Mbeya. Je, unafahamu kwamba kuna ugonjwa wa wasiwasi? Ndiyo, ni moja ya magonjwa ya afya ya akili na unashika nafasi ya pili kwa kuathiri watu wengi na waathirika wakubwa wanatajwa kuwa wanawake.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba katika kundi la watu 100, watatu kati yao wana na dalili za ugonjwa huo.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na daktari bingwa wa tiba ya afya ya akili katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Stephano Mkakilwa ambaye anaeleza kwa kina kuhusu ugonjwa huo na matibabu yake.
Dk Mkakilwa amesema ugonjwa huo unasababishwa na saikolojia na mwenendo wa maisha katika jamii (malezi na makuzi).
Amesema katika takwimu za dunia, wanawake ndiyo wanaathirika zaidi ukilinganisha na wanaume kutokana na kushindwa kuvumilia na kupata mfadhaiko tofauti na wanaume.
“Hata hapa Tanzania, wagonjwa wengi ni kina mama kwa sababu ya mapokeo ya hali, wao ni rahisi sana kupatwa jambo wakapata mfadhaiko, tofauti na wanaume wanaoweza kuvumilia.
“Mwanaume mmoja akiwa na ugonjwa huu, basi wanawake kuanzia wawili watakuwa katika hali hiyo, lakini katika kundi la watu 100, watatu kati yao wana dalili za ugonjwa huu,” amesema Dk Mkakilwa.
Anaongeza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa baada ya ugonjwa wa sonona, unaoongoza katika magonjwa ya afya ya akili, wasiwasi ndio unaofuata katika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi.
“Katika hospitali hii, tunapokea si chini ya wagonjwa watano kwa siku ambapo kwa mwezi mmoja utaona tunayo idadi kubwa hadi 150. Huu ni ugonjwa wa pili duniani kuwa na wagonjwa wengi ukitanguliwa na Sonona,” amesema.
Dk Mkakilwa anaeleza kuwa ugonjwa wa wasiwasi ni hali inayompata mtu anayetarajia kupatwa na jambo baya hadi kumpa mfadhaiko usio wa kawaida.
Anasema hali hiyo inafuatana na hisia kubwa baada ya tarajio baya la kudumu kwa muda mrefu hadi kushindwa kufanya majukumu yake kwa ufasaha.
“Mtu huyu anaposhindwa kufanya shughuli zake kwa ufasaha kama alivyozoea, hali hiyo humsababishia ugonjwa huo rasmi hadi kukosa utulivu na hata muda mwingine kukosa kujiamini,” amesema Dk Mkakilwa.
Dk Mkakilwa anaeleza kuwa mgonjwa wa wasiwasi anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutimiza majukumu yake ipasavyo tofauti na alivyozoea.
Anasema dalili za ugonjwa huo ni mtu kukosa utulivu ikilinganishwa na hali ya awali, kujisikia kutokwa na kijasho chembamba ambacho ni tofauti na joto la uhalisia kama jua.
Anasema mwingine hujisikia mapigo ya moyo kwenda mbio, hali inayomfanya kufikiria kuushikilia na muda mwingine kifua kubana hadi kukosa pumzi.
“Kwa mantiki hiyo, mtu akijisikia hali hiyo, akili yake humfikirisha kwamba amerogwa, kuwa na mapepo au ni ugonjwa wa kimwili na hufikiria kuwa kuna shida kwenye moyo,” amesema Dk Mkakilwa.
Mtaalamu huyo anaeleza kuwa ugonjwa huo unaweza kusababisha athari nyingine kwa mgonjwa na kujikuta akikumbana na mabadiliko mengine kiafya hadi yatakayompa changamoto zaidi.
Anasema mgonjwa wa wasiwasi anaweza kupata pia ugonjwa wa sonona ambao uko karibu sana na wasiwasi.
“Magonjwa ya wasiwasi yako karibu sana na ugonjwa sonona, lakini mgonjwa hufikiria kujikita katika matumizi ya vilevi ili kujiweka katika hali ya kujiamini baada ya kukosa amani au utulivu.
“Fikra humfanya awaze kuwa kutumia vilevi itamsaidia kumtuliza na muda mwingine kuamua kujikatia tamaa hadi kufikia uamuzi wa kujiua,” amesema Dk Mkakilwa.
Daktari bingwa huyo anafafanua kuwa wagonjwa wa wasiwasi wanaweza kupata tiba na kurejea katika hali zao za kawaida, baada ya kuripoti tatizo lake haraka kwa mtaalamu wa afya ya akili.
Anasema wataalamu wa saikolojia wanaweza kusaidia kurejesha hali ya mgonjwa, lakini kwa matumizi ya dawa sahihi, pia, kushiriki na kujichanganya na jamii.
“Magonjwa haya yanatibika hospitali, kuanzia kwa wanasaikolojia na kuripoti tatizo haraka na kuamua kushirikiana na watu au kuchangamana,” amesema.
Mbobezi huyo wa afya ya akili, anasema ugonjwa huo huanzia zaidi ngazi za malezi na makuzi, ambapo watoto ndio huathirika hadi wanapokuwa watu wazima.
Anasema namna ya kujikinga na ugonjwa huo, lazima watoto kuwekwa karibu na mzazi au mlezi ili kuhakikisha wanaripoti tatizo bila kuwakaripia.
Anasema jamii ina nafasi ya kusaidia mgonjwa mwenye ugonjwa huo kwa kumpa ushirikiano na kutoa taarifa ili kuweza apatiwe tiba.