Waziri Prof.Mkenda azindua kituo cha afya kilichogharimu Mil.500 wilayani Wanging’ombe

Wananchi wa kata ya Makoga halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wameishukuru serikali kwa ujenzi wa kituo cha afya kilichogharimu Sh.500 Milioni na kudai kuwa kitawapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ikiwemo za upasuaji kwa wakinamama wajawazito.

Wameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa kituo cha afya Makoga kilichopo wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.

Wanasema uwepo wa kituo hicho cha afya ni naafuu kwao kwani utawapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma za afya.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Makoga akiwemo Lucy Chaula amesema kabla ya kuwepo kwa kituo hicho cha afya wanawake walikuwa wanajifungulia njiani kutokana na umbali wa kufuata huduma ya kujifungua katika hospitali ya Ikonda iliyopo wilayani Makete.

“Tunamshuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupa huu mradi kituo cha afya maana ametupunguzia adha kubwa sana hata mama wajawazito nao wanajaliwa sana” amesema Chaula.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda amesema kwenye kituo hicho cha afya wakina mama wajawazito watapatiwa huduma daraja la kwanza hivyo endapo watapata dharua hawana sababu ya kwenda mpaka Njombe kwa ajili ya kufuata huduma.

“Ukihitaji upasuaji huduma zipo hapa hapa kwenye kituo chetu cha afya kutokana na kazi hii ya Rais ambayo anaifanya nchi nzima” amesema Mkenda.

Amesema kazi inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kupeleka huduma za afya kiwango cha juu ni kielelezo kuwa hataki kuona wananchi hasa wakina mama wanapata huduma hafifu.

Amesema mara nyingi imekuwa rahisi watu kuona na kubeza yale ambayo hayajafanyika lakini kituo hicho cha afya ni kizuri na kina huduma zote zinazohitajika.

Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe Zakaria Mwansasu kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amemuomba waziri Mkenda kufikisha salamu za shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nyingi na inayotekelezwa wilayani Wanging’ombe.

Amesema wananchi wa Kijiji cha Makoga walikuwa wanasubiria kituo cha afya na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh.500 milioni na kituo hicho kimekamilika na kuanza kuhudumia wananchi.

“Wananchi wa Makoga ni wachapa kazi lakini ni waaminifu walizitumia zile milioni mia tano lakini walichangia nguvu zao katika kuchimba mifereji, misingi na majengo haya yamekamilika” amesema Mwansasu.

Mganga Mfawidhi kituo cha afya Makoga Dk. Joseph Chota amesema ujenzi wa kituo hicho cha afya Makoga umegharimu zaidi ya Sh. 500 milioni ikihusisha jengo la mama na mtoto, jengo la maabara, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhi maiti, jengo la kufulia na nyumba ya mtumishi.

Amesema kituo hicho cha afya Makoga kinahudumia wakazi 9941 pamoja na wakutoka vijiji jirani vya Igosi na Ulembwe ambapo wastani wa wagonjwa wanaohudumiwa kwa mwaka ni 2766.

“Wakati wa utekelezaji wa mradi huo wananchi wa kata ya Makoga walishiriki katika ujenzi kwa kuchangia Sh. 11.06 milioni pamoja na kutoa nguvu kazi zao katika kuchimba misingi katika majengo yote” amesema Dk. Chota.

Mbunge wa Wanging’ombe Dk. Festo Dugange amesema miaka minne iliyopita kijiji cha Makoga hakikuwa na majengo ya kituo cha afya kama ilivyo sasa na wananchi walikuwa wanatibiwa katika zahanati ndogo licha ya kuwa kata hiyo ina wananchi wengi.

“Simama hapa mbele ya wananchi hawa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta zaidi ya 500 milioni na kituo cha afya leo kipo na wananchi wameanza kupata huduma hapa” amesema Dugange.

Related Posts