Dk Mpango ‘awashukia’ watumishi wa Mungu

Arusha. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, ametoa rai kwa viongozi wa dini nchini na barani Afrika kujikita katika misingi ya kidini badala ya hali inayoshuhudiwa sasa, baadhi wakiondoana kwenye nyumba za ibada wakigombea madaraka na rushwa.

Amesema pia wamekuwa wakituhumiana kwa ushirikina, matumizi mabaya ya fedha na mali za kanisa, kuajiriana kwa upendeleo na kuchanganya siasa na dini.

Dk Mpango amesema hayo leo Jumamosi Septemba 21, 2024 kwenye kongamano la nne la Uhuru wa Kidini Barani Afrika lililoongozwa na kaulimbiu isemayo, “Kuishi pamoja kwa amani barani Afrika, tunu isiyopingika ya dhihiri ya kibinadamu.”

Dk Mpango aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kongamano hilo, amesema licha ya umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani ila kiuhalisia siyo jambo rahisi, ni lazima liwe endelevu. Amesema amani inayosemwa katika Biblia, akinukuu kitabu cha Isaya 11:6 siyo rahisi.

Amesema ni jambo muhimu kuheshimiana na kustahimiliana, akiwasihi Watanzania na watu wa Bara la Afrika waache kukashifu wenzao kwa misingi ya kwamba imani yake ni bora kuliko ya mwingine kwa kushirikiana katika shughuli za kijamii na kufikia maridhiano.

Dk Mpango amesema anapoitazama Tanzania na nchi nyingine za Afrika kwa jumla anaona changamoto ya kuishi pamoja kwa amani ina sura mbalimbali.

“Hapa ninapenda na ninaomba nieleweke kuwa, haya nitakayoyasema hayalengi madhehebu yoyote ya dini, hivyo ninaomba radhi kama itaonekana kugusa madhebeu fulani,” amesema.

Dk Mpango amesema kumekuwa na changamoto ya watu wa imani moja ya kidini kushindwa kuishi kwa amani.

Amesema siku hizi imeshuhudiwa ugomvi na vurugu za aina mbalimbali miongoni mwa waumini wa imani moja ikiwamo baadhi ya viongozi wa dini kama vile wachungaji, masheikh, wazee wa kanisa na ma-ustadhi.

“Tunashuhudia viongozi wanaondoana au wanafukuzana kwenye nyumba za ibada, na hata kwenu ndugu zangu Kanisa la Waadventista Wasabato, tunaona kuna nyaraka mbalimbali kwenye mitandao. Mfano ni yule anayejulikana kama jicho la mwewe,” amesema.

“Kwenye nyaraka hizo zimejaa tuhuma nyingi zinazohusisha matumizi mabaya ya fedha na mali za kanisa, kugombea madaraka, kuajiriana kwa upendeleo, rushwa, kukosekana kwa haki kwenye chaguzi na hata katika madhehebu mengine ya dini mambo ni hayo hayo,” amesema.

Dk Mpango amesema, “japo kwa viwango tofauti nako ninaona kuna kuenguana kwenye uongozi, kuhamishwa kutoka kwenye mitaa, usharika, vigango, parokia au misikiti hasa ile yenye sadaka kubwa na kupelekwa kwenye vituo vyenye ‘maokoto’ kidogo. Ninashangazwa zaidi ni kuwepo hata tuhuma za ushirikina.”

Amesema kwa maoni yake baadhi ya mambo hayo yanasababishwa na baadhi ya viongozi kugeuza dini kuwa ajira badala ya utumishi wa Mungu na wakati mwingine tofauti hizo zinatokana na tafsiri tofauti ya maandiko, kila mtu akijiona ndiye mwenye tafsiri sahihi.

“Viongozi wetu wa dini mnayo nafasi na heshima ya pekee katika jamii yetu, hapa Tanzania na katika nchi nyingine zote za Afrika. Kwa unyenyekevu kabisa naomba nitoe rai, watumishi wa Mungu kutafakari mwenendo huu unaozidi kuota mizizi,” amesema.

“Nafikiri jambo muhimu ni kudhibiti tamaa ya mali iliyopitiliza, watu wanataka magari na nyumba za kifahari, fedha, uchu wa madaraka. Sasa mrudi kwenye wito wenu halisi wa kumtumikia Mungu.”

Dk Mpango amesema wana wajibu wa kusemana na kuonyana kwa upendo makanisani au misikitini badala ya kuhamia mitandaoni, kwani wasipofanya hivyo itakuwa vigumu kuhubiri amani wakati wao hawaishi kwa amani.

Amesema baadhi ya viongozi wa dini wamejiambatanisha na chama kimojawapo cha kisiasa na kusababisha maoni yao binafsi ya kisiasa kuonekana ni ya dini au madhehebu anayoongoza, jambo linalosababisha hali ngumu kwa wafuasi wa vyama vingine wanaoabudu sehemu hizo.

“Hili ni jambo la hatari kwa umoja wa kitaifa na linaleta changamoto kubwa katika uhusiano na ushirikiano baina ya Serikali ambayo haina dini na baadhi ya viongozi wa dini wenye mrengo dhahiri wa kisiasa. Wito wangu kutochanganya dini na siasa,” amesema.

Utunzaji mazingira, maadili

Mbali na hayo, amewaomba viongozi wa dini kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa kuwa, mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu zinachangia uharibifu wa mazingira.

Kuhusu maadili mema katika jamii, amesema dini zina mchango mkubwa wa kujenga familia zenye maadili, amewaomba viongozi hao kusimamia suala hilo akieleza jamii isiyokuwa na maadili inakuwa na vitendo viovu.

“Mmomonyoko wa maadili unasababisha ulevi, uasherati, ulawiti, ubakaji, matukio ya mauaji, ubadhirifu wa mali za umma. Shauku ni kuona jamii inayozingatia maadili, viongozi wa dini simamieni hili,” amesema.

Pia, ameomba viongozi hao nchini kupeleka walimu wa dini waliobobea katika shule za msingi na sekondari ili wanafunzi wanapokuwa na vipindi vya dini wapate elimu hiyo muhimu katika kukuza imani na maadili yao.

Awali, ombi hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, akiomba viongozi wa dini nchini kurudisha morali ya kupeleka walimu wa dini shuleni ili kunapokuwa na vipindi vya dini wanafunzi wapate elimu hiyo.

Katika hatua nyingine, Tanzania imekabidhiwa tunu iliyotolewa kwa mara ya kwanza na taasisi inayosimamia uhuru wa dini barani Afrika, baada ya kuonekana kuwa nao tangu Taifa lilipopata uhuru wake mwaka 1961.

Dk Mpango akizungumzia uhuru huo, amesema una misingi yake iliyoasisiwa na waasisi ili kuhakikisha uhuru wa kidini wa watu wa dini zote unatekelezwa na unalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 19 (1).

Amesema nchini katika kukabiliana na kuvunjika kwa amani miongoni mwa jamii kutokana na tofauti za kidini, kuna Kamati ya Maridhiano ya Amani yenye wajumbe kutoka madhehebu yote ya kidini inayoanzia ngazi ya Taifa hadi wilaya.

“Napenda kusisitiza kuwa kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu dini na ustahimilivu wa kidini, kukosa au kunyimwa haki, miiko ya desturi ambazo ni vikwazo kwa wanadamu wengine pamoja na umasikini, vimekuwa vyanzo vya kuvuruga hali ya usalama na utulivu,” amesema.

“Serikali imepokea na itazifanyia kazi changamoto zilizoelezwa hapa ikiwemo usaili na mitihani kufanyika siku ya sabato, baadhi ya changamoto hizi zinahitaji mashauriano na wadau mbalimbali, siyo maamuzi ya Serikali peke yake,” amesema.

Dk Mpango amesema amani ni tunu adhimu kwa Taifa lolote, akisema ipo mifano mingi inayokumbusha kushindwa kuheshimu tofauti za kiimani kunavyoweza kuchochea vita na migogoro katika mataifa mbalimbali na kusababisha vurugu, vifo na kuathiri uchumi na maendeleo kwa nchi nzima kwa ujumla.

Amesema baadhi ya migogoro inayojitokeza barani Afrika inatokana na imani kali za kidini, na taarifa zinaonyesha nusu ya vifo vilivyohusishwa na ugaidi duniani vilitokea eneo la kati la Sahara. Amesema itikadi kali za kidini zimeenea katika nchi nyingine za Afrika zikiwamo Nigeria, Msumbiji, Somalia na Sudan na kusababisha vifo, utekaji na watu kuyakimbia makazi yao.

Dk Mpango pia, amewaomba viongozi wa dini nchini, kuombea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 ili ufanyike katika hali ya amani na utulivu.

Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Jimbo Kuu la Kaskazini, Mark Marekana, amesema kongamano hilo lilianza Septemba 17 hadi 19, 2024 na kuwashirikisha viongozi kutoka nchi 55 za Afrika.

Amesema lengo la kongamano hilo lililoshirikisha wadau mbalimbali nje ya kanisa ni kuhimiza amani, haki za binadamu na uhuru wa kuabudu.

“Tunataka Afrika inayopendana, kuheshimiana na ndiyo maana tukachagua Tanzania kwani ni nchi yenye amani na upendo,” amesema.

Kongamano lilihusisha kada mbalimbali ikiwemo majaji, wanasheria, wanadiplomasia, viongozi wa dini na wengine.

Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya, David Maraga, amesema uhuru wa kuabudu hakuna anayepaswa kumzuia mwingine na kuwa ni jambo linalopaswa kuheshimiwa kuanzia na wenye mamlaka.

“Uhuru wa kuabudu ni haki ambayo inapaswa kutolewa na kila mtu haipaswi kuchukuliwa na yeyote mwenye mamlaka, tumefurahi kutambua Tanzania inatambua na kuwezesha haki hiyo kupitia Katiba yake, kwani nchi nyingine hawaruhusiwi hata kama Katiba inaruhusu hivyo,” amesema Jaji Maraga.

“Tumeshuhudia amani ikivunjika katika nchi zingine, inapaswa kuruhusiwa ili mradi hakuna kuvunja amani,” amesema.

Related Posts