Dar es Salaam. Serikali na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzania (TMDA) zimetoa tahadhari ya matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs) kunenepesha mifugo, ikitajwa kuwa ni athari kwa afya ya jamii.
Mbali na usugu unaosababishwa na ARV, utafiti uliofanyika mwaka 2018 ulionyesha kuwa asilimia 90 ya wafugaji wanatumia dawa za antibiotiki kutibu wanyama badala ya chanjo.
TMDA imetoa onyo hilo leo Jumapili, Septemba 22, 2024 ikiwa ni siku mbili tangu wanasayansi, watafiti kukutana kujadili, matumizi holela ya ARV yanavyochangia usugu wa dawa hizo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo imeeleza kuwa mamlaka imepata taarifa juu ya uwepo wa baadhi ya wafugaji wanaotumia vibaya dawa hizo kwa lengo la kunenepesha mifugo yao, akikemea matumizi hayo kwa kuwa yana madhara kwa afya ya jamii.
Kwa upande wake, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema kitendo hicho ni kinyume cha sheria za nchi na suala hilo linaanza kufuatiliwa na Wizara ya Afya na Wizara ya Mifugo na uvuvi kwa pamoja.
“Serikali haikubaliani na hili, yeyote anayefanya hivyo anakiuka kanuni na taratibu, kwa hiyo TMDA wanafuatilia ili kujua nani anafanya na hatua za kisheria zitafuata kwa watakaobainika,” amesema Msasi.
Taarifa ya TMDA imeelezwa kuwa dawa hizo zinatakiwa zitumike kwa ajili ya kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi kwa binadamu baada ya mgonjwa kushauriwa na daktari, hivyo matumizi yake katika kulisha mifugo yanahatarisha afya ya jamii.
“Atakayebainika kufanya hivyo, atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kuharibiwa mifugo yake, kwani itakuwa mazao ya mifugo husika hayafai tena kwa matumizi ya binadamu,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, TMDA imetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa ofisi za TMDA makao makuu na ofisi za kanda zilizopo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Songea, Tabora na Geita.
Septemba 20 mwaka huu, Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Mololo Noah alisema kutokana matumizi hayo holela, Serikali imelazimika kufanya vikao na wadau wa sekta ya afya na mifugo kuweka mikakati ya pamoja kutafuta suluhisho la udhibiti wa matumizi yake na kutoa elimu kwa jamii.
“Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi holela ya ARV kunenepesha kuku na nguruwe, hali inayochangia mlaji kupata madhara ya usugu wa dawa kutokana na wingi wa mabaki ya vimelea kwenye kitoweo,” alisema Dk Noah.
Hata hivyo, alisema bado hawana takwimu kwa sababu wanaendelea kufanya utafiti na sasa wako kwenye kampeni ya mkoa kwa mkoa ambayo wakiimaliza watakuwa na uhalisia wa picha kamili na kutoa taarifa.
Utafiti ulionukuliwa na Mwananchi Septemba 13, 2024 uliotolewa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), ulionyesha asilimia 5.8 ya waviu na wanaotumia dawa, wanakabiliwa na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.
Mtafiti Mwandamizi Kitengo cha Maikrobiolojia na Kinga Muhas, Dk Doreen Kamori alisema walifanya utafiti huo mwaka 2020 katika mikoa 22 ya Tanzania Bara.
Mbali ya ARV kutumika kunenepesha mifugo na kuleta usugu wa dawa, Dk Kamori alisema dawa nyingine zinazotumiwa ni antibiotiki.
Naye Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) Fadhili Hezekiah alisema lazima kuwe na usimamizi wa sheria kwa dawa zinazoathirika na usugu wa vimelea ziweze kujulikana na kufuatiliwa.
Alisisitiza: “Dawa hizi tuhakikishe zinapatikana kwa cheti tu hivyo tutadhibiti usugu, wafamasia wasimamiwe vizuri kwa kufuatiliwa kwa hakika ili kuziuza kwa kuzingatia sheria.”
Alishauri elimu ya kutosha itolewe kwa jamii na si kuhusu usugu wa vimelea bali Watanzania wafundishwe namna sahihi ya matumizi ya dawa.