Rombo. Wakati Serikali ikitoa hatimiliki za ardhi zaidi ya 250 kwa wananchi katika mji wa Tarakea, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, wananchi hao wameishukuru Serikali huku wakieleza kwamba itapunguza migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao.
Wakizungumza na Mwananchi leo Septemba 22, 2024, wananchi hao wamesema migogoro ya ardhi imekuwa ni kichocheo kikubwa cha matukio ya ukatili wilayani humo na uwepo wa hati hizo utaipunguza kwa baadhi ya familia.
Happness Cosmas, mkazi wa Tarakea, amesema kupatikana kwa hati hizo kutachochea shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye maeneo yao, badala ya kuendeleza migogoro ya ardhi ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.
Amewashauri wananchi ambao maeneo yao bado hayajapimwa kutoa ushirikiano kwa maofisa wa ardhi ili waweze kupata hati hizo kwa haraka.
Kwa upande wake, Godfrey Mwaiyo, mmoja wa wahamasishaji wa urasimishaji wa maeneo wilayani humo, amesema ilikuwa ni ndoto kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kumiliki maeneo yao kisheria, kutolewa kwa hati hizo kutachochea maendeleo ya wananchi wilayani humo pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi kwa.
“Tulianza mwaka 2023 kuupanga mji wa Tarakea na leo tumeweza kupata hati zetu, tunamshukuru mbunge wetu kwa kushirikiana na wananchi wake pamoja na maofisa ardhi,” amesema Mwaiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hata hizo, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala amesema asilimia kubwa ya kero alizozikuta wilayani humo ni migogoro ya ardhi, kutolewa kwa hati hizo kutapunguza changamoto hiyo.
“Asilimia kubwa ya kero nilizokuwa nazipata kwenye mafaili ni ardhi lakini leo zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na maeneo mengi kurasimishwa,” amesema DC Mwangwala.
Amewapongeza wananchi wanaoishi Tarakea kwa kutoa ushirikiano kwa maofisa wa ardhi waliokuwa wakipita katika maeneo yao na hatimaye kufanikisha shughuli hiyo, ambapo wananchi 250 wamepatiwa hati zao.
Akizungumzia umuhimu wa hati hizo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amesema, “hati ni uhai wenu, hivyo ninawaomba Watanzania wote wapime maeneo yao kwa sababu ukishakuwa na hati hata ile migogoro midogomidogo inayojitokeza inakuwa haipo tena,” amesema Pinda.