Mwili wa mtoto uliokutwa kwenye mashamba ya miwa Kilombero wazikwa

Kilombero. Mwili wa mtoto Rashmi Abdallah (5), mkazi wa Kijiji cha Katurukila, wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, uliokutwa kwenye mashamba ya miwa wilayani humo, umezikwa katika makaburi ya familia kijijini hapo.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Septemba 22, 2024, Mwenyekiti wa Kijiji cha Katurukila, Jela Meja amesema mtoto huyo na mama yake walifika kijijini hapo Agosti 7, 2024 kwa baba yake mkubwa, Joseph Nyoni, ili mtoto aanze masomo.

Hata hivyo, Septemba 12, 2024 mtoto huyo alitoweka nyumbani wakati akicheza na wenzake.

Meja amesema wazazi walitoa taarifa ofisi ya kitongoji cha Kondo baada ya kumtafuta bila mafanikio.

“Taarifa hizo zilipelekwa ofisi ya kijiji, ambapo walipiga mbiu ya mgambo na kuanza msako wa kumtafuta mtoto katika mashamba, mapori na vijiji jirani, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda,” amesema.

Amesema Septemba 18, 2024 zikiwa zimepita siku sita tangu mtoto huyo apotee, walipata taarifa kuwa mwili wake  umekutwa kwenye mashamba ya miwa yaliyokuwa yameungua moto ukiwa umeungua pia.

Mwenyekiti Meja alibainisha kuwa si tukio la kwanza la watu kutoweka katika eneo hilo, ambapo kuna mwanamke kutoka kijiji jirani aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha na bado hajapatikana mpaka sasa.

Kwa upande wake baba mkubwa wa Rashmi, Joseph Nyoni amesema mtoto huyo alikuja kijijini hapo kwa ajili ya masomo.

Alitoweka siku ya Jumapili, Septemba 12, wakati yeye akiwa kanisani. “Baada ya jitihada za awali za kumtafuta kushindikana, waliripoti tukio hilo kwa ofisi ya kijiji na kuendelea kumtafuta,” amesema.

Nyoni amesema Septemba 18, 2024 alipokea simu iliyoeleza kuwa mwili wa mtoto umepatikana katika mashamba ya miwa ya Kilombero, yakiwa yameungua.

“Niliutambua mwili wa mtoto kupitia kipande cha nguo ambacho kilikuwa kimeungua,” amesema.

Baba huyo ameiomba Serikali ifuatilie tukio hilo kwa kina na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika.

Amesema mtoto huyo alikuwa wa pekee kwa wazazi wake na baba yake mzazi alifariki baada ya mtoto huyo kuzaliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema uchunguzi unaendelea.

Pia ametoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha uchunguzi wa tukio hilo.

Related Posts