Serengeti. Jengo la Hosteli katika Shule ya Sekondari Ngoreme wilayani Serengeti lililoshindwa kukamilika kwa takriban miaka saba sasa limekamlika kwa asilimia 98.
Jengo hilo ambalo lilianza kujengwa na umoja wa wanafunzi waliiowahi kusoma shuleni hapo limefikia hatua hiyo baada ya Mkuu wa Mko wa Mara, Evans Mtambi kufanya ziara shuleni hapo Agosti,13 2024 na kutoa muda wa wiki sita kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuhakikisha linakamilika na kuanza kutumika.
Akitoa taarifa ya ukamilishaji wa jengo hilo leo Septemba 21,2024 kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa shule hiyo, Daniel Mgaya amesema baada ya agizo la mkuu huyo wa mkoa, ofisi ya mkurugenzi ilitoa Sh26.6 milioni kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo hilo ambalo kabla ya kukwama ujenzi wake lilikuwa limegharimu zaidi ya Sh78 milioni.
“Kabla ya kutoa kiasi hicho cha fedha ofisi ya mkurugenzi ilituma timu ya wataalamu ikiongozwa na mhandisi wa halmashauri na baada ya kufanya tathmini walibaini ili jengo liweze kukamilika litahitaji zaidi ya Sh26.6 milioni fedha ambazo zilitolewa mara moja na ujenzi kuanza,” amesema
Amesema jengo hilo likikamilika litatumiwa na wanafunzi 80 wa kiume hali ambayo itasaidia kumaliza changamoto ya hosteli za wanafunzi shuleni hapo ambapo hivi sasa wanalazimika kutumia madarasa kwa ajili ya wanafunzi kulala.
Mtambi amesema Serikali inapaswa kushirikiana na wadau ambao wanajitolea kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii, huku akisema kitendo cha halmashauri hiyo kutelekeza jengo hilo kwa miaka saba, huku kukiwa na uhitaji wa hosteli katika shule hiyo sio busara.
“Watu wamejitolea mamilioni ya fedha zao wakajenga jengo hadi kufikia hatua hiyo halafu Serikali inakaa kimya bila kukamilisha wakati kiasi kilichokuwa kinahitajika ni kidogo zaidi ya msaada uliotolewa. Hii sio sawa na haikubaliki lazima tuthamini msaada unaotolewa na wadau,” amesema.
Mtambi amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo ambao hivi sasa ni wiki ya tano na kwamba anaamini baada ya wiki sita alizotoa, jengo hilo litakuwa limekamilika kabisa na kuanza kutumika.
Baadhi ya wananchi wamemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa uamuzi wa kuingilia suala la ujenzi wa hosteli hiyo baada ya kutelekezwa kwa muda mrefu.
“Tulishakata tamaa baada ya jengo kuwepo hapa kwa miaka yote bila kukamilishwa na hata alipotoa maagizo sisi tulijua hakuna kitakachofanyika,” amesema Makori Nyitange.
Naye Veronica Petro amesema ni vema utaratibu ukawekwa namna ambavyo Serikali itakuwa ikikamilisha miradi inayotekelezwa na wananchi, badala ya kuitelekeza hali ambayo inakatisha tamaa na kuonyesha kuwa Serikali haithamini mchango wa wananchi.