Dau la Elie Mpanzu Simba

KAMA ulidhani ni utani, basi utakuwa unakosea, kwani Wekundu wa Msimbazi, Simba wameamua msimu huu kufanya yao na wakati wowote watamtangaza winga mpya, Elie Mpanzu ambaye inadaiwa amevuta mkwanja wa maana kutoka kwa bilionea wa klabu hiyo, Mohamed ‘MO’ Dewji ili kumwaga wino.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa la kwanza kuripoti juu ya dili la Mkongomani huyo aliyekuwa akiviziwa pia na Yanga, alitua majuzi jijini  Dar usiku kimyakimya kumalizana na Simba na dili hilo limetiki na kwa sasa anasubiri dirisha dogo lifunguliwe ili aanze kufanya mambo na kikosi hicho.

Winga huyo ametua Simba akiwa mchezaji huru baada ya mkataba aliokuwa nao na AS Vita ya kwao, DR Congo kumalizika huku akiwa amekwama kwenye mipango ya kutua KRC Genk ya Ubelgiji alikokuwa amekwenda alipoipotezea Simba iliyomtaka dirisha kubwa lililofungwa Agosti 16, mwaka huu.

Lakini, taarifa zaidi zikufikie na ambazo Mwanaspoti imezinasa zinaeleza kwamba Mpanzu amesaini mkataba wa kuwatumikia Wekundu hao kwa miaka miwili, lakini siyo kwa mkwanja wa kitoto kwa sababu atachukua Sh782 milioni katika klabu hiyo kutokana na  dili hilo nono alilosaini mbele ya MO na msaidizi wake, Salim Abdallah ‘Try Again.

Inaelezwa, MO amemnasa Mpanzu akiipiga bao Yanga kwa kumpa dau la Dola 200,000 (zaidi ya Sh543.3 milioni) kwa miaka miwili na kila mwaka atachukua Dola 100,000 (Sh272 milioni).

Hata hivyo, ndani ya Dola 200,000 Mwanaspoti linafahamu Mpanzu atachukua Dola 120,000 (Sh326 milioni), huku kiasi kinachosalia Dola 80,000 (Sh217 millioni) zitakwenda kwa rais anayemmiliki.

Kama hufahamu ni mbali na wachezaji Wakongomani kuwa kwenye klabu, wanamilikiwa na viongozi wao wanaowasimamia ambao katika mauzo yao lazima wapate mgao wao.

Wamiliki hao ndio waliochelewesha dili la Mpanzu kutua Simba, wakati akiwa bado na mkataba na AS Vita na klabu na vigogo hao walikuwa wakihitaji pesa ndefu, hatua ambayo wekundu hao waliona ni gharama kubwa.

Taarifa hizo zinafichua, Simba imekubaliana na Mpanzu mshahara wa Dola 7,000 kwa mwezi (Sh19 milioni) na kwa miaka miwili winga huyo atachukua Sh456 millioni ndani ya klabu hiyo.

Mapema Rais wa AS Vita, Amadou Diaby alifichua kukwama kwa dili la Mpanzu nchini Ubelgiji, na kurejea tena klabuni hapo ni kama aliwazingua.

“Wakati naingia klabuni hapa nilikuta Elie (Mpanzu) analipwa Dola 500 (kama Sh1.3 milioni) kwa mwezi na mkataba wake ukikaribia kuisha, hivyo nikamshawishi aongeze mpya na kumwongezea dau hadi Dola 3,500 lakini akagoma,” alikaririwa Diaby na kuongeza:

“Baadaye niligundua ana ofa ya Dola 6,000 kutoka klabu nyingine, hivyo nami nikaongeza ofa hadi ikafika Dola 5,000 (Sh13 milioni) kwa mwezi jambo lililomfanya akubali kusalia klabuni, ila kabla hatujasaini naye mkataba nikaambiwa atasaini kama mchezaji wa mkopo.”

Alifafanua Diaby kwa kusema: “Hii ilimaanisha, sisi (Vita) tutakuwa sehemu ya umiliki wa Mpanzu, lakini klabu yenye nguvu ya umiliki wake itabaki kuwa ni ile iliyomlea ya AJ Vainqueurs. Nilipingana na hilo na kuamua kusitisha dili hilo.”

Alisema hilo ndilo lililomfanya Mpanzu kuwa huru na kukimbilia Tanzania kujiunga na Simba kama mchezaji huru.

“Niliona siwezi kumlipa mchezaji Dola 50,000 (zaidi ya Sh136) kama ada ya usajili na hapo hapo tuwalipe AJ Vainqueurs Dola 50,000 halafu nimlipe tena mshahara wa Dola 5,000 (Sh13 milioni) akicheza kwa mkopo wa miaka miwili. Ndiyo maana tumeshaachana naye aende anapopataka ila kwa upande wetu tumeshindwa hilo,” alikakariwa rais huyo wa AS Vita na kuilainisha Simba kumnasa winga huyo mahiri.

Related Posts