tumejikita sana kutafuta fedha kuliko malezi hali ambayo inayochangia watoto kujilea wenyewe.Wazazi tukiwa mstari wa mbele katika malezi, naamini hata mauaji na ukatili unaoshuhudiwa hautakuwepo,” amesema Saada.