INAWEZA ikaingia katika vitabu vya rekodi kama mechi rahisi kuliko zote Tanzania imewahi kushinda katika mchezo wa kriketi baada ya kuifunga Mali kwa wiketi 10 katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya kufuzu kombe la dunia kwa kriketi ya mizunguko 20 iliyopigwa katika uwanja wa Dar Gymkhana mwishoni mwa juma.
Mali wakiwa ni wageni kabisa katika mchezo wa kriketi ndiyo walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 18 tu baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 12 kati ya 20 iliyowekwa.
Tanzania iliweza kujibu vyema alama hizi dhaifu kwa kutengeneza mikimbio 19 bila ya kupoteza wiketi ikiwa imetumia mizunguko 0.5 kati ya 20 na hivyo kuondoka ma ushindi wa wiketi zote 10.
Sanze Kamate na Yacouba Konate ndiyo walocheza vizuri kwa Mali baada kila mmoja wao kutengeneza mikimbio 3 tu.
Sanjay Bom aliyeungusha wiketi 4 za wapinzani,Laksh Snehal na Harsheed Chohan aliyepata wiketi 2, walichangia sana kuifanya Tanzania ishinde kirahisi mchezo huo.
Katika mechi nyiongine ya ufunguzi, Ghana iliwafunga Cameroon kwa wiketi 8 katika mchezo uliopigwa katika uwanja UDSM jijini.
Cameroon ndiyo walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 40 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 14 kati ya 20.
Wakitumia mizunguko 8 tu, Ghana waliweza kuzifikia alama za wapinzani wao kwa kupata mikimbio 41 huku wakipoteza wiketi 2 na hivyo kutakata na ushindi wa wiketi 8.
Kofi Bagabena aliyetengeneza mikimbio 10 na Vincent Ateak aliyeongezea mikimbio 9 walikuwa ni mssada mkubwa kwa ushindi wa Ghana katika mechi hiyo.
Mechi ya tatu kati ya Malawi na Lesotho ndiyo iliyoongoza kwa wingi wa mikimbio baada ya Malawi kuifunga Lesotho kwa mikimbio 92 katika uwanja wa UDSM.
Wakiwa wamepata kura ya kuanza, Malawi walifanikiwa kutengeneza mikimbio 144 baada ya kumaliza mizunguko yote 20 wakiwa wamepoteza wiketi 4.
Alama hizo zilikuwa ni mlima mrefu sana kwa Lesotho, kwani jitihada zao ziligota kwenye mikimbio 52 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 14 kati ya 20, na hivyo kuwafanya Malawi wajivune kwa ushindo mnono wa mikimbio 92.
Nyota wa mikimbio katika mechi hiyo alikuwa Sami Mohammad Sohail wa Malawi ambaye peke yake alitengeneza mikimbio 61.