KOCHA wa Bigman FC, Salhina Mjengwa amesema katika championship wao ni kama ‘Underdog’ lakini iwapo watapata nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara wataitumia vyema, huku akisifia ubora wa kikosi hicho kutokana na mastaa wengi wa ndani na nje ya nchi.
Timu hiyo ambayo zamani ilikuwa inafahamika Mwadui FC ya mkoani Shinyanga, ilianza kwa sare ya mabao 2-2, juzi dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi ya Championship, uliopigwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
“Sisi ni ‘Underdog’, ila tukipata nafasi ya kwenda mbele hatutaacha, kimsingi tuna kikosi imara chenye wachezaji wazoefu na mchanganyiko mdogo wa damu changa, hivyo tutashindana na kila aliyekuwa mbele yetu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mwadui.
Kwa upande wa kipa wa kikosi hicho, Deogratias Munish ‘Dida’ aliyewahi kutamba na timu mbalimbali zikiwemo Simba, Yanga na Azam FC alisema, anajitahidi kuwaelekeza wenzake kama ambavyo yeye alielekezwa na wengine waliomzidi uwezo na uzoefu.
Nyota wengine wapya wa kikosi hicho waliotamba na timu za Simba, Yanga, Azam FC na Kagera Sugar na Namungo FC ni Ally Ally, Mohamed Jafari, Mohamed Issa ‘Banka’, Salum Kanon, Salum Kipaga, Mohamed Kapeta, Steven Dua na Mohamed Ibrahim ‘Mo’.