Makamu wa Rais Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa tuzo kwa niaba ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa na Uhuru wa kuabudu ikiwa ni nchi ya kwanza barani Afrika kupokea tuzo hiyo Katika Kongamano la Nne la Uhuru wa Kidini la Afrika leo tarehe 21 Septemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akipokelewa na Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda alipowasili katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tayari kwaajili ya kushiriki kwenye Kilele cha Kongamano la Nne la Uhuru wa Kidini la Afrika leo tarehe 21 Septemba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango wamewasili katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda tayari kwaajili ya kushiriki kwenye Kilele cha Kongamano la Nne la Uhuru wa Kidini la Afrika leo tarehe 21 Septemba 2024.
Na. Vero Ignatius, Arusha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa Rai kwa viongozi watafakari mwenendo unaoendelea ambao kwa sasa umeota mizizi, badala yake wandelee kudhibiti Tamaa ya mali iliyopitiliza warudi kwenye wito wao walioitiwa kumtumikia Mungu
Dkt. Mpango ametoa wito huo leo Jumamosi Septemba 21, 2024 wakati alipokuwa akihitimisha Kongamano la nne la Uhuru wa Kidini barani Afrika kwenye Viwanja vya michezo vya Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha, ambapo aliwataka kurudi kwenye utaratibu mzuri wakusemana,kuonyana kwa upendo makanisa na Misikitini badala ya kuanza kuhamia Mitandaoni.
”Kumekuwa na kasumba ya kuenguana kwenye uongozi, Kuhamishwa kutoka kwenye mitaa, usharika Vigango Parokia au Misikiti na haswa ile yenye sadaka kubwa na kupelekwa kwenye vituo vyenye maokoto kidogo,vilevile nashangazwa kumekuwa na tuhuma za ushirikina baadhi ya Mambo haya yanatokana na baadhi ya viongozi wamegeuza Dini kuwa Ajira badala ya utumishi kwa Mungu”alisema Dkt. Mpango
Vilevile aliwataka Viongozi wa Dini Kuzingatia masomo ya dini kwenye ngazi mbalimbali za Elimu kwenye maeneo yao ya kiuongozi kwa kuhakikisha shule zote zinakuwa na waalimu wa dini waliobobea kwani itawasaidia Watoto kukua katika maadili mema pamoja na kumpendeza Mungu.
“Kumekuwa na tuhuma nyingi zinazojumuisha matumizi ya fedha na Mali za kanisa, Misikiti ikiwemo kugombea madaraka kuajiriana kwa upendeleo rushwa na kukosekana kwa haki kwenye katika ngazi za Union conference na field ambapo hata katika madhehebu mwengime ya Dini Mambo ni hayohayo kwa viwango tofauti tofauti rekebisheni mambo haya. Alisema
Kauli ya Makamu wa Rais imekuja baada ya Ombi la Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda kwa Viongozi wa dini, akitaka Morali zaidi kwa Viongozi wa dini katika kutafuta na kuwapanga waalimu wa dini kwenye shule zinazopatikana Mkoani Arusha ili kusaidia katika kukuza maadili mema kwa watoto.
“Nimefanya utafiti katika mkoa wetu,tuna vipindi viwili kwa kila wiki, karibia karibia dakika 80 kwa wiki zilizotengwa kwaajili ya kuwafundisha watoto wetu habari za Mungu lakini moja ya changamoto kubwa tuliyoipata ni kuwa hakuna waalimu wa kufundisha watoto wetu habari za Mungu.” Amesema Mhe. Makonda
Aidha Kongamano la nne la Uhuru wa Kidini Barani Afrika lililokuwa na kaulimbiu isemayo “Kuishi pamoja kwa amani barani Afrika, Tunu isiyopingika ya dhamiri ya binadamu.”ambapo limehuduriwa na Viongozi mbalimbali kutoka katika Bara hilo.