BEKI wa kati Mtanzania, Noela Luhala anayeitumikia ASA Tel Aviv inayoshiriki Ligi ya Wanawake, Israel ni kama amejihakikishia namba kwenye kikosi cha timu hiyo akicheza mechi tano kwa dakika zote 90.
Beki huyo alisajiliwa hivi karibuni akitokea Yanga Princess ambako nako alikuwa ingia toka eneo la beki.
Alianza kwenye michuano ya Athena Cup akicheza mechi tatu kisha kwenye Ligi mechi mbili dhidi ya Hapoel Be’er Sheva timu hiyo ikitoka sare ya 3-3 Septemba 12 na juzi Septemba 19 dhidi ya Hapoel Katamon Jerusalem 0-0 akitumika dakika zote.
Kwa matokeo hayo yanaifanya timu hiyo kusalia nafasi ya sita kati ya nane zinazoshiriki Ligi ya Israel ikikusanya pointi mbili.
Akizungumzia juu ya kupata nafasi ya kucheza Luhala alisema ni kwa sababu amekuwa akipambana na kuaminiwa na kocha.
“Ni kupambana tu kuhakikisha tunaendelea kupata nafasi ya kucheza nyingine juhudi binafsi zinafanya tunaaminiwa na kocha.”