‘Bei za nishati ya kupikia vijijini ziangaliwe upya’

Dodoma. Wadau wa mazingira nchini Tanzania wameishauri Serikali, kuanzisha wakala utakaowezesha wakazi wa vijijini kupata nishati safi ya kupikia kwa gharama ya chini kama ilivyo kwa umeme.

Serikali inatekeleza mkakati wa miaka 10, ulioanza mwaka 2024, unaolenga asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Wadau hao wameyasema hayo leo Jumapili, Septemba 22, 2024 katika mdahalo ulioandaliwa na Mtandao wa Policy Forum uliowakutanisha vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za Serikali na wizara.

Akizungumza kwa niaba ya wadau wenzake, Shirika la BBC Action, Faraja Samo amesema gharama za kupata umeme kwa vijijini na mijini ni tofauti na hata namna ambavyo wanavyogharamia kuunganishiwa ni tofauti na wale wa mjini.

Kuunganishiwa umeme  kwa wateja wa vijijini ni Sh27,000 wakati wa mjini ikiwa ni Sh320,000.

“Tunadhani ni vyema vitu kama nishati ya gesi na nyingine za kupikia (safi) kungekuwa na wakala ambaye anaweza kupeleka nishati ya kupikia vijijini kukawa na bei tofauti na mijini,” amesema.

Amesema hiyo inatokana hata athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa vijijini kwa kuwa wanategemea kilimo na mifugo na hata kipato cha wakazi hao kimepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi.

Samo amesema kwa kufanya hivyo kutashawishi watu kutumia nishati safi ya kupikia.

Mwakilishi wa Shirika la Uratibu wa Huduma za Maendeleo (DSC), Laurence Lwanji amesema kinachotakiwa ili kufanikiwa katika mpango huo ni lazima sera na mipango mikakati kuhusu matumizi ya nishati mbadala iendane na hali halisi ya maisha ya watu wa vijijini.

“Tunajua nchi yetu bado masikini na wananchi wengi vijijini wana uwezo mdogo, kwa hiyo suala la bei ndogo ya nishati mbadala ni lazima Serikali iliangalie na liwe la kisera hata katika miongozo ili liweze kutoa unafuu kwa watu wengi kuvutiwa,” amesema.

Amesema bei ya nishati mbadala ikiwa juu, uharibifu wa mazingira utaendelea kwa watu kuendelea kutumia mkaa na kadhalika na kuomba Serikali kuangalia suala la bei iwe rafiki ili kuwavutia watu wengi vijijini.

Aidha, ametaka Serikali za vijiji kuendelea kuhamasisha upandaji na matunzo ya miti inayopandwa katika maeneo yao ili kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Naye Ofisa Misitu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Felister Kagembe amesema Tamisemi inazo shughuli na mikakati iliyojiwekea katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema katika halmashauri 184 nchini, Tamisemi inashirikiana na wadau, taasisi za Serikali, jambo ambalo limewezesha kupanda miti mingi kupitia miradi mbalimbali inayofanyika.

Ofisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Clarance Nkwera amesema juhudi zimekuwa zikifanyika katika ngazi ya Taifa na kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema juhudi zinafanyika kimataifa kwa sababu ukiachana na masuala ya fedha, tafiti zinazofanywa na nchi nyingine dunia zinasaidia katika kutatua changamoto.

Meneja wa uchechemuzi na Ushirikishaji wa Shirika la Policy Forum, Elinami John amesema mdahalo huo ulilenga kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo azaki za kiraia, wadau wa maendeleo na wanasiasa.

Amesema lengo ni kuwakutanisha kuzungumza kuhusu mabadiliko ya tabianchi, changamoto na kama nchi wanaelekea wapi na nini kifanyike ili kuwe na maendeleo, ambayo yatashawishi utekelezaji mzuri wa mikakati na mipango inayolenga kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Related Posts