Songwe. Kwa miaka tisa sasa, Pascolina Mgala, binti mwenye miaka 20 kutoka kijiji cha Nambinzo wilayani Mbozi, mkoani hapa amekuwa akiishi na uvimbe wa ajabu mguuni baada ya kupata jeraha dogo lililotokana na kujikwaa mwaka 2015.
Pamoja na juhudi mbalimbali za kutafuta matibabu, amekosa msaada wa Sh200,000 kwa ajili ya operesheni ya pili na kuendelea kuishi na mateso ya maumivu.
Hali hii imesababisha atelekezwe na ndugu zake huku mzigo wa kumuhudumia ukibebwa na bibi yake, Layness Mwampashi (77), ambapo baba yake alishafariki dunia.
Safari ya maumivu, changamoto za matibabu
Ilikuwa Aprili 16, 2015, Pascolina anasema alijikwaa wakati akitoka dukani na kupata jeraha ambalo alidhani ni la kawaida ambalo lingepona haraka.
Lakini anasema kadri siku zilivyokuwa zikienda, hali ilizidi kubadilikia kwa mguu wake kuzidi kuvimba tofauti na kipele kilichokuwa kimejitokeza baada ya kujikwaa.
Licha ya machungu yote aliyokuwa akiyapitia, binti huyu anasema hakukata tamaa ya kwenda shuleni. Alikuwa anasoma Shule ya Msingi Mageuzi darasa la nne wakati ameumia.
Pascolina alihitimu elimu ya msingi akiwa na jeraha hilo na alifanikiwa kufaulu na kujiunga na Shule ya Sekondari Malama ambako safari yake ya elimu ilikatishwa akiwa kidato cha kwanza, baada ya kuzidiwa na ugonjwa. Kama asingeandamwa na ugonjwa huo, ilikuwa ahitimu mwaka huu 2024.
Anasema “Nikawa najikuna kawaida pale palipokuwa na kidonda cha kujikwaa, pakawa panaonekana kama panapona, lakini kadri siku zilivyokuwa zinaenda, nikawa nahisi mabadiliko kwenye mguu wangu, ukawa unavimba, baadaye bibi alinipeleka hospitali hapa kijijini,” anasimulia binti huyo.
Anasema hospitali walipobaini ugonjwa ni mkubwa wakampa rufaa ya kwenda kutibiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ambako alifanyiwa upasuaji na eneo aliloumia walitoa kijiwe.
“Ila baada ya mwezi mmoja kupita, nyuzi za kidonda zilifumuka, kwa kuwa hatukuwa na hela za kwenda kutibiwa tena, nikakaa tu nyumbani nikawa nasaidiwa tu na bibi na watu wengine, lakini ndiyo mguu ukawa unazidi kuvimba na kidonda nacho kikawa kinaongezeka ukubwa,” anasema Pascolina.
Lakini anasema mwaka 2019, baada ya hali kuwa mbaya zaidi, bibi yake alimpeleka Hospitali Teule ya Ifisi ambayo iko eneo la Mbalizi.
Anasema baada ya vipimo, alitakiwa afanyiwe upasuaji mwingine na gharama yake waliambiwa ni Sh200,000.
“Ukumbuke muda wote huo nilikuwa naugulia tu maumivu nyumbani, sina msaada wowote,” anasema.
Akizungumza kwa kujiamini, Pascolina anasema amepitia maisha magumu kutokana na ugonjwa huo, hata kufikia kunyanyapaliwa na watu ambao walitakiwa kuwa karibu naye kumfariji.
Anasema mama yake mzazi ambaye kwa sasa anaishi Chunya, kuna kipindi alisikia namna anavyoishi maisha magumu huku akiumwa.
“Aliamua kuja kunichukua ili kikaishi naye, lakini bibi aliwaambia watu kuwa mama ni mwizi wa watoto amekuja kuniiba mimi, alinusurika kushambuliwa na kundi la watu wa hapa kijijini, basi mama hakuweza kunichukua tena akaniacha,” anasema.
Anasema kilichomuokoa mama yake asishambuliwe ni barua aliyoibeba kutoka Chunya.
“Aliwaonyesha kwamba yeye siyo mwizi wa watoto ila ni mama yangu mzazi amekuja kunichukua, ile barua alikabidhi kwa mwenyekiti wa kijiji, mama aliandikiwa na viongozi kutoka Chunya aje aikabidhi kwa mwenyekiti kusudi aruhusiwe kunichukua, wananchi waliposomewa, ndiyo wakaamini wakamuacha na wengine wakawa wanamuambia bibi amuache anichukue, lakini alikataa,” anasema binti huyo.
Anasema mwaka huohuo 2019, baba yake mdogo (jina linahifadhiwa kwa kuwa hajapatikana) alimchukua akakae naye.
Anasema ilishindikana baada ya mkewe kugoma binti huyo asiende kuishi kwao kutokana na matatizo aliyokuwa nayo.
“Kila ndugu, hanitaki, ugonjwa wangu umenifanya nitengwe na sasa niko na bibi tu hata mama hajawahi kurudi tena toka alivyovamiwa siku ile,” anasema Pascolina.
Anamlilia Rais Samia na Watanzania
Pascolina anasema kwa sasa hana uwezo wa kujisaidia mwenyewe na bibi yake, ambaye ndiye mlezi wake, hawezi kumsaidia kutokana na umri wake mkubwa na kushindwa kufanya kazi yoyote.
Ameeleza kuwa hana matumaini ya kesho kwa sababu ya maumivu na changamoto anazopitia kila siku, na sasa anamlilia Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Watanzania kumsaidia.
Bibi yake, Layness ambaye ndiye mlezi wake, anasema wamemuachia Mungu kila kitu, kwa kuwa hata yeye hana msaada wowote. Anasema hata kufika hospitali ni changamoto kutokana na umri wake kuwa mkubwa.
“Walisema nipambane naye, lakini hakuna anayekuja kumwona au kuulizia hali yake. Namuachia Mungu, mimi nimezeeka, sina nguvu,” anasema Layness.
Anasema amekuwa akizunguka na binti huyo hospitalini, “Baba yake amekufa, lakini wazazi wengine waliobaki walimkataa. Nimewaomba waje kumchukua, lakini wanasema tutakuja siku zijazo.”
Uongozi wa Kata na Kijiji
Diwani wa Nambizo, Gilbert Vundwe anasema walimgundua binti huyo hivi karibuni, japokuwa amekuwa akiugua kwa muda mrefu.
Anasema wamepanga kuitisha mkutano wa dharura kujadili hatma ya binti huyo.
Ameongeza kuwa, pamoja na viongozi wa afya ya jamii, watakutana kujadili namna ya kumsaidia kwa michango ya hali na mali.
Mtendaji wa kijiji hicho, Hamis Nsikini anasema hakujua kuhusu mgonjwa huyo hadi alipopewa taarifa.
Ameeleza kuwa ni maumivu makubwa kuona jinsi binti huyo anavyougua na kuhitaji msaada wa haraka.
Sikujua Msukwa, mtoa huduma ngazi ya jamii, anasema alipata taarifa kuhusu mgonjwa huyo kutoka kwa diwani.
Rachel Msonde, mmoja wa majirani, ameeleza kuwa binti huyo ameteseka kwa muda mrefu kutokana na ugumu wa maisha ya mlezi wake. Ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kumsaidia, huku akisisitiza kuwa familia nyingi katika eneo hilo zinakabiliwa na umasikini uliokithiri.