Zahanati Ngorongopa kuwapa kufuta machungu ya wananchi

Liwale. Changamoto ya wakazi wa kijiji cha Ngorongopa ya kutembea umbali mrefu zaidi ya kilomita10 kutafuta huduma ya afya katika kijiji cha Nangirikiti, inakwenda kumalizika mara baada ya kupata Sh50milioni kutoka serikalini kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho.

Leo Jumamosi Septemba 21, 2024 Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati hiyo

Akizungumza mara baada ya kushuhudia uwekaji wa jiwe hilo la msingi mkazi wa kijiji cha Ngorongopa Hawa Abdallah amesema kuwa wanatembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma ya afya katika kijiji cha Nangirikiti.

Amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha wagonjwa  wakiwemo  wajawazito wanachelewa kuanza mahudhurio ya kliniki pamoja na watoto wachanga kutokamilisha ratiba ya chanjo mbalimbali kutokana na kukwepa gharama za usafiri kwenda Zahanati ya Nangirikiti.

“Nina imani kubwa kuwa baada ya zahanati hii kufunguliwa, hatutakuwa na haja ya kutembea umbali mrefu. Wajawazito wataanza kuhudhuria kliniki kwa wakati na hatutolazimika kuwakatiza watoto wetu kupata chanjo zote zinazostahili kama inavyotakiwa, “amesema Abdallah

Naye Salome Alex mkazi wa kijiji cha Nangorongopa ameishukuru  kwa kuwaletea fedha za ujenzi wa zahanati kwani walikuwa wanateseka muda mrefu kufuata huduma katika kijiji kingine.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutujali wananchi wake wa Liwale pamoja na vijiji vyake, kwa kutuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa zahanati nina imani kubwa ujenzi huu utakapokamilika utasaidia kumaliza kero ya huduma ya afya katika kijiji chetu, “amesema Alex

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa Zahanati ya Ngorongopa,  Mtendaji wa Kata ya Ngorongopa Baraka Juguju amesema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo utagharimu kiasi cha Sh50 milioni na utawanufaisha wakazi wapatao 1219.

Jugugu amesema pia kukamilika kwa zahanati hiyo kutaondoa changamoto za huduma ya afya zilizokuwa zinawakabili kwa muda mrefu,hasa huduma ya kujifungua pamoja na huduma ya kliniki ya mama na mtoto.

 “Zahanati hii itakapokamilika itasaidia wakazi wapatao 1219 na itakwenda kuondoa changamoto ya huduma ya afya ambayo wananchi wangu walikuwa wanateseka kwa muda mrefu sana, amesema Juguju

Waziri Dk Jafo amewahakikishia wananchi hao kuwa zahanati hiyo itaanza kutoa huduma mara tu ujenzi wake utakapokamilika ifikapo Novemba 30 mwaka huu.

“Niwahakikishie kuwa tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajiri ya kununulia vifaa tiba na imeshaelekeza wahudumu wa afya watakaokuja kutoa huduma hapa, hivyo zahanati hii itaanza kufanya kazi mara tu ujenzi wake utakapokamilika Novemba 30 mwaka huu,”amesema

Waziri Dk Jafo Waziri Dk Jafo yupo mkoani Lindi kwa ziara maalumu ya kikazi kwa kukagua miradi ya maendeleo na kuweka mawe ya msingi.

Related Posts