Ujenzi barabara ya Iringa – Msembe kilometa 104 kufungua fursa Nyanda za Juu Kusini

Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe inayoelekea kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye urefu wa kilometa 104 kwa kiwango cha lami utakaogharimu Sh142.56 bilioni.

Ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ufungua fursa za kiutalii, kiuchumi na kibiashara kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Utiaji saini mikataba miwili kati ya Wakala ya Barabara (Tanroads) na Mkandarasi wa Ujenzi pamoja na Mhandisi Mshauri umefanyika leo Jumamosi Septemba 21, 2024 katika Uwanja wa Samora Mkoani Iringa na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu  Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile pamoja na viongozi wa CCM, Serikali na wananchi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba.

Akizungumza na wananchi, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroads kuhakikisha anamsimamia mkandarasi kampuni ya  CHICO aliyeshinda zabuni, kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa ubora na viwango na kukamilisha kazi ndani ya muda kwa mujibu wa mkataba.

“Rais Samia Suluhu Hassan anatambua barabara hii ikijengwa itafungua fursa za kiuchumi na kitalii kwa wana Iringa na ametoa fedha maalumu kiasi cha Sh142.56 bilioni ambayo itawezesha barabara kuanza kujengwa mpaka kukamilika fedha inatiririka tu,” amesema Bashungwa.

Bashungwa ameitaja mikakati ya Serikali kwa Mkoa wa Iringa ikiwa ni kuanza manunuzi kwa ajili ya kujenga barabara ya mchepuo ya Iringa – Iringa Bypass kilometa 7.3 pamoja na kuendelea na upanuzi wa mlima kitonga ambapo tayari kazi inaendelea katika kona  tano hatarishi na ujenzi umefikia asilimia 65.

Kwa upande wake Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera na Uratibu William Lukuvi, ameeleza kuwa ujenzi wa  barabara ya Iringa – Msembe ukikamilika kwa kiwango cha lami utafungua uchumi wa wananchi wa Iringa kwa kuwa tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli na hivyo wananchi watashuhudia makampuni mengi ya kitalii yakiongezeka. 

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana ameeleza kuwa kukamilika kujengwa kwa barabara ya Iringa –  Msembe utasaidia kukuza utalii wa  Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hasa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kurahisisha ufikaji wa watalii katika hifadhi hiyo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba ameiomba Serikali kushughulikia mapema suala la fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe kilometa 104 kwa kiwango cha lami ili isiwe kikwazo katika mradi huo.

Related Posts