Sare ya Mashujaa yamtibua Kopunovic  

KOCHA wa Pamba Jiji, Goran Kopunovic, amegeuka mbogo kufuatia nyota wa timu hiyo kushindwa kulinda mabao mawili iliyoyapata kipindi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Goran alisema kuwa hajui kilichotokea katika kipindi cha pili, ambako waliongoza kwa mabao 2-0 hadi kufikia dakika 13  kabla ya mechi kumalizika lakini yakarudishwa yote na mpira kumalizika kwa sare ya 2-2.

“Ni ngumu sana kwangu kuelewa,” alisema Kopunovic akionyesha wazi hasira. “Kila siku naongea kitu kilekile na kuwaambia wachezaji jinsi ya kumaliza mechi. Lakini haijafanyika. Labda mimi si mtu sahihi kwa hii timu.”

Pamba Jiji, ambao walionekana kuwa na wakati mzuri katika kipindi cha kwanza, walijikuta wakianguka kiufundi kipindi cha pili, wakiruhusu wapinzani kurudisha magoli yote mawili kupitia mabadiliko ya kimbinu yaliyofanywa na kocha wa Mashujaa.

“Tumefanya vibaya lazima niseme kwa uwazi, tulitakiwa kuwa makini kila mmoja alitakiwa kufanya kazi yake ipasavyo,” alisema kocha huyo.

Kwa upande mwingine, kocha wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, alionekana kufurahia alama waliyopata, ingawa alikiri kuwa walipanga kushinda mchezo huo. “Tumeshukuru kwa alama moja, lakini lengo letu lilikuwa ni kupata alama tatu. Kipindi cha kwanza hatukuwa kwenye kiwango chetu bora. Tulifanya makosa mengi, hasa kwenye ulinzi, na tukaruhusu magoli mawili kirahisi,” alisema Bares.

Kipindi cha pili kilikuwa tofauti kabisa kwa Mashujaa FC, hasa baada ya Baresi kufanya mabadiliko kadhaa yaliyobadilisha mchezo. “Nilifanya mabadiliko muhimu kipindi cha pili, hasa kwa kumuingiza David Ulomi. Niliona kuwa mechi ilikuwa inamhitaji mtu kama yeye. Alikuwa na njaa ya ushindi, na magoli yake mawili yametupatia alama muhimu.”

Ulomi, aliingia kutokea benchini ndiye aliyeibuka shujaa wa Mashujaa baada ya kufunga mabao hayo mawili ya dakika za ‘jioni’, likiwemo bao la kusawazisha katika dakika za mwisho. Mabao ya Pamba yalifungwa na Saleh Masoud na John Nakibinge.

Related Posts