Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesisitiza maandamano ya maombelezo na amani yaliyopangwa kufanyika kesho Jumatatu Septemba 23, 2024 yapo palepale huku akitaja njia zitakazotumika.
Septemba 11, 2024 Chadema ilitangaza maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika Septemba 23 kulaani matukio ya watu kutekwa na mauaji yakiwemo ya makada wake, hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake David Misime ilitangaza kuyapiga marufuku.
Juzi Ijumaa, hadi leo Jumapili askari polisi wameonekana katika maeneo mbalimbali yakiwemo Ubungo, Mwenge, Ubungo, Kinondoni, Mbagala na Mbezi jijini Dar es Salaam wakifanya doria kwa kutumia magari ya maji, maarufu washawasha.
Jana Jumamosi, Mwananchi lilipomuuliza Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuhusu hali hiyohali alisema ni jambo la kawaida ya masuala ya kiusalama na wanataka waende nayo kwenye mfumo wa kata.
Leo Jumapili Septemba 22, 2024 katika hotuba yake kwa Watanzania aliyoizungumza kwa njia ya X (zamani twitter), Mbowe amewataka Watanzania wenye vyama na wasiokuwa na vyama kujitokeza katika maandamano hayo ya maombolezo na amani yatakayoanza saa tatu asubuhi.
Kwa mujibu wa Mbowe, wameamua kuweka mkazo suala hilo, baada ya maombi ya mahitaji ikiwemo kutaka kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, viongozi waandamizi wa ulinzi na usalama, kama sehemu muhimu ya uwajibikaji.
Amesema jambo jingine waliloliomba ni kurejeshewa kwa viongozi wa chama hicho, waliotekwa kwa nyakati tofauti wakiwa hai au hali ya umauti akiwemo Deusdetith Soka, Dioniz Kipanya, Jacob Mlay na Mbwana Kombo.
“Tulidai Serikali iruhusu uchunguzi huru utakaofanywa na wachunguzi huru kutoka Scotland Yard kwa sababu vyombo vyetu ni sehemu ya washukiwa na tutasubiri hadi Septemba 21, kama hakuna hatua zozote za kutoa mwanga tutafanya maandamano ya maombelezo na amani jijini Dar es Salaam Septemba 23.
“Ndugu Watanzania wenzangu hadi jana Septemba 21 hakuna lolote lililopewa nafasi au kujibiwa kati ya mahitaji yetu, badala yake tumeona askari wa jeshi wengi wakisambazwa wakiwa na silaha, farasi, mbwa,” amesema.
Mbowe amesema kwa mujibu wa sheria, wameandika barua kwa Jeshi la Polisi kueleza nia ya kufanya maandamano ya maombelezo lakini jeshi liliwakatalia badala ya kutoa ulinzi katika mchakato huo.
“Baada ya mashauriano na viongozi wenzangu, tumeamua kuendelea na maandamano ya amani kesho yatakayofanyika kwa njia mbili, ya kwanza ni Ilala Boma hadi Viwanja vya Mnazi Mmoja na njia ya pili itakuwa Magomeni Mapipa hadi Mnazi Mmoja.
“Makutano ya maandamano yatakuwa viwanja vya Mnazi Mmoja, tutakutana wote, ndugu zangu Watanzania tukumbuke maandamano yetu ni ya maombelezo na amani,” amesema Mbowe.
Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai, amesema chama hicho, hakifurahii uvunjifu wa sheria za nchi wala amani kama inavyojaribu kuaminishwa.
Amesema Chadema ipo kwa mujibu wa kifungu 3 (1) ya Katiba ya nchi inayotoa haki ya kujumuika na kukusanyika kupitia ibara ya 20(1) ya Katiba na kifungu cha 11 (4) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, kinachotoa haki kwa chama cha siasa kufanya maandamano kwa kutoa taarifa kwa OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) jambo alilodai lililotekelezwa.
Amesema vitendo vya utekaji vimelitia doa Taifa, akisema matukio hayo yalizua hali tete baada ya kutekwa kwa mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao Septemba 6,2024 akiwa katika usafiri wa umma eneo Kibo Complex Tegeta, Dar es Salaam ambapo alichukuliwa na watu wasiojulikana, lakini kesho yake mwili wake uliokotwa maeneo ya Ununio.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan alilani tukio hilo na kutaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi ili waliohusika wapatikane.