Sababu WPL kusogezwa mbele | Mwanaspoti

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) uliokuwa uanze rasmi Oktoba 2 baada ya mechi za Ngao ya Jamii zilizokuwa zipigwe kuanzia Jumanne ijayo, umesongezwa mbele na sasa itaanza Oktoba 9, huku sababu za kuahirishwa zikiwekwa wazi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Klabu 10 zikiwamo nane zilizosalia msimu uliopita na mbili zilizopanda daraja za Mlandizi Queens na New Heroes Queens, ndizo zitakazoshiriki ligi ya msimu huu na Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema maandalizi ndiyo sababu ya ligi hiyo kusogezwa mbele.

“Mechi za Ngao ya Jamii zilizotakiwa zianze kuchezwa Septemba 24, pia zimesogezwa mbele kwa sababu kuna vitu vilikuwa havijamaliziwa kwa maandalizi yake, hivyo ligi na mechi hizo kwa jumla zitapigwa mwezi ujao,” alisema Ndimbo alipozungumza na Mwanaspoti jana.

Kwa mujibu wa ratiba mpya ya mechi za Ngao ya Jamii sasa zitachezwa kuanzia Oktoba 02 na fainali yake itapigwa Oktoba 5, siku nne kabla ya msimu mpya wa WPL kuanza Oktoba 09 na awali zilipangwa kuanza Septemba 24-27 ikishirikisha timu zilizomaliza nafasi nne za juu msimu uliopita, mabingwa watetezi, Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess na Ceasiaa Queens.

Ratiba inaonyesha Simba ambao pia ni mabingwa watetezi wa Ngao ya Jamii, itacheza na watani zao Yanga Princess iliyomaliza ligi nafasi ya tatu mechi moja ya nusu fainali, huku JKT Queens na Ceasiaa Queens zilizomaliza msimu nafasi ya pili na ya nne zitaumana nusu fainali ya pili.

Related Posts