Geita. Ukosefu wa ujuzi wa teknolojia umetajwa kuwa moja ya changamoto inayowafanya wajasiriamali kushindwa kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali kupitia mifumo ya kidijitali.
Sababu nyingine ni pamoja na kutorasimisha biashara, ukosefu wa leseni pamoja na kutokuwa kwenye kanzidata, jambo ambalo Serikali imeamua kulipatia ufumbuzi kupitia program mpya ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (Imasa)
Akizungumza wakati wa kutambulisha programu ya Imasa mkoani Geita jana Septemba 20, 2024, Katibu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa, amesema wafanyabiashara wengi hawana ujuzi wa teknolojia hivyo kukosa fursa za kiuchumi kutoka serikalini.
Amesema katika mazingira ya biashara ya kisasa, ujuzi wa teknolojia unachukua nafasi muhimu katika kuleta maendeleo, hivyo kukosekana kwa ujuzi huo kunawafanya wakose uwezo wa kufikia fursa za mikopo, masoko, na fursa nyingine muhimu zinazotolewa na Serikali.
Aidha, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeanzisha programu mpya ya ‘Imarisha Uchumi na Mama Samia’ ambayo inalenga kuwajengea uwezo na kuwapatia wafanyabiashara mafunzo juu ya matumizi ya mifumo ya teknolojia.
Programu hiyo pia inatarajia kuimarisha uchumi wa mjasiriamali kwa kuwasaidia kufanya biashara zenye tija na hivyo kujikwamua kiuchumi.
“Mfano sasa hivi fursa zilizoko serikalini lazima ujue mifumo ukitaka mkopo wa asilimia 10 lazima uingie kwenye mtandao ujisajili, kama ni ununuzi lazima utumie mfumo hii tumeiona kuwa changamoto inayowafanya wakose fursa hata kama wana uhitaji,” amesema Issa.
Issa ametaja fursa zilizopo mkoani ukiwamo hapo kuwa ni uchimbaji madini, uvuvi na kilimo ambazo kupitia program hiyo zitaangaliwa fursa za kipaumbele na kuwajengea wananchi uwezo ili waweze kunufaika nazo.
Kwa upande wake, Mshauri wa Rais wa wanawake na makundi maalum, Sophia Mjema amesema tayari wametembelea mikoa 17 kuona majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyoanzishwa tangu mwaka 2017, wakilenga kuyatambua na kuona jinsi gani yataweza kufanya kazi ya kuwaondoa wananchi kwenye umaskini.
“Majukwaa haya yalianzishwa na Rais Samia akiwa Makamu wa Rais sasa hivi ameona andelee nayo lakini lengo kuu likiwa kuleta mapinduzi ya uchumi kwa kuangalia namna gani ya kuwasaidia wananchi kupitia fursa za kiuchumi zilizopo kwenye eneo lao,” amesema Mjema.
Programu ya Imasa inatarajia kutekelezwa mikoa yote 31 ya Tanzania na kuwafikia wanufaika zaidi ya 62,000 na itakua na awamu tatu na kwa sasa wameanza na kutambua vipaumbele vya kifursa.