IDADI ya wachezaji wa Tanzania Prisons kutamani kustaafu soka imeendelea kuongezeka baada ya Salum Kimenya, kuonesha nia ya kutundika daruga ili kugeukia shughuli nyingine nje ya uwanja.
Hata ya Kimenya anayemudu kucheza kama beki na winga wa kulia, imekuja baada ya Benjamin Asukile kutundika daruga tangu kumalizika msimu uliopita na kugeukia ukocha ambapo kwa sasa anaendelea na kozi, huku nahodha wa muda na beki wa kati, Jumanne Elfadhil naye akiwa mbioni kufanya hivyo.
Elfadhil alisema anataka kuachana na soka mwisho wa msimu huu ili kutulia na familia yake kwa kazi za kilimo na biashara.
Wakizungumza na Mwanaspoti, mastaa hao waandamizi kikosini, wamesema baada ya kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu ni muda wao sasa kupisha vijana wengine kuonesha walichonacho mguuni.
Kimenya alisema anatamani baada ya msimu huu aachane na mpira na badala yake ageukie majukumu mengine akibainisha kuwa hata hivyo mpira haikuwa ndoto zake ni kipaji tu kilimbeba.
Alisema pamoja na muda aliodumu uwanjani anajivunia mafanikio mengi na kwamba midhamu na kujituma ndio siri kubwa iliyomfikisha sehemu hiyo kwani amevumilia mengi ikiwamo kudharauliwa wakati akijiunga kikosini humo.
“Mimi nilikaa msimu mzima bila kujua nimesajiliwa nikawa najitolea, nashukuru kwa sasa nafahamika kwa watu wengi, nimepata ajira ambayo imesaidia familia yangu na mimi mwenyewe, Mama yangu hakutaka nicheze mpira niwe msomi kama ndugu zangu.”
“Moja ya mechi ambayo sitaisahau ni dhidi ya Mashujaa msimu uliopita walipotufunga 2-1 Sokoine tukatuhumiwa kuuza hasa sisi wachezaji wakongwe,lakini tulivumilia maisha yakaenda” alisema nyota huyo.
Mkongwe huyo kikosini alisema katika soka lake anavutiwa na kiwango cha beki wa Simba, Shomari Kapombe ambaye amejifunza mengi kwake na amekuwa somo kwa wachezaji wengi wa ndani.
“Nikiwa nje ya uwanja mimi ni Askari kwelikweli hivyo napangilia vyema muda wangu kutegemeana na majukumu ninayopangiwa na wakuu wangu, vijana wavumilie mpira siyo kitu cha mafanikio ya haraka” alisema beki huyo.
Hata hivyo, hakusita kueleza wakati akijitafuta alitendwa sana na wapenzi wake lakini kwa sasa waliomtenga kwa sababu ya ugumu wa maisha wamebaki kuwa marafiki na wanatamani kurejesha upya uhusiano.