WATETEZI wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), JKU juzi walitoa dozi ya maana baada ya kifumua Mwenge kwa mabao 9-0 na katika mechi ya upande mmoja ya ligi hiyo, huku nyota wa timu hiyo Mudrik Abdi Shehe akiweka rekodi msimu huu kwa kufunga mabao matano pekee yake.
JKU ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba na kuifanya ifikishe pointi sita na kuchupa kutoka nafasi ya nane hadi kileleni ikiing’oa Malindi yenye alama kama hizo sawa na Uhamiaji, KVZ na Mafunzo kutokana na tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mchezo huo unaokuwa wa kwanza wenye mabao mengi zaidi ikiupiku ule ya Malindi iliyoshinda 4-0 dhidi ya Inter Zanzibar, JKU ilianza kuandika bao dakika ya nane tu ya mchezo kupitia kwa Mudrik, aliyeongeza mengine mawili dakika za 21 na 44 na kuifanya iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Kofi Hamza aliiandika JKU bao la nne dakika ya 64 kabla ya Salum Chubi kutupia bao la tano na Suwedi Juma akatupia chuma cha sita dakika ya 73.
Wakati Mwenge ikijiuliza itayarudisha vipi mabao hayo, Mudrik akawanyong’onyeza kwa kufunga bao la nne kwake na la saba kwa JKU dakika ya 77 na Neva Kaboma akafunga bao la nane dakika ya 85 kabl;a ya Mudrik kupigilia msumari wa mwisho likiwa bao la tano kwake na la tisa kwa timu hiyo dakika ya 90.
Mwenge inayoshiriki ligi hiyo katika nafasi ya jina la Hard Rock, hicho ni kipigo pili katika ligi hiyo ikiwa imeshacheza michezo mitatu hadi sasa na imeporoka kwa nafasi moja ikitoka ya 11 hadi ya 12 ikiwa na pointi tatu ilizopata mechi iliyopita kwa kuinyoa Kipanga kwa mabao 2-1.
Mabao matano aliyofunga Mudrik yamemfanya awe mchezaji wa pili msimu huu kufunga hat trick na kuongoza msimamo wa wafungaji akimuengua Seleman Kibadeni Pwele wa Malindi aliyekuwa wa kwanza kupiga hat trick wakati timu anayoichezea kushinda mabao 4-0 dhidi ya Inter Zanzibar.