Dar es Salaam. Hatima ya dhamana ya Meya wa zamani wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai inatarajia kujulikana leo Jumatatu, Septemba 23, 2024, wakati Mahakama itakapotoa uamuzi wa maombi ya Serikali ya kuzuia dhamana yake.
Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa ambaye aliwahi kuwa meya wa Manispaa ya Ubungo anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo kwenye mitandao.
Alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu Alhamisi Septemba 19, 2024 na akasomewa mashitaka mawili, ambayo hata hivyo aliyakana.
Upande wa mashitaka uliowasilishwa na jopo la mawakili wa Serikali lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga uliieleza Mahakama upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hata hivyo, iliwasilisha maombi mawili, la kwanza Mahakama itoe amri ya vifaa vya kielektroniki vya mshitakiwa yaani simu pamoja na akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), viweze kuingiliwa kwa ajili ya upelelezi.
Katika ombi la pili upande wa mashitaka uliiomba Mahakama izuie dhamana yake kwa kile ulichoeleza ni kwa ajili ya usalama wa mshitakiwa.
Wakili Katuga alidai mshitakiwa alimweleza Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kinondoni, Davis Msangi baada ya kutoa taarifa hizo anazotuhumiwa anajua atatekwa na kuuawa.
Hata hivyo, maombi hayo yote mawili yalipingwa na jopo la mawakili wa utetezi lililoongozwa na Peter Kibatala, pamoja na mambo mengine walidai yamewasilishwa kinyume na utaratibu wa matakwa ya kisheria na kwamba kiapo kilichotumika kuwasilisha mahakamani maombi hayo kina kasoro za kisheria.
Sambamba na hoja za kupinga maombi hayo ya Serikali, pia mawakili wa utetezi waliiomba Mahakama impe dhamana mshitakiwa huyo, wakidai ni haki ya Kikatiba ya mshitakiwa.
Hoja hizo za mawakili wa utetezi pia zilipingwa vikali na mawakili wa Serikali, Katuga na Wakili wa Serikali Job Mrema, huku wakisisitiza uhalali na umuhimu wa hoja zao kuhusiana na maombi yao.
Baada ya mvutano mkali wa hoja za kisheria kuhusiana na uhalali wa maombi hayo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo aliahirisha mpaka leo, Jumatatu, Septemba 23, 2024 kwa ajili ya uamuzi.
Hivyo aliamuru pia mshitakiwa Boni Yai aendelee kuhifadhiwa mahabusu mpaka leo atakapotoa uamuzi, ambao ndio utatoa hatima ya dhamana yake.
Hakimu Kiswaga katika uamuzi wake ataamua iwapo hoja za Serikali kuhusiana na maombi ya amri ya vifaa na akaunti ya X ya mshitakiwa kuingiliwa kwa ajili ya upelelezi au la.
Ikiwa Hakimu Kiswaga atakubaliana na hoja za Serikali, atatoa amri kumuelekeza mshitakiwa Boni Yai kutoa nywila (password) za simu zake pamoja na ya akaunti yake ya X ili kumuwezesha mpelelezi kuzifanyia uchunguzi.
Kuhusu maombi ya zuio la dhamana, kama Mahakama itatupilia mbali hoja za Serikali dhamana ya Boni Yai itakuwa wazi na Mahakama itatoa masharti ambayo atapasaa kuyatimiza ili aachiliwe huru kwa dhamana.
Lakini kama Mahakama itakubaliana na hoja za Jamhuri, Boni Yai ataendelea kusota mahabusu kwa muda usiojulikana mpaka hapo sababu za usalama wake zilizoelezwa na Jamhuri zitakapokuwa zimekwisha.
Katika kesi hiyo Boni Yai anakabiliwa na mashitaka mawili yakiwamo kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.
Alisomewa mashitaka hayo na mwendesha mashitaka Wakili wa Serikali, Nurati Manja.
Katika shitaka la kwanza Wakili Manja alidai kuwa , Septemba 12 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar Es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).
Taarifa hizo zinasomeka kuwa, “Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey.”
Katika shitaka la pili Wakili Manja alidai kuwa Boni Yai alitenda kosa hilo Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam akidaiwa kuchapisha taarifa za uwongo zinazowahusisha Wakuu wa Upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.
“Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu …bali Ma-RCO waliokuwa wakiteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi.”
Hii ni mara ya pili Boni Yai kupandishwa kizimbani mwaka huu kwa kesi na mashitaka ya aina hiyo.
Katika kesi ya kwanza anakabiliwa na mashitaka kama hayo na mwenzake Godlisten Malisa.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, wanadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao ya kijamii, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka wanadaiwa kutoa taarifa za uchochezi kuwa Jeshi la Polisi linaua raia, wakilihusisha na kifo cha mwananchi mmoja, Robert Mushi, maarufu kama Baba G na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Arusha, Omari Msamo.